KAMA wewe ni shabiki wa Yanga na ulikuwa na presha juu ya kikosi cha Yanga kwa ajili ya mchezo wa keshokutwa dhidi ya MC Alger ya Algeria wa Ligi ya Mabingwa Afrika basi tulia.
Yanga inatarajiwa kuwa wageni wa MC Alger inayoshika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Algeria katika pambano la pili la Kundi A baada ya kuanza na kipigo cha mabao 2-0 mbele ya Al Hilal ya Sudan.
Ni kwamba nyota watatu wa Yanga akiwamo kiungo Khaluid Aucho na mabeki Dickson Job na Chadrack Boka walioukosa mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, kwa sasa wamekoleza mzuka baada ya daktari wa timu kuweka wazi kwamba wapo fiti kwa ajili ya kukiwasha Jumamosi dhidi ya MC Alger.
Kwa sasa benchi la ufundi la Yanga chini ya Kocha Sead Ramovic limepumua na kilichobaki kwao ni kusuka mikakati ya kuhakikisha timu hiyo inarudi Dar es Salaam ikiwa na matokeo mazuri dhidi ya MC Alger hapo kesho ikiwa ugenini Algeria.
Yanga iliyopo nchini humo kwa mchezo utakaopigwa kesho ikiikabili MC Alger, lakini taarifa njema ni kuwepo kwa matumaini makubwa ya nyota waliokosekana katika mchezo wa kwanza akiwamo Chadrack Boka kuwepo katika kikosi cha kesho na kumfanya kocha Ramovic achekelee.
Hiyo inatokana na ripoti ya Daktari wa Yanga, Moses Etutu, kusema wachezaji wote waliosafiri wapo vizuri kiafya na kilichobaki ni benchi la ufundi kuangalia nani anafaa kutumika kulingana na mikakati iliyopo.
Kurejea kwa Khalid Aucho, Clement Mzize, Chadrack Boka na Aziz Andabwile ambao walikosekana mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Al Hilal wakati Yanga ikifungwa 2-0, kunamfanya Kocha Sead Ramovic kufumua kikosi chake.
Mbali na nyota hao, pia kuimarika kiafya kwa Dickson Job, ni nafasi nyingine inayowapa Yanga matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo huo utakaoipgwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa 5 July 1962, saa 4 usiku kwa saa za Tanzania wakati Algeria ikiwa saa 2 usiku.
Uwepo wa wachezaji hao, inatoa taswira kwamba kikosi cha Yanga kitakachocheza dhidi ya MC Alger kitakuwa na mabadiliko makubwa sana kulinganisha na kilichoivaa Al Hilal.
Katika mchezo dhidi ya Al Hilal ambao Yanga iliutawala kwa asilimia 63 lakini ikapoteza kwa mabao 2-0, Aucho, Mzize na Boka hawakuwepo huku Job akicheza muda wote lakini alikuja kuumia katika mchezo wa Ligi Kuu Bara wakishinda 2-0 dhidi ya Namungo, akatolewa uwanjani dakika kumi kabla ya mchezo kumalizika.
Wakati Boka alipokosekana, nafasi yake alicheza Nickson Kibabage ambaye alionekana kuwa na makosa mengi ya wazi katika kuzuia na kupandisha mashambulizi huku bao la pili walilofungwa na Al Hilal likipitia upande wake.
Boka anabebwa na mambo mawili, ni mzuri katika kuzuia akitumia urefu wake kukabiliana na wapinzani, lakini pia kasi yake anaitumia vizuri kupandisha mashambulizi yakiwemo ya kushtukiza, pia ni mzuri kupiga krosi chonganishi zinazoweza kuwafanya mabeki wa timu pinzani hata kujifunga.
Duke Abuya alifanya kazi kwa kushirikiana na Mudathir Yahya katika eneo la kiungo cha kati ambapo huwa anacheza Aucho japo nao hawakuwa kwa kiwango cha juu kutokana na muda mwingi kutokuwepo eneo husika hali iliyosababishwa na aina ya uchezaji wao wa kushambulia zaidi kuliko kulinda.
Kwa upande wa Mzize, nafasi yake ya ushambuliaji kuna ushindani huku siku za karibuni Kennedy Musonda akionekana kumshawishi mwalimu licha ya kwamba Prince Dube ndiye alianza dhidi ya Al Hilal. Kurejea kwake ni sehemu tu ya kumpa chaguo Ramovic aanze na nani kati yao akiwemo pia Jean Baleke ambaye ni mshambuliaji mwenye nafasi ndogo zaidi hadi sasa kutokana na takwimu zilivyo akiwa hana bao.
Daktari wa Yanga, Moses Etutu, alisema: “Wachezaji wote wapo vizuri kiafya hata wale waliokuwa na majeraha hapo awali, kilichobaki ni benchi la ufundi kuangalia nani anafaa kwa mujibu wa mipango ya mchezo.”
Wakati kukiwa na matumaini hayo, hali ya hewa yenye baridi kali iliyopo Mji wa Algiers imewalazimu Yanga kufanya mazoezi muda mwingi ili kuizoea kwa haraka.
Kwa sasa katika Mji wa Algiers, hali ya hewa ni nyuzi joto 16 wakati Dar es Salaam ikiwa ni takribani mara mbili yake ikisoma nyuzi joto 30 jambo ambalo kwa Yanga wameamua kukabiliana nayo kibishi.
Mmoja wa watu wa benchi la ufundi la Yanga, amesema: “Program ya mazoezi imepangwa kufanyika kwa takribani saa 3 tukiwa hapa Algeria ingawa siku ya kwanza tulipofika wachezaji walifanya mazoezi mepesi ya kuweka miili sawa ambapo ilikuwa ni uwanjani japo sio ule tutakaochezea mechi.
“Baada ya hapo, ndiyo mbinu za kiufundi zinafuata chini ya Kocha Ramovic akiwa na wasaidizi wake kuhakikisha hakuna kinachotufanya tushindwe kukabiliana na hali ya hewa ambayo ni tofauti na nyumbani Tanzania. Siku moja kabla ya mechi ndiyo tutafanyia kwenye uwanja tutakaochezea ambapo pia program itakuwa ni ileile kama tuliyoanza nayo.”
Kwa upande wa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema: “Baada ya kuwasili Algeria, kikosi kilifanya mazoezi ya kuweka miili sawa kwa mujibu wa mipango ya benchi la ufundi, kisha program zingine kuendelea. Tumekuja hapa Algeria kwa ajili ya kuweka heshima ya klabu yetu ya Yanga.
“Mazoezi yanafanyika saa 2 usiku hapa Algeria ambapo nyumbani ni saa 4 usiku. Tunalazimika kufanya mazoezi muda huo kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa kwani kuna baridi kali sana.”
Yanga ipo Algeria ikiwa na msafara wa watu 53 wakiwemo viongozi wa benchi la ufundi na wachezaji 25 kwa ajili ya mchezo huo utakaochezeshwa na mwamuzi wa kati, Daniel Nii Laryea raia wa Ghana.
Rekidi zinaonyesha kwamba, Yanga hii ni mara ya tatu inakutana na MC Alger katika michuano ya Caf ambapo mara mbili ilikuwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2017. Mechi ya kwanza nyumbani Yanga ilishinda 1-0, ugenini ikafungwa 4-0.
Msimu huu katika Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Hilal inaongoza ikiwa na pointi tatu, MC Alger na TP Mazembe zinafuatia zikiwa na pointi moja wakati Yanga haina kitu ikiburuza mkia.