Fei, Aziz Ki mambo mazito, deni lawatesa

LIGI Kuu Bara imesimama hadi katikati wiki ijayo, huku baadhi ya mastaa wa timu mbalimbali wakitembea, lakini kukiwa na mambo ambayo hayaeleweki katika maisha yao ya uwanjani na hata nje ya viwanja.

Msimu huu wa ligi umekuja na mambo yake, lakini kwa mastaa waliokuwapo uliopita wakigeuka kupambana ili kuweka mambo sawa, ilhali walioingia msimu huu wakitaka kufanya mambo yao.

Mastaa waliotesa msimu uliopita akiwamo Feisal Salum ‘Fei toto’ wa Azam, Waziri Junior (Dodoma Jiji) na Stephane Aziz KI (Yanga), msimu huu umekuja ukiwa na kibarua cha kurejea kile walichofanya msimu uliopita walipomaliza katika tatu bora ya wafungaji.

Katika msimu huo, Aziz KI alimaliza kinara wa mabao akifunga 21 na kuipa Yanga ubingwa msimu wa tatu mfululizo, huku Fei akishika nafasi ya pili na mabao 19 na kuiwezesha Azam kumaliza ya pili, na kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ilhali Waziri akiwa wa tatu na mabao 12.

Mbali na kuwa vinara wa mabao wakali hao waliasisti pia, Aziz KI mara nne akishika nafasi ya pili nyuma ya  kinara Kipre Junior aliyekuwa Azam, huku Fei Toto akiwa na saba na Waziri mara mbili. 

Hata hivyo, wakati ligi ikiwa raundi ya 13 msimu huu wakali hao na wengine waliofunika msimu uliopita mambo si mazuri kivile, kwani Aziz Ki amefunga bao moja dhidi ya Pamba na kuasisti mara mbili, Fei Toto akiwa na mabao manne na asisti nne vilevile na Waziri akiwa na bao moja.

Mchezaji mwingine aliyefunika msimu uliopita Maxi Nzengeli aliyefunga mabao 11 na asisti mbili angalau msimu huu anapambana akiwa na mabao matatu na asisti mbili jambo lililowaibua wadau waliozungumza kwamba licha ya kuwa ni mapema kuanza kuwajadili, lakini mastaa hao wana kibarua cha ziada. 

Staa wa zamani wa Simba,  Steven Mapunda ‘Garrincha’ amesema: “Ni muhimu kwa mchezaji kulinda kiwango chake. Kile walichofanya msimu uliopita kiwe na mwendelezo, kwani ni wachezaji wazuri na wana vipaji pamoja na hayo yote lazima wajitume mazoezini na kujitunza.”

Staa wa zamani wa mabao aliyetamba Bandari, Yanga, Simba na Taifa Stars, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ aliyeweka rekodi ya kufunga mabao 26 mwaka 1999 amesema : “Naamini wanaweza wakayafikia,  kuzidi ama wasiyafikie kinachotakiwa kwao ni kuonyesha kiwango cha kuzisaidia timu zao na wawe na mwendelezo wa viwango vyao. Pia wajitunze kwa kuzingatia nidhamu ya soka inavyotakiwa.”

Katika mechi 11  ilizocheza Yanga msimu uliopita sawa na za msimu huu, Aziz Ki alikuwa amefunga mabao saba wakati Fei Toto katika mechi 12 za msimu uliopita sawa na ilizocheza Azam sasa alikuwa na mabao saba kuonyesha mambo sio mambo kwao sawa na ilivyo kwa Waziri aliyefunga mabao 12 akiwa na KMC.

Waziri mwenyewe amekiri kuwa na kibarua kigumu kufikisha na kuvunja rekodi yake ya mabao ya msimu uliopita, kwani bado hajaianza rasmi ligi kutokana na kuwa majeruhi kwa muda mrefu.

“Ni suala la muda kufunga. Bado mechi zipo naamini nitafanya vizuri baada ya kurejea kutoka kwenye majeraha,” amesema Waziri, huku Fei Toto akisisitiza: “Nitaendelea kufunga bado mechi zipo, jambo la msingi ni afya njema, kujituma kwa bidii, kwa sababu soka linachezwa sehemu za wazi, hivyo tunachokifanya uwanjani kitaonekana.”

Kwa upande wa Maxi aliwahi kusema:  “Ninachokiangalia ni kuisaidia timu kwanza, nitafunga mabao mangapi hilo siwezi kulisema, jambo la msingi ni kuzingatia maelekezo ya kocha anataka nikifanye kipi uwanjani, nitakifanya kwa bidii.”

Kwa sasa kinara wa mabao ni Seleman Mwalimu (Fountain Gate) mwenye mabao sit akifuatiwa na  Jean Ahoua wa Simba na Elvis Rupia wa Singida Black Stars kila mmoja akiwa mabao matano, huku Edger William (FOG), Peter Lwasa (Kagera Sugar) wakilingana na Fei kila mmoja akiwa na manne.

Kwa upande wa Edger amesema: “Natamani msimu huu uwe wa kuandika rekodi ya kufunga mabao mengi, ingawa ni vigumu kusema mangapi, lakini natamani yasiwe chini ya 10.”

Related Posts