Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitarajia kuzindua Rasimu ya kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Desemba 11, 2024, matamanio na matarajio ya wananchi na wadau yamelala katika maeneo makubwa matano na sekta tano za kufanyiwe kazi ipasavyo.
Maeneo ambayo wanataka yafanyiwe kazi ni kujenga uchumi imara unaostawi na unaoboresha maisha yao, huduma bora za jamii kama elimu na afya, utawala bora, utoaji haki, ulinzi na usalama, maendeleo ya teknolojia na ubunifu, ulinzi na matumizi endelevu ya raslimali za Taifa.
Sekta tano ambazo wametaka zizingatiwe ni kuelekea mwaka 2050 ni kilimo, uzalishaji viwandani (kuongeza thamani), uboreshaji wa miundombinu, huduma bora za jamii na madini, mafuta na gesi.
Hayo yameelezwa leo Desemba 6, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo wakati akizungumza na waandishi na wahariri juu ya hatua iliyofikiwa katika uandaaji Dira ya Maendeleo 2050.
Uzinduzi rasmi kwa mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ulifanyika Aprili 2023 na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.
Akizungumza katika mkutano huo, Profesa Mkumbo amesema kwa kuzingatia maoni ya wananchi na wadau mbalimbali, taarifa za kitafiti na uzoefu kutoka nchi mbalimbali zilizopiga hatua kubwa za kimaendeleo, kamati ya kitaalamu tayari imeandaa rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Rasimu itazinduliwa rasmi Desemba 11, 2024 katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar na mgeni rasmi katika tukio hili atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi,” amesema Profesa Mkumbo.
Amesema uzinduzi wa Rasimu ya Dira 2050 utaenda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya kukusanya maoni ya wadau kwa njia mbalimbali zilizoandaliwa, ambapo watu watapata nafasi ya kusoma kilichopendekezwa na kusema wanachotaka kiboreshwe.
“Zoezi la kukusanya maoni ya uhakiki litahitimishwa Januari 18, 2025 kwa Waziri Mkuu kupokea rasimu ya pili ya Dira 2050 iliyoboreshwa kutokana na maoni ya wadau katika hatua ya uhakiki,” amesema Profesa Mkumbi.
Baada ya hatua hiyo Machi mwakani Rasimu ya Dira 2050 itajadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika vyombo vya Serikali kikiwemo kikao cha makatibu wakuu, Tume ya Taifa ya Mipango na Baraza la Mawaziri.
“Na kati ya Aprili hadi Mei 2025 Rasimu ya Dira 2050 itapokelewa, kujadiliwa na kuidhinishiwa rasmi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuizinduliwa rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Mei au Juni 2025,” amesema Profesa Mkumbo.
Amesema maandalizi ya Dira 2050 yanaenda sambamba na maandalizi ya Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa Maendeleo, utakaotafsiri maono na matamanio yaliyopo katika Dira 2050.
Hadi hatua hii inafikiwa kwa mujibu wa Profesa Kitila, Serikali ilikuwa imekusanya maoni ya wananchi wadau wa maendeleo milioni 1.17 hadi Oktoba 2024.
Wachangiaji hao walitoa maoni kwa njia mbalimbali ikiwemo tafiti katika ngazi ya kaya 15,483, Ujumbe kwa njia ya simu (USSD) 1,118,978, tovuti 13,459, Makongamano 12 yaliyohudhuriwa na watu 22,779.
“Pia kulikuwa na mahojiano mahsusi na ya kina na viongozi mbalimbali waliopo madarakani na waliostaafu wapatao 44, kulikuwa na mikutano ya semina 220 na Nyaraka zilizokusanywa 33,” amesema Profesa Mkumbo.
Dira hii inaandaliwa wakati ambao Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2000-2025, ambayo imekuwa ikiongoza mipango ya maendeleo ya nchi katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.
Profesa Mkumbo amesema mchakato huu wa kuandika Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2050, umezingatia hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa na kuidhinishwa kwa miongozo ya kuandika Dira.
Akizungumza kwa niaba ya vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania Deodatus Balile amesema anapenda kuona Tanzania inayotengeneza mazingira ya Serikali kuwa na ushirikiano mzuri na vyombo vya habari.
“Lazima tuwe na utamaduni wa Serikali kuwafikishia wananchi taarifa, na Serikali kupata taarifa kutoka kwa wananchi,” amesema Balile.
Mbali na ushirikiano huo alisema katika Dira ya mwaka 2050 anatamani kuona Tanzania inayotoa kipaumbele kwa sekta ya viwanda na elimu bora.
“Ili tuweze kulipeleka mbele Taifa letu la Tanzania, lazima Dira ya Taifa iwe chombo kinachounganisha Taifa kwa muktadha kuwa mabadiliko yoyote ya viongozi yasije yakapelekea mabadiliko ya vipaumbele vilivyopo kwenye dira,” amesema.