Mwambusi sasa auma meno mapema

KOCHA wa Coastal Union, Juma Mwambusi ameamua kufunga ukimya na kuweka mikakati kwa ajili ya msimu huu ili kuhakikisha kwamba anapambania nafasi ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Coastal ina kumbukumbu nzuri ya kushika nafasi ya nne msimu uliopita chini ya kocha David Ouma na kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika ilikotolewa raundi ya awali na Bravos ya Angola kwa mabao 3-0, kisha kocha huyo Mkenya akatimuliwa.

Matokeo ambayo yalimfanya Ouma afungashiwe virago kisha timu ikawa chini ya Joseph Lazaro kama kaimu kocha mkuu ambaye alianza msimu huu wa 2024/25 wa Ligi Kuu Bara kwa kuiongoza katika michezo minane sawa pointi ilizokusanya.

Mwambusi alikabidhiwa timu hiyo Septemba na hadi sasa ameiongoza katika michezo mitano ikishinda miwili sawa na sare, ikipoteza mmoja mbele ya Yanga na kocha huyo kukusanya pointi nane ambazo ukijumlisha na zile nane timu ikiwa chini ya Joseph Lazaro inakuwa nazo 16, ikiwa ni 14 tofauti na vina ra wa ligi, Azam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwambusi alisema kwa namna timu inavyocheza inampa matumaini kwamba inaweza kupambania ubingwa au kumaliza katika nafasi tatu za juu ambayo ndio malengo yao makubwa msimu huu licha ya ligi hiyo kuwa na ushindani mkubwa.

“Malengo ni ubingwa ama nafasi tatu za juu, sisi wala hatuwazi nafasi ya nne tunawaza ubingwa ndio malengo yetu makubwa,” alisema Mwambusi aliyewahi kuinoa pia Yanga.

Alisisitiza katika kuhakikisha wanatimiza malengo hayo kama kiongozi wa benchi la ufundi anaendelea na kazi ya kurekebisha sehemu ambazo zilionekana kuwa na upungufu katika michezo iliyopita ikiwemo safu ya ushambuliaji.

Related Posts