VINARA wa msimamo wa Ligi Kuu Bara, Azam FC pamoja na Singida Black Stars wanatarajia kushuka uwanjani jioni ya leo kuanza msako wa tiketi ya michuano ya kimataifa ya CAF kwa msimu ujao watakapocheza mechi za hatua ya 64 Bora ya Kombe la Shirikisho kwenye viwanja viwili tofauti.
Timu hizo zinazoongozwa na nyota wanaokimbiza katika orodha ya ufungaji mabao, Elvis Rupia na Feisal Salum zitashuka zikiwa na rekodi tamu za mechi za mwisho za Ligi Kuu Bara iliyosimama hadi wiki ijayo.
Azam inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 30 itakuwa wenyeji wa Iringa Sports kwenye Uwanja wa Azam Complex mchezo utakaopigwa saa 1:00 usiku, huku Singida itakuwa nUwanja wa Liti, Singida, kuikaribisha Magnet FC kuanzia saa 10:00 jioni kusaka tiketi ya kuingia hatua ya 32 Bora.
Licha ya kuwa na rekodi katika Ligi Kuu, Azam na Singida zinapaswa kuwa makini dhidi ya wachezaji wa timu wanazocheza nao ambazo ni za madaraja ya chini, kwani soka limekuwa na maajabu ya kushangaza katika michuano hiyo inayotoa mwakilishi wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Kocha wa Azam, timu iliyofika fainali ya msimu uliopita na kufungwa na Yanga kwa penalti, Rachid Taoussi aliyeshinda tuzo ya Kocha Bora kwa Novemba, alisema wanatarajia kuendelea walipoishia kwa kuahakikisha wanapata matokeo kwenye mchezo huo ili waweze kusonga hatua inayofuata.
“Simfahamu mpinzani wangu ila nimeiandaa timu ili iweze kupenye hatua hii ya awali na wachezaji wangu wapo kwenye hari nzuri ya ushindani wanautaka huo mchezo malengo ni kufanya vizuri ili tuweze kusonga mbele,’’ alisema Taoussi, huku Azam ikiwa na rekodi tamu katika hatua za awali za michuano hiyo.
Kocha msaidizi wa Singida, David Ouma alisema wamejiandaa vyema kwa mchezo huo na licha ya kutokuwa na matokeo mazuri kwa siku za hivi karibuni, ila amewataka nyota wa timu hiyo kutobweteka na kutumia faida ya kucheza uwanja wa nyumbani.
“Ni wakati wangu sahihi kuiongoza timu hii ambayo licha ya matokeo mabaya bado naamini ina kikosi bora na cha ushindani hivyo sitarajii kuangushwa licha ya wachezaji wangu kukutana na timu ambayo hawaifahamu.”