Kocha Matola kutoa ushahidi kesi ya Muharami, wenzake

Dar es Saalam. Mashahidi 30 akiwemo, Kocha Seleman Matola (45) wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito kilo 34.89 inayomkabili mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy, Kambi Seif na wenzake watano.

Hayo yamebainishwa na Jamhuri baada ya kuwasomea washtakiwa hao orodha ya mashahidi na vielelezo, na kisha kesi hiyo kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa hatua ya usikilizwaji.

Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Mbali na idadi hiyo ya mashahidi, Jamhuri imesema itakuwa na vielelezo 89, zikiwemo hati za ukamataji mali, magari manane, maboksi mawili ya mbao yaliyohifadhia dawa kulevya, mfuko uliokuwa na heroini, simu zaidi ya nane, hati ya upekuzi na ripoti mbalimbali ikiwemo ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Kati ya vielelezo hivyo 36 ni halisia na 53 ni nyaraka.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 43 ya mwaka 2023 kukamilika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Muharami Sultani (40), maarufu Shilton, aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba Sport Club, Maulid Mzungu (54) maarufu Mbonde, mkazi wa Kisemvule ambaye ni dalali wa viwanja na muuza nazi, ambaye ni ndugu wa Muharami.

Wengine ni Said Matwiko mkazi Magole, John Andrew maarufu Chipanda (40) mkazi wa Kitunda, ambaye kazi yake ilikuwa kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na Sarah Joseph, ambaye ni mke wa Matwiko.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga akisaidiana na mawakili wa Serikali, Roida Mwakamele na Judith Kyamba aliieleza hayo Mahakama Desemba 5, 2024 wakati akiwasomewa washtakiwa maelezo.

Wakili Mwanga aliwasomewa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.

Baadhi ya vielelezo vilivyotajwa ni simu nne, magari matano aina ya Tata, fedha taslimu Sh9 milioni, Dola 500 za Marekani alizokuwa anamiliki Kambi.

Kompyuta mpakato (Laptop) aina ya Dell, maboksi matatu mojawapo likiwa limehifadhia kilo 7.79 za heroini, gari aina ya Toyota Noah, Harrier na Fortuner, hati ya ukamataji mali, maelezo ya mashahidi na maelezo ya onyo ya washtakiwa.

Vielelezo vingine ni hati za kusafiria za washtakiwa, funguo za gari hizo, rimoti ya gari ya Kambi, vitabu vya kumbukumbu viwili na ripoti mbalimbali za uchunguzi kutoka Jeshi la Polisi, TRA, Brela na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Mawakili Kyamba na Mwakamele walitaja mashahidi baadhi yao wakiwa ni Wakaguzi wa Polisi watano kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya( DCEA) ambao ni Hassan, Wamba, Johari, Brown na Lazaro Mhegere.

Wengine ni Matola ambaye ni Kocha Msaidizi wa Timu ya Simba, mdogo wake Kambi, Sabrina Seif; Tunu Bisanga, Asia Majid, ambaye ni hakimu; askari polisi mwenye namba H. 4153 Sajenti Timotheo na Abubakary Kindanguye.

Wengine ni Edith Ignas; Shakule Mustafa; askari polisi mwenye namba G. 934  Koplo Hassan; Aneth Mfinanga; Maureen Kitupa; Asia Charli, Seleman Mbwambo; Ester Ishenda; Ashura Bwatamu; Jackson Shambwe; Optatus Kimunye na Stanley Magoda.

Wengine ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Innocent Masangula na Witness wote kutoka DCEA; Jeremia Chacha; Shabani Mahenjela na Everligh Matinga.

Upande wa mashtaka baada ya kumaliza kuwasomea maelezo hayo, washtakiwa walidai watakuwa na mashahidi watakaowatetea katika kesi hiyo na vielelezo.

Washtakiwa walirudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Wanadaiwa kutenda makosa kati ya mwaka 2016, Aprili 15, 2021, Aprili 24, 2021, Oktoba 27, 2022 na Novemba 4, 2023 katika maeneo ya Kamegele wilayani Mkuranga na Dar es Salaam.

Related Posts