Sera pendekezwa ya jinsia kwa vyama vya siasa yazinduliwa 

Unguja. Ili kuweka usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali ndani ya vyama vya siasa Zanzibar, imezinduliwa sera ya jinsia ya mfano, inayopendekezwa kwa vyama vya siasa.

Pia umezinduliwa muundo unaopendekezwa wa dawati la jinsia kwa vyama vya siasa visiwani humo.

Miongoni mwa mambo yanayosisitizwa katika sera hiyo ni muhimu kwa kila chama cha siasa kuwa na mipango ya kuhamasisha wanawake kushiriki katika uongozi kufikia asilimia 40.

Kila chama kitoe muongozo wa sera kwenye chama chake na kuhakikisha wanawake wanahamasishwa sawa na wanaume ili kufikia asilimia 50 kwa 50.

Pia kila chama kinatakiwa kuweka sera wazi, mipango na bajeti itekelezwe, kiwajengee uwezo na kutoa fursa sawa kwa wanawake, huku msajili wa vyama vya siasa akitakiwa kuweka kipengele maalumu cha kukagua sera ya vyama vya siasa, iwapo inatekelezwa na kuchukua hatua.

Mapendekezo ya sera na muundo huo wa dawati la jinsia, vimeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa –Zanzibar), Jumuiya ya Ulinzi wa Mazingira na Jinsia Pemba (Pegao), Chama cha Wanasheria Wanawake (Zafela) na Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (Juwauza) kwa ufadhili wa ubalozi wa Norway nchini Tanzania.

Akizungumza leo Desemba 7, 2024 wakati wa kuzindua sera hiyo ikiwa ni sehemu ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijisnia duniani, Mkurugenzi wa Tamwa-Zanzibar, Dk Mzuri Issa, amesema mfumo wa sera hiyo unatambua mahitaji ya usawa na ushiriki wa pamoja kwa wanawake na wanaume katika mifumo yote ya usawa wa kisiasa na ngazi zote za maamuzi.

“Malengo ya ujumla ya sera hiyo ni kutoa msingi wa ujumuishaji wa jinsia katika michakato ya kupanga, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini katika mipango mikubwa ya kijamii, kiuchumi, utamaduni na michakato ya kisiasa ambayo inaleta usawa wa kijinsia na maendeleo ya usawa Zanzibar,” amesema.

Amesema tangu Tanzania iwe mwanachama wa Jumuiya ya Madola, imesaini mikataba na matamko ambayo yanalenga kuleta usawa, kwa hiyo sera hiyo ingependa kuthibitisha dhamira ya kufikia usawa kati ya wanawake na wanaume pamoja na ahadi za lazima katika vyama vya siasa kama inavyoonyeshwa katika idadi ya nyaraka, mikataba na maazimio.

Hii ni pamoja na chata ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 1945, Tamko la Haki za Binadamu la mwaka 1948 na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966.

Hata hivyo, amesema sera hiyo haiwezi kufanikiwa pasipokuwa na michango na utayari wa vyama vya siasa na taasisi zingine.

Mshauri katika uandaaji wa sera hiyo, Dk Sikujua Omar, amesema licha ya ukosefu wa data katika maeneo mengi, ushahidi unaonyesha wanawake hawana uwakilishi katika ngazi zote katika siasa na kufanya maamuzi.

“Hapa Zanzibar hasa wanawake wanapata asilimia 37 katika Baraza la Wawakilishi. Uwakilishi wa wanawake pia unategemea sana huruma ya viti maalumu,” amesema.

Dk Sikujua ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), amesema sera hiyo inawiana na mageuzi ya hivi karibuni ya sheria yanayosisitiza ushirikishwaji wa kijinsia, usalama na uwakilishi sawa katika mazingira ya kisiasa.

Sheria ya Uchaguzi ya Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 kifungu cha 135, inalenga kuzuia ukatili wa kijinsia ndani ya michakato ya kisiasa, ikisisitiza umuhimu wa vyombo vya siasa kutekeleza sera makini zinazowalinda washiriki dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

“Wanawake mara nyingi hukabiliana na vizuizi kwa ushiriki wao mzuri katika mchakato wa uchaguzi kama wapigakura, wagombea na mawakala wa kura miongoni mwa uwezo mwingine,” amesema.

Amesema haki zao za ushiriki mara nyingi zinahujumiwa na matarajio ya kitamaduni na kanuni za kijamii, kutengwa na majukwaa ya maamuzi yanayotawaliwa na wanaume, ukosefu wa rasilimali za kifedha, ufikiaji wa kikomo wa habari na maarifa, ubaguzi na unyanyasaji ulioenea.

“Haya yote yanapaswa kuangaliwa kwa kina, kuwasaidia wanawake na kuondoa mifumo hii ili kuweka usawa,” amesema.

Mkuu wa misheni kutoka Ubalozi wa Norway, Kjetil Schie amesema hiyo ni fursa katika uongozi na siasa.

Amesema maendeleo bila wanawake hayawezekani na kwamba: “Wakati Tanzania ikijiandaa katika uchaguzi mkuu mwaka ujao, ni muhimu kuhakikisha usawa unazingatiwa kwa namna gani wanawake hususani wasichana kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika mchakato huo.”

Amesema ukiangalia katika ngazi za juu huoni usawa licha ya wanawake kuwa wengi na kuwa na rasilimali nyingi ambazo zinaweza kumsaidia mwanamke kuwa kiongozi.

“Tunapowainua wanawake, nchi inapata uchumi imara, uongozi thabiti katika jamii,” amesema Schie, akitoa mfano wa Norway kwamba asilimia 40 ya viongozi katika sekta za umma ni wanawake hata kwenye sekta binafsi wanajumuisha zaidi wanawake.

“Wanawake wanatuhitaji kuwasaidia kushiriki katika uongozi, tunaweza kuondoa vikwazo na kutengeneza nafasi za uongozi kwa wanawake jambo hili ni muhimu, na hili tunaweza kujenga jamii yenye usawa,” amesema.

Halima Ibrahim Mohamed kutoka ACT-Wazalendo, amesema chama hicho kina sera ya jinsia na inatekelezwa kwa vitendo. Ilizinduliwa Aprili 2024 na wanataka kuwa na dawati la jinsia.

Amesema mwaka 2025 watagombea na asilimia itapanda.

Azah Ali Seleman, kutoka Chama cha Demokrasia Makini, amesema amepata hamasa kuingia kwenye uongozi tofauti na alivyokuwa awali, kwani anaweza kujisimamia na kujiamini.

“Matukio tulikuwa tunayaona kupitia chaguzi zilizopita lakini kwa sasa inabidi tuamke na kugombea ngazi tofauti,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mgeli Mshindani Ali amesema uwezeshaji wanawake uende sambamba na mipango ya kuiondoa nchi kuwa Taifa linaloendelea na kufika hatua ya kuwa lililoendelea.

Related Posts