Yanga yamtisha Kipre JR Algeria

WAKATI wadau wengi wakiibeza Yanga kutokana na mfululizo wa matokeo mabaya waliokuwa nao wakipoteza mechi tatu mbili za Ligi Kuu na moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wenyeji wa MC Alger ya Algeria itakayokuwa wenyeji wa mechi ya kesho, wameingia mchecheto kutokana na uzoefu wa mastaa wao.

Yanga itashuka uwanjani kesho saa 4:00 usiku kucheza mchezo wa pili wa Kundi A dhidi ya MC Alger, ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza 2-0 nyumbani mbele ya Al Hilal ya Sudan, huku baadhi ya mastaa wa timu hiyo akiwamo Kipre Junior aliyewahi kukabiliana na Yanga katika Ligi Kuu Bara amekiri mchezo huo ni mgumu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kipre Jr alisema licha ya Yanga kutokuwa na matokeo mazuri kwenye mechi zao za ligi wanatarajia mchezo mzuri na wa ushindani kutokana na timu hiyo kuzungukwa na wachezaji wengi wazoefu kwenye michuano hiyo.

“Ni kweli wamepoteza mechi kama inavyoripotiwa lakini hilo haliwezi kutufanya ukaachana na maandalizi kwa kuamini kuwa mchezo utakuwa rahisi tumekaa na viongozi, mashabiki na benchi la ufundi kwaajili ya kujiweka sawa kuelekea mchezo huo,” alisema Kipre aliyeondoka Bara akifunga mabaop tisa na kuasisti tisa msimu uliopita, aliyeongeza;

“Tutaingia kwa kuiheshimu Yanga kutokana na ukubwa wao kwenye michuano lakini pia ubora wa mchezaji mmoja mmoja, wamepoteza lakini bado ni bora na wao wanatakiwa kuja kwa kutuheshimu wasitarajie mchezo rahisi.”

Akizungumzia suala la mashabiki zao kutokuwa sehemu ya mchezo wao wa nyumbani dhidi ya Yanga alisema kwa namna moja wamepoteza mchezaji muhimu ambaye alikuwa ana mchango katika mechi yao.

“Mashabiki zetu kukosekana kuna namna tumepoteza watu muhimu ambao wanatujenga na kutupa nguvu kutokana na shangwe zao majukwaani na wana upendo na sisi,” alisema Kipre na kuongeza;

“Pamoja na kutokuwa nao pamoja wameweza kutupa nafasi ya kukaa nao pamoja wakitutakia kila lakheri kuelekea mchezo huo huku wakitusisitiza kuwa bado wana imani na sisi wanajua hatuwezi kuwaangusha.”

Kipre Jr anaifahamu Yanga amekutana nayo akiwa na Azam FC ambayo ameichezea misimu miwili na kuacha rekodi nzuri ikiwa ni ya msimu uliopita alipofunga mabao tisa na kuasisti tisa wakati Azma ikimaliza ya pili.

Kabla ya kuitumikia Azam FC alishawahi kuitumikia Asec Mimosas, 2018-2020 ubora wake ulimfaya apate nafasi ya kuitumikia timu ya taifa ya vijana ya Ivory Coasta U-15 na U-17, pamoja na kikosi cha wachezaji wa ndani (CHAN) 2020.

Related Posts