NA VICTOR MASANGU, BAGAMOYO
Wakala wa maendeleo ya uongozi wa elimu (ADEM) katika kuunga mkono juhudi za Rais wa awamu wa sita Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu hapa nchini inaendelea kuweka mikakati kabambe ya kuongeza juhudi katika uendeshaji wa elimu katika shule za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu pamoja na maafisa elimu wote kuanzia ngazi za kata Wilaya, Mkoa hadi Taifa ikiwa ni moja ya kutekeleza adhma ya serikali ya kuboresha uongozi.
Hayo yamebainishwa na mtendaji mkuu wa Wakala wa maendeleo ya uongozi wa elimu (ADEM) Dkt. Maulid Maulid wakati wa halfa ya mahafali ya 32 ambayo yameudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali, wadau wa elimu ikiwa sambamba na wahitimu wapatao 998 ambao wamehitimu katika kozi mbali mbali.
Mtendaji huyo amesema kwamba malengo makubwa ya kuanzishwa kwa Wakala ni kwa ajili ya kuweza kuboresha uongozi ikiwa sambamba na na usimamizi na uendeshaji wa elimu ikiwa pamoja na kutoa mafunzo mbali mbali kwa wadhibiti wa ubora katika shule ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.
“Jumla ya wanachuo wapatao 998 wameweza kufanikiwa kuhitimu katika mahafali ya 32 ya ADEM, na kati ya hao wahitimu wapatao 745 ni wale ambao wamesoma stashahada ya uongozi na usimamizi wa elimu (DEMA) na wanachuo 250 ni waliomaliza kozi ya stashahada ya udhibiti ubora wa shule (DSQA) na wanachuo wengine watatu wamehitimu astashahada ya uongozi , usimamizi na utawala wa elimu (CELMA)
Aidha mtendaji huo amebainisha kwamba ADEM imeweza kushirikiana na chuo cha Aga Khan University katika kuendesha mafunzo ya stashahada ya uongozi na usimamizi wa elimu (DEMA) kwa walimu wakuu wapatao 47 kutoka katika Mkoa wa Lindi ambao nao wameweza kupata fursa ya kusoma na kuhitimu.
Kadhalika amewahimiza wahitimu wote kuhakikisha kwamba wanayatumia vizuri mahalifa ambayo wameyapata katika kipindi chote wakiwa masomoni kwa lengo la kuweza kulitumikia vema Taifa la Tanzania katika suala zima la sekta ya elimu.
“Nipende kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa wahitimu wote ambao wamefanikiwa kumaliza katika kozi zao mbali mbali lakini kikubwa wanapaswa kuwekaa misingi mizuri ya kutumia taaluma yao waliyoipata katika kipindi chote kwa ajili ya kuweza kuisaidia Wizara pamoja na Taifa la Tanzania katika sekta ya elimu,”alisema Dkt. Maulid
Kwa upande wake Naibu katibu mkuu Wizara ya ya elimu ,sayansi na teknolojia Dkt. Wilson Mahera amesema kwamba serikali inatambua umuhimu wa mafunzo kazini ikiwa ni pamoja na yale ambayo yanatolewa na ADEM aambayo lengo lake kubwa ni kuimarisha utendaji,usimamizi na udhibiti wa ubora wa elimu inayotolewa shuleni.
Aliongeza kuwa mafunzo ambayo yanatolewa na ADEM kwa baadhi ya watumishi wakiwa kazini ni moja ya chachu kubwa katika kuwajengea uwezo watumishi hao kwa ajili ya kuendana na mabadiliko katika mazingira ya kiutendaji wa kazi zao za kila siku.
“Ujio wangu wa leo kwa kweli umeweza kunipa nafasi ya kujionea shughuli mbali mbali ambazo zinafanywa na ADEM katika suala zima la utoaji wa elimu na kwamba kupitia mafunzo haya yataweza kuwaongezea ujuzi zaidi ambao utawasaidia kwa kiasi kikubwa katika utekelezzaji wa majukumu yao ya kazi,”alisema
Pia alibainisha kuwa Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia inatambua kuwa mafunzo ambayo yanatolewa na ADEM yamekuwa na matokea chaanya kwa watendaji na viongozi , wasimamizi pamoja na wadhibiti ubora hapa nchini.
Katika hatua nyingine aliuomba uongozi wa ADEM kuhakikisha kwamba wanapaswa kuongeza juhudi zaidi na ubunifu na kuzingatia misingi ya utawala bora katika mafunzo wanayoyatoa ili kuweza kuisaidia serikalhi kufanikisha dhima ambayo imejiwekea katika sekta ya elimu hapaa nchini.