Jafo: Matumizi bora ya nishati kukuza uchumi wa EAC, SADC

Arusha. Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC), zimetakiwa kutengeneza teknolojia ya matumizi bora ya nishati kwa manufaa ya uchumi wa Afrika.

Pia, imeelezwa kwamba nishati ya uhakika ndiyo kichocheo kikubwa cha uchumi wa kanda hiyo na bara zima, kwa kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya shughuli mbalimbali zikiwemo za uendeshaji viwanda na ujasiriamali.

Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo wakati akifunga kongamano la kikanda kuhusu matumizi bora ya nishati, lililokuwa na kaulimbiu ‘Kuchagiza matumizi bora ya nishati kwa maendeleo endelevu.’

Amesema ili nchi hizo ziendelee kukuza uchumi kupitia shughuli za viwanda na biashara zenye tija, hilo linaweza kufikiwa iwapo kutakuwa na nishati ya kutosha na matumizi yake ni sahihi na yenye tija.

“Nchi yetu sisi tuna lengo la kutengeneza uchumi ukue zaidi, viwanda na biashara zitakuwa sana na ni lazima tuwe na nishati ambayo itatumika kwa usahihi zaidi. Tanzania imewekeza sana kwenye nishati na uwekezaji huo una maana sana katika uendelezaji wa biashara,” amesema.

Awali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk Khatibu Kazungu ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati itasimamia mkakati wa kwanza wa kitaifa wa miaka 10 wa matumizi bora ya nishati.

Amesema mkakati huo utakuwa mwongozo wa kufikia malengo ya ufanisi wa nishati kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

“Tutahakikisha kuwa mkakati huu unatekelezwa kwa kutenga bajeti ili nchi iweze kuwa na vifaa bora vya nishati,” amesema.

Ameongeza kuwa kupitia kongamano hilo maazimio kadhaa yametolewa ikiwemo kufanya tafiti za pamoja ili kuboresha matumizi bora ya nishati na kushirikisha sekta binafsi kikamilifu.

“Tutafanya kazi pamoja kutengeneza teknolojia ya matumizi bora ya nishati ili kuhakikisha matumizi bora ya nishati katika nchi za EAC na SADC kwa manufaa yao,” amesema.

Related Posts