Chuo Kikuu Ardhi chajivunia ongezeko la ajira kwa wahitimu wake

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wakati Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) kikiweka malengo ya kufikia wahitimu 13,000 ifikapo mwaka 2029 kimesema kinajivunia asilimia 95 ya wahitimu wake wanapata ajira ndani na nje ya nchi.

Akizungumza Desemba 5,2024 na waandishi wa habari wakati wa mahafali ya 18 Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Evaristo Liwa, amesema wahitimu wa chuo hicho wamekuwa wakiajiriwa katika sekta binafsi, Serikali na mataifa ya nje.

“Katika utafiti tuliofanya tumegundua asilimia 60 ya wanafunzi wote wanaajiriwa katika sekta binafsi, ni makampuni na mashirika yaliyoanzishwa na wahitimu wetu, asilimia 30 wanaajiriwa na Serikali, asilimia tano wanakwenda nje ya nchi…ziko nchi huwa zinasubiri tukishafanya mahafali wanakuja kuchukua ‘surveyrs’,” amesema Profesa Liwa.

Aidha amesema wamekuwa wakisisitiza maadili kwa wanafunzi wao tangu wanaporipoti chuoni mpaka wanapomaliza hatua iliyowezesha kupata sifa nzuri katika soko la ajira.

Kwa mujibu wa Profesa Liwa, idadi ya wahitimu imeongezeka kutoka 1,148 mwaka 2023 na kufikia 1,453 mwaka huu huku malengo yakiwa kufikia wahitimu 13,000 mwaka 2029.

Amesema malengo hayo yatafikiwa kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambao unalenga kukuza elimu ya juu kama chachu ya uchumi mpya wa Tanzania.

Mmoja wa wahitimu wa Shahada ya Sayansi na Uhandisi wa Mazingira, Lucy Masatu, amesema masomo hayo yatamsaidia katika masuala mbalimbali ya kimazingira na nchi kwa ujumla.

“Chuo hiki wengi wanakiogopa wanakiona kigumu, lakini napenda kuwatoa hofu hasa wasichana wenzangu kila kitu kinawezekana, kama ambavyo mimi nimeweza na wao wataweza,” amesema Masatu.

Katika mahafali hayo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande, amewatunuku wahitimu 1,453 shahada mbalimbali ambapo 11 wametunukiwa Shahada za Uzamivu, 86 Shahada za Uzamili na 1,356 Shahada za Awali.

Related Posts