Matola kusimama kizimbani kesi ya Cambiaso na wenzake

Mashahidi 30 akiwemo, Kocha Seleman Matola (45) wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito kilo 34.89 inayomkabili mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy, Kambi Seif na wenzake watano.

Hayo yamebainishwa na Jamhuri baada ya kuwasomea washtakiwa hao orodha ya mashahidi na vielelezo, na kisha kesi hiyo kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa hatua ya usikilizwaji.

Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Mbali na idadi hiyo ya mashahidi, Jamhuri imesema itakuwa na vielelezo 89, zikiwemo hati za ukamataji mali, magari manane, maboksi mawili ya mbao yaliyohifadhia dawa kulevya, mfuko uliokuwa na heroini, simu zaidi ya nane, hati ya upekuzi na ripoti mbalimbali ikiwemo ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Kati ya vielelezo hivyo 36 ni halisia na 53 ni nyaraka.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 43 ya mwaka 2023 kukamilika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Related Posts