Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, ametoa uchambuzi wa kina kuhusu ushindi mkubwa wa chama hicho katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Septemba 27, mwaka 2024.
Dkt. Dimwa ameleza sababu, dhamira na mafanikio yaliyofikiwa na CCM, na pia kuonyesha jinsi ushindi huo unavyotoa picha ya nguvu ya chama na uwajibikaji wenye tija na dhamira ya dhati ya CCM ya kuwatumikia wananchi wote bila ubaguzi kwa muktadha wa siasa za ushindani chini ya mfumo wa vyama vingi.
Hayo ameyasema katika mahojiano maalum ya kutoa tathmini yake ya mafanikio na uimara wa CCM katika medani za kisiasa nchini.
Sababu za Ushindi wa Kishindo
Dkt. Dimwa amebainisha kuwa ushindi wa asilimia 99 wa CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni matokeo ya utendaji bora wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi .
Ameeleza kuwa CCM imeshinda kwa kiwango hicho kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi wote mijini na vijijini, kuimarisha huduma za kijamii, na kutoa fursa za ajira kwa vijana wa rika tofauti na makundi mbalimbali ya wanawake.
“Ushindi huu ni matokeo ya uongozi thabiti na wa kujitolea wa viongozi wetu. Wananchi wameshuhudia mabadiliko ya kweli katika maisha yao. Ujenzi wa miundombinu, huduma za afya, elimu na kilimo ni baadhi ya sekta zinazoimarisha maisha ya watu wote bila ubaguzi wa kisiasa,kidini na kikabila. Hii inadhihirisha kuwa CCM ni chama kinachotekeleza ahadi zake na ni chama cha maendeleo,” alisema Dkt. Dimwa.
Demokrasia na Mfumo wa Vyama Vingi
Katika mchango wake, Dkt. Dimwa alieleza kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni dhihirisho la nguvu ya demokrasia katika mfumo wa vyama vingi.
Alisisitiza kuwa siasa za ushindani ni muhimu katika kuleta maendeleo na kwamba CCM inaheshimu na kutambua mchango wa vyama vingine, ingawa CCM inabaki kuwa chama chenye uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko ya kivitendo kwa wananchi.
“Katika mfumo wa vyama vingi, ushindani ni muhimu, lakini ushindi wa CCM katika uchaguzi huu ni uthibitisho wa kwamba wananchi wanatambua juhudi za serikali yetu.
Demokrasia siyo tu kushiriki katika uchaguzi, bali ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anafaidika na matunda ya demokrasia hiyo,” alisema Dkt. Dimwa.
Mafanikio ya Falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya 4R
Dkt. Dimwa pia alifafanua mafanikio yaliyofikiwa katika kutafsiri kwa vitendo falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya 4R imeleta matokeo chanya ya upatikanaji wa ushindi huo na kwamba mafanikio haya ni dhihirisho la jinsi serikali ya CCM inavyotoa huduma bora kwa wananchi, huku ikirudisha imani ya wananchi kwa serikali na kuimarisha umoja wa kitaifa.
” Tumeshuhudia maendeleo katika maeneo mengi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu, upatikanaji wa huduma za afya na elimu, na uimarishaji wa uchumi wa Zanzibar. Kwa hiyo, ushindi huu unaonyesha kuwa falsafa ya Rais Samia ya 4R inatekelezwa kwa vitendo na inagusa maisha ya wananchi,” alisema Dkt. Dimwa.
Ushindi wa Serikali za Mitaa kama Tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa 2025
Dkt. Dimwa alisisitiza kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni tathmini halisi ya matokeo yanayoweza kutarajiwa katika uchaguzi mkuu wa dola wa mwaka 2025.
Alieleza kuwa ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo pia unatoa picha ya kuwa CCM ni Chama kiongozi katika siasa za Tanzania na kwamba wananchi wenyewe kwa ridhaa yao wameamua kukiunga mkono kukipigia kura nyingi za ndio kupitia mfumo huru wa kidemokrasia.
“Ushindi wa serikali za mitaa ni kielelezo cha mapenzi ya wananchi kwa CCM na dhamira ya chama chetu ni kuhakikisha kuwa kila mtaa, kila kijiji, kila wilaya na kila kisiwa kinapata maendeleo.
Huu ni ushindi wa wananchi na ni uthibitisho wa kwamba uchaguzi mkuu wa 2025 utakuwa na mafanikio makubwa kwa CCM,” alisema Dkt. Dimwa.
Wito kwa Wananchi na Wanachama wa CCM
Dkt. Dimwa alitoa wito kwa wananchi wote, hasa wanachama wa CCM, kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la awamu ya pili ya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura litakalofanyika hivi karibuni.
Aliwakumbusha wananchi kuwa zoezi hili ni haki yao ya kikatiba na ni muhimu kwa kuimarisha demokrasia na uhuru wa kucgagua na kuchaguliwa nchini.
“Ni muhimu kwa kila mwananchi kuhakikisha kwamba jina lake linajumuishwa katika daftari la wapiga kura.
Hii ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania.Tunatoa wito kwa wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika zoezi hili muhimu, ili kuimarisha ushiriki wetu katika uchaguzi mkuu wa 2025,” alisisitiza Dkt. Dimwa
Pamoja na hayo Dkt.Dimwa, anaeleza kuwa CCM inaendelea kujizatiti na kuboresha huduma kwa wananchi, huku ikisisitiza kuwa uchaguzi wa 2025 utakuwa ni uthibitisho wa mafanikio ya chama na serikali katika kuleta maendeleo ya kweli kwa kila Mtanzania.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa,akizungumza juu ya mafanikio yaliyofikiwa na CCM kwa kuisimamia vizuri Serikali itoe huduma bora kwa wananchi.