Mwanza. “Tangu nimeanza kupanda miti mwaka 1959 nikiwa darasa la kwanza mpaka sasa nimepanda zaidi ya miti 1,700,000 kiasi kwamba sasa kila ninapokwenda huwa nakutana na watu wananiambia huu ni mti wangu nilipanda.”
Hayo ni maneno ya Padri wa Kanisa la Katoliki Jimbo la Geita, Thomas Bilingi wakati akisimulia namna alivyopanda miti zaidi ya 1,700,000 katika kipindi cha miaka 65.
Akizungumza na Mwananchi leo Disemba 7, 2024 baada ya kufanya matembezi ya kuhamasisha watu kutumia nishati safi jijini Mwanza, Padri Bilingi mwenye miaka 76 sasa, amesema alivutiwa kuanza kupanda miti baada ya kubaini miti ya matunda huleta ujirani mwema.
“Tangu kuzaliwa kwangu nyumbani nilikuta kuna mti wa matunda ambao kwa kilugha chetu unaitwa Sungwi, sasa watoto wa majirani walikuwa wakija nyumbani kula matunda hayo, nikaona kumbe miti ya matunda inaleta ujirani mwema na huduma mbalimbali,” amesema.
“Nilianza kupanda miti nikiwa na umri wa miaka 11 wakati naingia darasa la kwanza, mwaka 1959, katika shule ya msingi Kasisa iliyopo Buchosa, Mwanza, nikaja kuendelea nikiwa darasa la tano ambapo hapo nilianza kupanda miti kwa wingi,” ameongeza.
Padri Bilingi amesema miti hiyo ameipanda katika maeneo mbalimbali ambayo amekuwa akipita, mfano kwenye taasisi za elimu, dini, Serikali na maeneo binafsi.
“Baadhi ya shule nilizowahi kupanda miti ni shule ya msingi Kasisa, St Ambrose Mitere baada ya hapo nikaenda Nsumba sekondari, kila sehemu nilipokuwa naenda nilikuwa napanda miti na mara nyingi nilikuwa peke yangu, japo baadaye niliamua kushirikisha wenzangu tukawa kama kikundi nikishirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS),” amesema.
Ameongeza: “Changamoto kubwa ambayo nilikuwa nikikumbana nayo ni kuchekwa, uharibifu wakati mwingine mifugo inapelekwa kwenye maeneo ambayo nimepanda miti. Changamoto nyingine ni wizi, japo hii wakati mwingine nilikuwa na furahia kwamba kama wanaiba mti ina maana anaenda kupanda nyumbani kwake, kitu ambacho ni kizuri,” amesema.
Hata hivyo, amesema mbali na kupanda miti, pia, huwa anahamasisha watu kupanda kupitia mahubiri, mafundisho na kuongea na mtu binafsi akiwaeleza umuhimu wake.
“Nikiwa nafundisha mfano leo Jumamosi, nina vipindi vya ndoa kanisani huwa nawapatia mti na kuwaambia wakapande, endapo ikitokea mti huo ukakauka basi na ndoa yao itakuwa imeishia hapo, huwa wanakuja wananiambia ndoa haijavunjika na mti wenyewe haujakauka,” amesema Padri Bilingi.
Kiongozi huyo wa kiroho amesema moja ya siri ya kuendelea kuwa hai mpaka sasa,ni kutokana na yeye kupanda miti ambayo inamsaidia kiafya na wakati mwingine kujitibu.
“Kupanda miti ipo kwenye damu ndio maana kuna muda huwa nakula majani ya miti hiyo kwa sababu inanisaidia kusafisha na kutibu kifua, mfano badala ya kutumia majani ya dukani mimi nachuma majani ya mti wa mchachai, nakunywa,” amesema.
Akizungumzia maisha ya padri huyo, mmoja wa wadau wa mazingira jijini Mwanza, William Missanga, mbali na kumpongeza amesema kwake kama kijana inamtia nguvu ya kuendelea kupambana kuhakikisha jamii inaondokana na matumizi ya nishati chafu, huku suala la upandaji miti akilipa kipaumbele.
“Ni jambo la kusisimua kwa mimi kama kijana, linanifunza mambo mengi na kunifanya nione bado dunia inanitaka. Bado nina safari ndefu ya kufikia rekodi ya mtu kama huyo kwa sababu sio jambo la kawaida linahitaji kujituma na kuwa moyo,” amesema Missanga.
Balozi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya MR Tree Foundation, Mrisho Mabanzo (Mr Tree) amesema siku 10 zilizopita amempoteza mama yake, chanzo kikiwa ni moshi uliokuwa unatokana na matumizi ya kuni na mkaa.
“Mama yangu alikuwa mfanyabiashara mkubwa sana wa mkaa mpaka ikawa inafikia wakati analipia miti ili kukata na kupata kuni, lakini madhara yake miaka 30 mbele tumejikuta tunatumia gharama kubwa kumtibu mpaka kumpoteza kwa sababu ya athari zilizobainika kuwa zimetokana na matumizi ya nishati isiyo salama kwa maana ya moshi wa kuni na mkaa,” amesema Mr Tree.
Akizungumzia takwimu, Mr Tree Amesema: “Asilimia 16 ya ardhi ya Tanzania imeelekea kuwa jangwa, zaidi ya ekari 469,000 zinaharibiwa kila mwaka kutokana na matumizi ya kibinadamu hasa matumizi ya kuni na mkaa, hivyo ni viashiria vinatuonyesha hali ya hatari ndiyo maana hali ya hewa haitabiriki.”
Askari mhifadhi misitu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Ziwa, Maija Mkomwa amewataka wananchi kufika kwenye ofisi zao kwa ajili ya kujipatia miti bure ya matunda ya kupanda, huku akihimiza jamii kuachana na nishati chafu.
“TFS tunatoa wito kwa wananchi kwanza kutumia nishati safi kwa maana ya umeme na gesi lakini pia waondokane na nishati zinazoleta uharibifu wa mazingira, mfano kuni na mkaa,. Pia wananchi wapande miti kwa wingi kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mkomwa.
Naye Mkurugenzi wa Watengenezaji wa KuniSmart na JikoSmart kutoka kampuni ya Chabri Energy, Bernard Makachia ametoa wito kwa kampuni za gesi kupunguza gharama za mitungi ya gesi ili kuwawezesha Watanzania wengi kumudu kununua.