Kijana amjeruhi mama yake kwa panga, adaiwa kuwa na matatizo ya akili

Morogoro. Mwanamke mmoja, Unna Martini (70) amenusurika kifo baada ya kukatwa panga kichwani na sehemu nyingine za mwili na mtoto wake wa kumzaa, Elias Paulo, kabla ya kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Akizungumzia tukio hilo, mke wa mtuhumiwa huyo, Evarista Matei ameeleza kuwa mume wake alianza kupata matatizo ya akili usiku wa kuamkia siku ya tukio, matatizo ambayo alikuwa nayo kwa muda mrefu na yalikuwa yametulia kwa muda.

“Usiku alianza kuongea vitu sivielewi, nikawa namuogopa, asubuhi nikamuomba nimpeleke hospitali, tulipofika akakataa kuchomwa sindano, akatoroka,” amesema Matei.

Amesema mume wake huyo anayefahamika kwa jina la Elias Paulo (38) baada ya kutoroka hospitalini hapo, alifika nyumbani na kumkuta mama yake huyo na kuanza kumshambulia kwa panga hadi kupoteza fahamu.

“Nilianza kuita majirani ambao wengi wao walikuwa mashambani walipofika wakanisaidia kumchukua mama tukamwahisha kituo cha afya cha jirani,” amesema Matei.

Paulo Paulo ambaye ni kaka wa mtuhumiwa ameeleza kuwa mdogo wake huyo alikuwa na matatizo ya akili yaliyosababishwa na uvutaji bangi, ambayo alipatiwa matibabu miaka saba iliyopita na aliacha kabisa uvutaji wa bangi lakini kutokana na tukio hili wana wasiwasi alianza tena uvutaji.

“Nilipata taarifa kwa majirani kuwa Elias alianza tena uvutaji bangi, nilimuuliza akakataa na hapo awali alikuwa na historia ya uvutaji bangi iliyomsababishia matatizo ya akili. Alipotekeleza tukio hilo alikimbia baadaye alirudi nyumbani na kuanza kufukia damu za mama,” amesema Paulo.

Frank Kalinga ambaye ni ofisa muuguzi kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro,  amethibitisha kumpokea mgonjwa huyo akiwa na majeraha matatu kichwani, mawili mkono wa kulia na lingine mguu wa kulia ambapo ameeleza kuwa anaendelea kupatiwa matibabu.

“Alipatiwa huduma ya kwanza kituo cha afya cha Mlali  saa 9 alasiri akaletwa hapa tukakuta baadhi ya majeraha bado yanavuja damu lakini tushampatia matibabu na anaendelea vizuri,” amesema Kalinga.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Gudugudu, Iddi Hassan amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo ambapo amesema kuwa alipokea taarifa hizo saa nne asubuhi.

Baada ya kufika eneo la tukio,  alimkuta mama huyo akiwa amefichwa nyuma ya nyumba damu zikiwa zinamwagika.

“Huyu kijana kweli alikuwa na matatizo ya akili na miaka ya nyuma aliwahi kushambuliwa na mapanga baada ya akili kuruka na kukimbilia kijiji cha jirani ambapo hawamtambui wakahisi ni mwizi hivyo wakamshambulia,” amesema Hassan.

Ameeleza kuwa baada ya kijana huyo kupona,  ghafla likatokea tukio la kumkata mama yake kwa panga.

Related Posts