Tabora. Mwili wa Mery Nassoro aliyefariki Desemba 5,2024 akiwa chumbani pamoja na mwanajeshi mstaafu, Petro Masali umezikwa leo kwenye makaburi ya Kanisa la Roman katoliki yaliyopo kata ya Ipuli manispaa ya Tabora bila misa ya msiba.
Mwananchi imeshuhudia watu wakiwa msibani mtaa wa Mhalitani wakiwa wamekusanyika wakatangaziwa kuwa hakutakuwa na ibaada wala wasifu wake, badala yake ataombewa sala tatu pekee kisha ataenda kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 7, 2024 Zakayo Gabriel kiongozi wa kanisa la Roman Katoliki, amesema kwa mujibu wa taratibu za kanisa Katoliki mtu anapofariki akiwa katika mazingira aliyokuwa nayo marehemu, anazikwa bila kufanyiwa ibaada kama watu wengine.
“Tunasikitika kwamba marehemu hatafanyiwa ibada licha ya kwamba alikuwa muumini mzuri wa kanisa letu na kwenye jumuiya yetu, hivyo kwa mujibu wa maelekezo ambayo yametolewa na kanisa, ataombewa sala tatu pekee kisha ataenda kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele” amesema Gabriel
Aidha, kiongozi huyo ameeleza kuwa tukio lililotokea kwa muumini mwenzao liwe fundisho kwa wale wote ambao wanasaliti ndoa zao kwani kifo ni fumbo.
“Kama angefariki kwa wema angefanyiwa ibada lakini amezikwa bila ibaada sababu ya matendo ambayo yamemfanya afe kifo kisicho chema mbele ya uso wa dunia na mbele za Mungu”.
Mume wa marehemu, Juma Masanja amesema mke wake amemuacha kwenye majonzi makubwa na kwamba hajui atawaleaje watoto saba walioachiwa kwa kuwa bado wadogo.
“Tumekaa miaka 30 na mwaka uliopita ndio tumefunga ndoa, binafsi nimemsamehe lakini naona nina mzigo mkubwa wa kuwalea watoto hawa saba ambao ameniachia” amesema Masanja
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Mhalitani Mwajuma Magomba amesema mpango wake kwa sasa ni kuitisha kikao kwa wanawake wote katika mtaa wake ili awape elimu kuhusu ndoa zao baada ya tukio hilo.
“Kama mtaa tumesikitishwa na tukio hili, marehemu alikuwa mtu wa watu na hakuna aliyedhani kama angefariki katika hali hii, kutokana na kilichotukuta nimepanga kuitisha kikao na wanawake wote katika mtaa huu kuwapa elimu jinsi ya kuishi katika ndoa zao na kuepukana na matendo ya usaliti jambo ambalo limetia aibu katika mtaa huu” amesema Mzee Yassin Hussein mkazi wa mtaa wa Nyerere kata ya Ipuli manispaa ya Tabora.
Desemba 5, 2024 Jeshi la Polisi mkoa wa Tabora kupitia kwa kamanda wa jeshi hilo Richard Abwao, alitoa taarifa za kufariki kwa Petro Masali ambaye ni mwanajeshi mstaafu pamoja na Mery Nassoro ambapo walifariki wakiwa faragha na leo hii mwili wa marehemu Meresiana Eduard umezikwa makaburi ya Roman Katoliki Ipuli manispaa ya Tabora huku mwili wa mwanajeshi mstaafu, Petro Masali ukisafirishwa kuzikwa wilayani Nzega.