Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu

Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba minne (4) yenye jumla ya euro milioni 118.8 sawa na Sh bilioni 323.4 kwa ajili kutekeleza miradi mbalimbali nchini ikiwemo Awamu ya Pili ya mradi wa nishati jua wa Kishapu mkoani Shinyanga, uendelezaji wa misitu na utunzaji wa hifadhi ya misitu ya mikoko.

Hafla ya utiaji saini wa Mikataba hiyo imefanyika jijini Dar es Salam kati ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dk. Mwigulu Nchemba, kwa upande wa Serikali na Naibu Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Axel-David Guuillon na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Celine Robert.

Akizungumza baada ya kusaini mikataba hiyo, Dk. Nchemba amesema katika mikataba hiyo, euro milioni 75.9 ni kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Nishati ya jua unaotekelezwa Kishapu Mkoani Shinyanga.

Amesema kuwa mradi huo utazalisha Megawati 150 ambapo Awamu ya Kwanza upo katika hatua za utekelezaji na unatarajiwa kuzalisha Megawati 50 na Awamu ya Pili ambayo mkataba wake umesainiwa inatarajiwa kuzalisha Megawati 100 na kufanya jumla ya Megawati zitakazozalishwa kuwa 150.

‘’ Kuingiza Megawati 150 kwenye gridi ya Taifa, kutapunguza utegemezi wa nishati ya nguvu za maji ambayo inaathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Mradi huu utaongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika katika Mkoa wa Shinyanga ambao una umuhimu wa kimkakati wa kiuchumi na kijamii kutokana na kuwepo kwa shuhguli kubwa na ndogondogo za uchimbaji madini” alibainisha Dk. Nchemba.

Amesema mkataba wa pili wa Euro milioni 39.9 ni kwa ajili ya uendelezaji wa mashamba ya misitu na utunzaji wa hifadhi ya mikoko ili kuongeza wigo wa upandaji miti, kuboresha ubora na wingi wa mbegu za miti na kuboresha usimamizi wa mbegu hizo.

Amesema mradi huo utaimarisha vituo vya kukusanya mbegu za miti na kuanzisha vitalu vya kisasa vya miti ikiwa ni pamoja na kutaboresha utunzaji wa hifadhi ya misitu ya mikoko, kuboresha uhifadhi wa uhasilia wa mazingira na kuchangia kuinua utalii na kuboresha maisha ya jamii.

Dk. Nchemba amesema mikataba ya euro milioni 2 ni kwa ajili ya utunzaji wa hifadhi ya mikoko na euro milioni 1 ni kwa ajili ya kufadhili mpangokazi wa jinsia unaotekelezwa na Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO), chini ya mradi wa uendelezaji wa nishati ya jua.

“Huu ni mwendelezo wa ushirikiano wetu mzuri ambao umeshuhudiwa kwa kuwepo kwa miradi mbalimbali ambayo inafadhiliwa kwa mikopo nafuu kutoka Serikali ya Ufaransa kupitia AFD,” amesema Dk. Nchemba.

Amesema kuwa Serikali ya Ufaransa kupitia AFD imefadhili miradi mbalimbali kupitia mikopo nafuu katika sekta za nishati, maji, usafirishaji na kilimo ambayo mingine inaendelea na mingine imekamilika.

Naye Kaimu Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Axel-David Guuillon amesema miradi itakayotekelezwa kupitia mikataba hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa itasaidia kupunguza gharama za kuagiza mafuta pamoja na kuhifadhi mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Celine Robert, amesema kuwa mikataba hiyo ni mwendelezo wa uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Shirika hilo.

“Mabadiliko ya hali ya hewa yapo na yanaathari nyingi siku za usoni, mradi huu wa umeme utaiwezesha Tanzania kukabiliana na tatizo la umeme hususani yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kutunza mazingira” amesema Celine.

Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, amesema fedha hizo zilizosainiwa katika mikataba hiyo zitatumika kupanda miti na kusimamia misitu ya mikoko.

Related Posts