Zanzibar yakabiliwa na uhaba wa wataalamu wa ganzi, usingizi

Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali inaendelea na juhudi za kuboresha utoaji wa huduma za matibabu kwa wananchi kwa kuimarisha vifaa vya uchunguzi, vifaatiba na rasilimali watu ambao wanatoa huduma za afya kwa wananchi.

Hata hivyo, amesema sekta ya afya bado inakabiliwa na uhaba wa wataalamu wa kada ya ganzi na usingizi ambao hadi sasa kwa Zanzibar wataalamu wa ganzi na usingizi ni 55 na mahitaji ni zaidi ya wataalamu 300.

Ametoa kauli hiyo leo Desemba 6, 2024 alipoahirisha mkutano wa 17 wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikichukua hatua kadhaa kukabiliana na changamoto hiyo, ikiwemo kada ya ganzi na usingizi kwa kutoa kipaumbele na kutoa ufadhili wa asilimia 100 kwa watakaosomea kada hiyo ndani na nje ya nchi. Amesema mpaka sasa madaktari 20 wameshapatiwa ufadhili huo.

Abdulla amesema Serikali imetoa kibali kwa kampuni zinazosimamia utoaji wa huduma katika hospitali za wilaya na mikoa kuwatafuta wataalamu wa ganzi na usingizi ndani na nje ya soko la Zanzibar ili waweze kuajiriwa.

“Napenda kutumia fursa hii kuwashajihisha madaktari wetu na vijana wetu kujitokeza na kusomea kada hii ya ganzi na usingizi ili tuweze kuwa na wataalamu wa kutosha katika utoaji wa huduma,” amesema.

Amesema jamii bado inakabiliwa na tatizo la udhalilishaji wa kijinsia, hivyo Serikali inaendelea kuchukua hatua kukabiliana na changamoto hiyo.

Amezitaja baadhi ya hatua zinazochukuliwa kuwa ni kuanzisha mahakama maalumu za kesi za udhalilishaji wa kijinsia kwa ngazi ya mikoa na kamati ya kuzuia udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar.

Amesema takwimu zinaonyesha kesi za vitendo vya udhalilishaji zimepungua kutoka 304 mwaka 2023 hadi kufikia 289 Oktoba 2024.

“Naendelea kutoa wito kwa jamii kuendelea kuwasimamia watoto wetu kwa malezi na kuwa nao karibu kwa kuwapatia elimu ya udhalilishaji, pia kuzuia mianya yote ya kufanya vitendo hivyo,” amesema.

Katika mkutano huo, amesema maswali 130 kutoka kwa wawakilishi yaliulizwa na kupatiwa majibu kutoka kwa mawaziri, huku Baraza likipokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za taasisi 14.

Baraza pia lilipokea hoja binafsi kumpongeza Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kutoka kwa mwakilishi wa kuteuliwa Juma Ali Khatib (Ada-Tadea) kwa mafanikio ya miaka minne.

Baadhi ya taarifa zilizowasilishwa barazani ni ya mwaka ya utekelezaji wa kazi za Ofisi ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa mwaka 2023/24, taarifa ya nane ya utekelezaji wa kazi za Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Zanzibar na taarifa ya utekelezaji wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (Zaeca) kwa mwaka 2023/2024.

Nyingine ni taarifa ya utekelezaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA) kwa mwaka 2023/2024.

Amesema Serikali kwa kutambua umuhimu wa elimu inaendelea kuboresha sekta hiyo kwa kuweka mifumo ya Tehama, ambayo itasaidia kuondoa changamoto mbalimbali na kuleta ufanisi katika utendaji.

Abdulla amesema Serikali imezindua mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za shule (SIS) ambao umeunganishwa katika shule zote Zanzibar na ofisi za elimu za mikoa na wilaya ukitarajiwa kurahisha kazi ya usimamizi wa elimu.

Amesema wizara inaendelea kuandikisha wanafunzi wapya kwa mwaka wa masomo 2025.

Makamu huyo wa rais amewataka wazazi kutumia fursa hiyo kujitokeza kuwaandikisha watoto wote waliofikia umri wa miaka minne kwa shule za maandalizi (awali) na miaka sita kwa shule za msingi ili wapate haki yao ya msingi ya elimu.

Akizungumzia ajali za barabarani, amesema bado zinaendelea kuathiri maisha ya watu na mali zao, licha ya juhudi kubwa za Serikali za kuboresha miundombinu ya barabara.

“Matukio ya ajali bado yanaendelea kujitokeza, takwimu zinaonyesha kuwa kwa kipindi cha kuanzia Januari 2024 hadi Oktoba, 2024 ajali 193 ziliripotiwa na kusababisha vifo 264 na majeruhi 216,” amesema.

Katika taarifa iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Zaeca, Ali Abdalla Ali alisema katika kipindi cha mwaka 2023/24 mamlaka imefanya uchuguzi wa vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

Amesema imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuhakikisha thamani halisi ya fedha iliyokusudiwa inafikiwa na kuelimisha wananchi juu ya athari za vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi, kuishauri Serikali kuhusu tuhuma mbalimbali zinazojitokeza dhidi yake na wananchi.

“Mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi hicho yamesaidia kuongeza nidhamu katika utumishi wa umma, hususani katika usimamizi wa rasilimali za umma,” amesema. 

Amesema wamepata taarifa hizo kupitia vyanzo mbalimbali, akieleza walipokea vyanzo vya moja kwa moja ofisini 195, waliopiga simu ya bure na kawaida walikuwa 3,576, taarifa zilizowasilishwa kupitia wasiri ni 279 na vyanzo vingine vinavyotokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), barua, mfumo wa sema na rais, mkutano wa wazi na televisheni ni taarifa 71.

Mkurugenzi huyo amesema kwa mwaka 2023, Zaeca imepokea taarifa 4,121 na baada ya kufanyiwa uchambuzi wa awali taarifa 3,524 zilihitaji ufafanuzi wa mambo mbalimbali ambayo hayahusiani na makosa yaliyopo chini ya Sheria ya Kuzuia Rushwa namba tano ya mwaka 2023.

“Hivyo taarifa hizo hazikuendelea na uchunguzi, na baada ya uchunguzi wa kina, taarifa 597 zilionekana kuwa na viashiria vya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, taarifa 79 zilitolewa ushauri wa kisheria, taarifa 27 zimesikilizwa na kuwasilishwa katika ngazi nyingine,” amesema.

Amesema taarifa 59 zilifungwa kwa kutojitosheleza kwa ushahidi, taarifa 78 zilifanyiwa udhibiti, taarifa 326 zinaendelea na uchunguzi na taarifa 28 zimewasilishwa katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka (DPP) kwa hatua zaidi za kisheria.

Related Posts