Moshi. Mzee Isaac Malya (72), aliyeuawa kwa kupigwa na kitu kizito nyumbani kwake, amezikwa, huku Paroko wa Parokia Teule ya Kifuni, Padre Thomas Tingo akionya jamii kuacha roho za chuki na visasi, akisema zimekuwa chanzo cha mauaji yanayotikisa familia na taifa kwa ujumla.
Mzee Malya amezikwa leo, Desemba 7, 2024 nyumbani kwake Kibosho Umbwe Onana, maziko ambayo yamehudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali huku vilio na simanzi vikitawala.
Mallya ambaye ni kaka wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, alifariki Desemba 2, 2024 kwa kupigwa na kitu kizito kichwani wakati akijiandaa kwenda kanisani asubuhi.
Akihubiri katika maziko hayo, Padre Tingo amesema mauaji yameonekana kama sehemu ya maisha katika jamii nyingi kwa sasa na chanzo kikubwa cha matukio hayo ni kutawala kwa roho za chuki na visasi.
“Ukisikiliza vyombo vya habari kila siku utasikia habari za mauaji ya ovyo, mara mke kaua mume, mara mume kaua mke, watoto wameua wazazi, ukoo wameuana na jamii kuuana, tumefanya mauaji kama sehemu ya maisha yetu kwenye jamii, hii siyo sawa,” amesema Padre Tingo.
“Kinachosababisha mauaji mengi leo katika jamii ni kuenea kwa roho ya visasi na kutoweka kwa hofu ya Mungu miongoni mwa watu. Tambueni mauaji hayaji kwa bahati mbaya huwa yanapangwa, tujiepushe nayo tuishi kwa amani,” amesema.
Padre Tingo ametoa wito kwa jamii kuungana kwa pamoja kukemea matukio yasiyofaa ikiwemo ya mauaji na kuhakikisha wanatoa taarifa pindi wanapoona viashiria au kubaini makundi yanayotaka kufanya uhalifu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
“Ndugu zangu Wakristo tusimame kukemea dhambi na kuonyana sisi kwa sisi, kila mtu achukue hatua na tujifunze kutumia njia sahihi kusuluhisha matatizo yetu, tutambue kuwa damu hizi tunazozimwaga juu ya ardhi hazimwagiki bure, zitageuka laana,” ameeleza padri huyo.
Amezitaka pia familia kujenga utamaduni wa kuitana vikao vya ukoo kuelezana changamoto mbalimbali zinazowahusu na kuondoa chuki miongoni mwao ili kuepuka vifo vya chuki na visasi.
“Ndugu tuishi maisha ya kupendana, kuheshimiana tuepuke hasira na tujifunze kutawala midomo yetu na siku zote tupende kufanya kazi kwa bidii na nidhamu ili kupata fedha halali,” amesema.
Ameitaka pia jamii kusimamia kweli na kutoa ushirikiano kuhakikisha wahusika waliohusika na tukio la mauaji ya mzee Malya wanakamatwa na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.
Akitoa salamu za Serikali, Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Yusuph Nzowa amesema tukio hilo ni la kinyama na kihuni na kuwataka wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika wa tukio hilo.
“Nitoe pole kwa msiba huu mzito, huu ni unyama, uhuni kwa watu wachache ambao wamethubutu kupoteza uhai wa huyu mzee, hili limetugusa sana kama uongozi wa mkoa. Hili halikubaliki na kuanzia siku tumepokea taarifa za tukio hili, tumechukua hatua mbalimbali kuhakikisha tunawatafuta wale wote ambao wamehusika na tukio hili,” amesema Nzowa.
Ameongeza kuwa: “Serikali ina mkono mrefu na tutahakikisha wale wote waliohusika wanakamatwa ili haki na sheria iweze kuchukua mkondo wake.Tukio hili tunalichunguza kwa kina na niwasihi wananchi wa eneo hili, yeyote ambaye ana taarifa kuhusiana na tukio hili, ajitokeze kutoa taarifa ili zisaidie vyombo vyetu vya ulinzi katika kuchukua hatua, tunajua watu hawa hawajatoka mbali ni ndugu zetu na baadhi yetu tunawajua.”
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema uchunguzi wa tukio hilo, unaendelea na tayari wamewakamata watu wanne.
“Uchunguzi wa tukio hili ulianza mara moja na mpaka sasa tunawashikilia watu wanne, tunaendelea na uchunguzi, lakini milango iko wazi mwenye taarifa zozote kuhusiana na tukio hili alete taarifa, tuzifanyie kazi,” amesema.
Amekemea vikali tukio kama hili kwani hakuna aliyepewa mamlaka ya kutoa uhai wa mtu lakini vyanzo vya vifo vingi vinatokana na matumizi ya vilevi kwa kuwa vilevi vimesababisha matukio mengi ya mauaji.
Akitoa salamu za rambirambi, mwanaharakati Vicky Massawe amesema Mzee Malya ni mtu wa 12 kuuawa katika kata hiyo katika kipindi cha hivi karibuni na kuitaka jamii kupaza sauti kutokomeza matukio hayo ya kinyama na kikatili.
“Mzee Isaac alikuwa ni mtu msema ukweli ndiyo maana ameuawa, lakini hawa waliotekeleza mauaji haya sidhani kama walikuwa sawa. Inaonekana walitumia dawa za kulevya, tuambiane ukweli hapa bangi inauzwa kama njugu,” amedai Massawe.
Akizungumzia tatizo la mauaji Kibosho, Kamanda Maigwa amesema ameshtuka kusikia kuna matukio 12 ya mauaji yaliyotokea katika kata hiyo na kuomba kupata taarifa ili waweze kufuatilia.
“Nimeshtuka kusikia kuna matukio 12 ya vifo, sasa sijui kama ni kabla sijaja au vipi, lakini kama yapo kesi hainaga mwisho. Wanishirikishe tushirikishane kuhakikisha eneo letu liko salama lakini pia niwasihi, toeni taarifa za matukio na viashiria vya matukio, kwani baba paroko ameelezea vyanzo vya vifo ni pamoja na wivu wa mapenzi, migogoro ya ardhi, visasi na mambo kama hayo ambapo hata vitabu vya dini vinakemea,” amesema Maigwa.
Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel anesema chama hicho kimepokea msiba huo kwa mshtuko mkubwa na kuiomba familia kuutumia msiba huo kuwaunganisha na kuimarisha umoja miongoni mwao.
“Tumempoteza baba, rafiki, mcheshi na mshauri, baba alikuwa mwenye upendo, msema kweli na mpenda haki, hakika tumepoteza mtu muhimu na kiungo katika familia,” amesema.