Sh110 bilioni kuboresha mashamba ya misitu, mikoko

Dar es Salaam. Tanzania imesaini mkataba wa Euro 39.9 milioni (sawa na zaidi ya Sh109.83 bilioni) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa mashamba ya miti ya Serikali na kuhifadhi misitu ya mikoko.

Mradi huu unalenga kuziba pengo hilo kwa kupanda hekta 22,500 za miti ndani ya miaka mitano kwenye mashamba ya Silayo, Mtibwa, na Wino.

Pia utaimarisha usimamizi wa kiikolojia katika misitu ya mikoko ya Kilwa na Rufiji, yenye ukubwa wa jumla wa hekta 76,000.

Akizungumza jana Desemba 6, 2024 wakati wa hafla ya kusaini mkataba huo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, amesema mradi huo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali katika kuhifadhi na kuendeleza sekta ya misitu nchini.

“Mradi huu ni muhimu kwa kupanua maeneo ya upandaji miti, kuboresha ubora wa mbegu, na kuimarisha uhifadhi wa mikoko kwa kushirikisha jamii na kuendeleza utalii wa kiikolojia,” amesema Kitandula.

Amesisitiza kuwa mashamba ya miti nchini Tanzania huchangia asilimia 50 ya mapato yanayokusanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na yana mchango mkubwa katika kuunga mkono viwanda, biashara ya kimataifa na maisha ya jamii za vijijini.

Tanzania Bara ina eneo la hekta milioni 48.1 za misitu, sawa na asilimia 55 ya eneo lake lote, lakini ni hekta 120,000 tu kati ya hekta 583,691 zinazofaa kwa upandaji miti ambazo zimepandwa.

Misitu ya mikoko, yenye ukubwa wa hekta 158,100 nchini Tanzania, ina mchango mkubwa katika kulinda ukanda wa pwani, kusaidia viumbe wa baharini na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Related Posts