Wananchi: Mipaka ya msitu Kigosi Myowosi ipimwe upya kudhibiti mauaji

Tabora: Wakazi wa Kijiji cha Mpanda Mlowoka wilayani Kaliua mkoani Tabora wameiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kupima upya mipaka ya hifadhi ya misitu ya taifa ya Kigosi Muyowosi na kijiji chao kwa lengo la kudhibiti mauaji yanayodaiwa kufanywa na askari wa uhifadhi dhidi ya wananchi.

Kauli hiyo imekuja baada ya tukio la Desemba 2, 2024, ambapo askari wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) walidaiwa kumuua mtoto wa shule ya awali Grace Mussa (4) na kumjeruhi Zengo Sandu (27) kufuatia wananchi kuwazingira askari hao, walipokamata trekta lililodhaniwa kuwa lilikuwa likilima ndani ya hifadhi ya misitu ya Kigosi Muyowosi.

Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 6, 2024, mkazi wa kijiji hicho, David Atoti amesema wakazi wa Mpanda Mlowoka wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya migogoro ya ardhi kutokana na kutokujua mipaka ya kijiji na hifadhi, hali inayosababisha taharuki na mauaji.

“Sisi wanakijiji cha Mpanda Mlowoka hatujui mipaka yetu. Tukijaribu kulisha mifugo yetu tunaambiwa tuko hifadhini, tukilima tunaambiwa tuko hifadhini. Hivyo, iko haja kwa Serikali kuhakikisha inaleta wataalamu watuonyeshe mipaka ya kijiji pamoja na hifadhi, maana tunaishi bila amani kwenye kijiji chetu.”

Naye Athuman Mrutu, mkazi wa kijiji hicho, aliunga mkono hoja hiyo, akisema awali Serikali ilipoweka mipaka haikuwashirikisha wananchi, hali ambayo ameieleza kuwa isiyo ya haki.

“Tumekuwa tukiishi na manyanyaso kwa muda mrefu, na viongozi wanatakiwa wajue kwamba hapa kuna watu. Hata bikoni za mipaka walizoweka hatukushirikishwa, na mpaka sasa hatuna maeneo ya kulima wala malisho. Tunaomba mipaka hii irudiwe na wananchi tushiriki,” alisema Mrutu.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Shelembi Nyanda, alisema kijiji kina wakazi zaidi ya 30,000, na hivyo ni muhimu kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kufika kijijini hapo kuweka mipaka upya.

“Bikoni ziliwekwa bila kushirikisha watu. Kila kukicha mizozo haiishi, na kijiji hiki kina watu zaidi ya 30,000. Kwa takwimu, watu hawa ni sawa na kata mbili. Sasa hawa wananchi wangu nitawapeleka wapi? Sehemu ya kulima hakuna, sehemu ya kulisha mifugo yao hakuna. Hivyo, Serikali ifike haraka kwenye kijiji hiki ili haki yetu iweze kupatikana,” alisema Nyanda.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi nchini, Ebrantino Mgiye, ambaye pia ni Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Magharibi, alipozungumzia suala hilo alisema ndani ya siku 10 zoezi la upitiaji upya wa mipaka litakuwa limekamilika.

“Awali, hifadhi ya Kigosi Muyowosi ilikuwa hifadhi ya taifa, lakini Serikali kwa masilahi mapana iliona kuna shughuli za ufugaji wa nyuki zinazotakiwa kufanyika pale, hivyo ikaifanya hifadhi ya misitu. Na kabla ya kuanza kusimamia hifadhi hiyo, tulifanya makabidhiano kwa kuonyeshana mipaka ya hifadhi, na suala hili lilikuwa shirikishi kwa vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi,” alisema.

Aliongeza: “Kwa kuwa wananchi wamesema mipaka hawaifahamu, tunakiri kwamba tutapita upya kuwaonyesha mipaka rasmi, lakini pia tutaendelea kutoa elimu. Najua kuna wanaohama na kuhamia; inawezekana mipaka hawaijui. Ndani ya siku 10 tutakuwa tumemaliza zoezi hilo, na wananchi wataendelea na shughuli zao.”

Related Posts