SHIRIKA LA KIMATAIFA LA DAWA ZA KULEVYA LATOA PONGEZI KWA DCEA

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Kimataifa la Dawa za Kulevya na Masuala ya Sheria (INL), imetoa pongezi kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa mafanikio makubwa katika kudhibiti biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Juhudi hizo za DCEA ni pamoja na kuvunja mitandao mikubwa ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kukamata kiasi kikubwa cha dawa hizo.

Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Tanzania yenye lengo maalum la kumpongeza mafanikio hayo, Naibu Waziri Msaidizi wa Shirika la Kimataifa la Dawa za Kulevya na Masuala ya Sheria(INL) Maggie Nardi amesifu juhudi za DCEA na serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Ameahidi kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo ili kufanikisha vita dhidi ya janga hilo.”Ninawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya katika kuvunja mitandao ya biashara ya dawa za kulevya na kukamata dawa nyingi.

” Ushirikiano wetu utaendelea kuimarika, na tunatoa pongezi kwa serikali ya Tanzania kwa jitihada zake madhubuti katika kukabiliana na changamoto hii,” amesema Maggie Nardi.

Pamoja na pongezi hizo Maggie pia amefurahishwa na huduma za kupunguza uhitaji ya dawa za kulevya na tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya.

“Sikufahamu kwamba DCEA pia inafanya kazi ya kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya pamoja na kupunguza madhara ya dawa hizo. Hii ni hatua nzuri ambayo inapaswa kuendelea,” alisisitiza.

Akizungumzia kuhusu tishio la dawa za kulevya, Nardi ameelezea tishio linalotokana na dawa za kulevya za kisintetiki kama vile fentanyl, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa na ushirikano wa habari ili kukabiliana na changamoto hii.

“Natumai fentanyl haijaingia kwa wingi hapa nchini, lakini lazima tuchukue tahadhari. Tunaendelea kushirikiana na kubadilishana uzoefu ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya biashara ya dawa za kulevya.

“Marekani ilijifunza kutokana na kile kilichotokea katika majimbo ya Kaskazini Mashariki, na hivyo walijitayarisha vyema wakati fentanyl ilipokuwa ikienea. Hii inadhihirisha umuhimu wa kushirikiana taarifa mapema.” Amesisitiza Maggie.

Ziara hii ni ishara ya ushirikiano wa kimataifa unaozidi kuimarika katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, na DCEA inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kupambana na janga hili na kupunguza athari zake kwa jamii.


 

Related Posts