Muleba. Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kagera umemkabidhi nyumba yenye thamani ya Sh12 milioni, mama mzazi wa marehemu mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath aliyeuawa na kunyofolewa baadhi ya viungo vyake.
UVCCM mkoani humo waliahidi kumjengea nyumba mama huyo, Judith Richard baada ya kukumbwa na tukio la kuuawa kwa mwanaye, Asimwe, tukio ambalo liliwahuzunisha Watanzania wengi.
Mtoto Asimwe (2) aliporwa mikononi mwa mama yake huyo na watu wasiojulikana Mei 30, 2024 majira ya saa 2 usiku akiwa na mama yake nyumbani kwao katika Kijiji cha Bulamula, kata Kamachumu, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.
Juni 14, 2024, baadhi ya viungo vya mwili wake vikakutwa vimetelekezwa kwenye mfuko wa sandarusi chini ya karavati katika barabara ya Ruhanga Makongora katika kitongoji Malele, kata ya Ruhanga.
Tayari watu kadhaa wanatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya Asimwe, akiwemo baba yake mzazi, Novath Venanth na Padri Elpidius Rwegoshora, waliofunguliwa kesi ya mauaji namba 17740/2024 katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba.
UVCCM Mkoa Kagera wametekeleza ahadi waliyoitoa ya kununua kiwanja na kisha kumjengea nyumba mama mzazi wa marehemu mtoto huyo aliyeuawa kikatili.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Desemba 7, 2024, mkazi wa kijiji cha Bulamula ambaye ni mama mzazi wa marehemu Asimwe, Judith Richard amewashukuru UVCCM kwa kupambana kuhakikisha anapata nyumba hiyo.
Nyumba hiyo aliyokabidhiwa Judith ina vyumba viwili na flemu moja ya biashara atakayoitumia mwanamke huyo kwa ajili ya biashara ndogondogo.
“Namshukuru sana mwenyekiti huyu wa UVCCM Mkoa wa Kagera, ukweli ameweza kunifariji vizuri na kunifuta machozi ambayo yanalia moyo mzima, sasa ni wakati sahihi wa kuanza kupambania maisha yangu na ndoto zangu,” amesema Judith.
Judithi, kwa furaha kubwa huku akilengwa na machozi usoni, amesema kwa sasa anahisi hajakaa vizuri kisaikolojia maana ni ngumu kusahau kilichotokea, hivyo anaomba Watanzania waendelee kumuombea uzima na arudi kwenye hali yake.
Kwa upande wake, mama mzazi wa Judith, Odeda Richard ameeleza kuwa familia imefurahi na kupokea msaada huo kwa mtoto wao kujengewa nyumba nzuri na ya kisasa huku akizidi kumsihi mwanaye kujifunza kutokana na makossa.
Amemtaka mwanaye huyo akimtaka aachane na wanaume, kwanza ajitengeneze kimaisha huku akiahidi kuendelea kumjenga kiimani na kutoa ushauri mzuri kuhusu msaada ambao anaendelea kupatiwa na wadau mbalimbali.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera, Faris Buruhan amesema wamekabidhi kiwanja cha robo eka na nyumba ya vyumba viwili, mashine ya kushona nguo, vyote vikiwa na thamani ya Sh12,792,000.
“Leo tumemkabidhi Mama Asimwe nyumba yake ambayo tumeijenga katika kata hii ya Izigo, wilayani Muleba ina sifa zote na hii ni ahadi tuliyoitoa kipindi dada yetu huyu wasiyojulika wamempora mtoto wake na kisha vyombo vya dola kuwashughulikia.
“Ni kama kurudisha faraja kwake, hivyo tunaomba dada yetu, mdogo wetu aweze kujitunza aepukane na vishawishi vinavyoweza kujitokeza maana tunaamini ana safari ndefu ya kutimiza ndoto zake,” amesema Faris.
Hata hivyo, Faris amewashukuru pia wadau mbalimbali waliyowezesha fedha kuhakikisha ujenzi wa nyumba hiyo unafanikiwa na kuahidi kuwa watakuwa bega kwa bega na mama huyo.