VYETI VYA WAFAMASIA VITUMIWE NA WAHUSIKA

Na, WAF-Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, ametoa wito kwa wamiliki wa maduka ya dawa kuhakikisha vyeti vya wafamasia vinavyotumika kwenye maduka hayo vimeambatana na uwepo wa wahusika kwa kujiriwa katika maduka hayo.
Akizungumza leo Disemba 04, 2024 wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 54 wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Dkt. Mollel ametoa rai kwa watu kutumia vyeti vya wafamasia kwa waliopo dukani badala ya cheti kinawekwa dukani huku mmiliki au mtaalam husika hapatikani mara kwa mara.
“Kuweka cheti cha mfamasia halafu mtu mwenye cheti hicho hayupo dukani huku cheti kikilipwa pasi na mwenyewe kutokuwepo dukani ni jambo la ajabu kwani tunatakiwa kuwapa fursa ambao hawana ajira ili na wao vyeti vyao vitumike sambamba na kupata ajira,” amesema Dkt. Mollel
Aidha Dkt. Mollel, amewataka wafamasia hao kutumia mkutano huo wa siku tatu kubainisha changamoto pamoja na kuwasilisha mawazo ambayo wataiweesha serikali kuboresha huduma za dawa nchini ili kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na huduma bora.
Mkutano huo uliwakutanisha wafamasia na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kujadili changamoto na mikakati ya kuboresha huduma za famasia nchini.

Related Posts