Mbowe kutoa msimamo uchaguzi wa serikali za mitaa

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anatarajia kutoa msimamo wa chama hicho kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji 2024 siku ya Jumanne Disemba 10, 2024 makao makuu ya chama Mikocheni, Dar es Salaam

Msimamo huo unakuja kufuatia vikao vya kamati kuu ya chama hicho vilivyoketi tangu wiki iliyopita kupitia mitandao na moja kwa moja jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema leo Desemba 7, 2024 imesema Mbowe atatoa kwa umma, maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya chama kuhusu kinachoitwa  msimamo wa chama.

Awali Novemba 28, Mrema alitoa taarifa ya kikao hicho kilichofanyika Novemba 29, 2024 na kilipanga kujadili ajenda maalum ya “yaliyojiri kwenye kinachoitwa Uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongoji 2024.”

Hata hivyo, taarifa ilizopata Mwananchi zilisema kuwa Chadema iliweka kiporo ajenda ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kwenye kikao chake cha Kamati Kuu kilichofanyika Novemba 29, 2024 kwa njia ya mtandao.

Badala yake waliamua ajenda ya uchaguzi huo uliofanyika Novemba 27, ijadaliwe Jumatatu Desemba 2 kwa wajumbe wa kamati hiyo kukutana ana kwa ana jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi Novemba 30, 2024, Mrema alisema kikao hicho cha kamati kuu kilipangwa kuendelea Desemba 2.

“Jana (Novemba 29), hatukumaliza tutaendelea Jumatatu, tutakutana Dar es Salaam. Kikao cha dharura ajenda yake ni moja tu ya tathmini ya hali ya uchaguzi wa serikali za mitaa,” alisema Mrema.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya Chadema zinaeleza kikao hicho kilichoanza mchana na kuahirishwa jioni, pia kilipokea taarifa za hali ya kisiasa za kanda 10 za chama hicho.

Inaelezwa baada ya taarifa hizo, wajumbe walishauri suala uchaguzi wa serikali za mitaa kulingana na uzito wake, lijadiliwe kwa mkutano wa  ana kwa ana.

Chama hicho mara kadhaa kimelalamika kuwa licha ya wagombea wake kuenguliwa, mawakala kuondolewa na kura bandia kupenyezwa, makada wake watatu waliuawa.

Related Posts