Tanzania ina jumla ya marubani 603, míongoni mwao ikiwa ni wazawa 344, wageni 259 huku ikiwa na uhitaji wa jumla ya marubani 755 na upungufu wa marubani 152.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Salim Msangi wakati akiongoza zoezi la kuwapongeza vijana wa kitanzania waliobahatika kupata udhamini wa kusomea urubani na Uhandisi wa Ndege. Desemba 7, 2024 jijini Dar es Salaam.
Bw. Msangi alisema Udhamini huu unatolewa na mfuko wa mafunzo ya urubani wa Mamlaka ‘Training Fund’.
Aliongeza kuwa Mfuko wa TCAA Training Fund ulianzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 74 cha sheria ya Usafiri wa Anga (Civil Aviation Act Cap 80 R. E. 2020 na unaratibiwa kwa mujibu wa kanuni ya The Civil Aviation (Contribution and Administration of the Training Fund) Regulation, 2013 na marekebisho yake ya 2016.
Bw. Msangi alisema mchakato wa masomo ulianza mwishoni mwa mwaka 2019 ambapo marubani hao walipelekwa masomoni chuo cha East African Civil Aviation Academy kilichoko nchini Uganda.
Alisema masomo hayo yaliendelea mwanzoni mwa mwaka 2023 marubani hawa walimaliza hatua ya Licence Commercial Pilot Licence (CPL).
Aliongeza kuwa marubani hao walijiunga na chuo cha Mafunzo cha Mosswood Transport Tanzania kwa mafunzo ya Multi-Engine Instrument Rating (MEIR) mnamo mwezi Julai 2023. Na sasa wamemaliza mafunzo hayo na wamefuzu kuwa marubani wa ndege za kubeba abiria yaani Commercial Pilot Licence with Instrument Rating and Multi – Engine Rating.
Alisema ufadhili wa mafunzo hayo utasaidia watanzania kusomea fani hizo kwani mafunzo hayo ni gharama na watanzania wachache wanaweza kuyamudu. Pia ilionekana kuwa kwenye soko la ajira kuna upungufu wa watanzania kwenye kada hizo.
Aliongeza pia kuwa mnamo mwaka 2022 Mfuko ulipeleka pia mhandisi mmoja katika chuo cha
Ethiopia Academy nchini Ethiopia ambae nae amemaliza masomo yake, na baadae mwaka 2023 walipelekwa wahandisi wengine 10 ambao hivi sasa bado wanaendelea na masomo na wanatarajiwa kumaliza mnamo mwezi Machi 2025.
Na kabla ya hapo, awali wakati mfuko umeanza walisomeshwa marubani wanne, ambao kwasasa wameajiriwa na mashirika mbalimbali, hivyo kwa ujumla mfuko hadi sasa umesomesha wanufaika 23.
Mbali na kutoa taarifa hiyo Bw.Msangi alitoa muhtasari wa mambo mbalimbali yaliyofanyika kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga Duniani (ICAD) ambayo kilele chake ni Desemba 7, 2024. Na kuongeza kuwa Maadhimisho ya mwaka huu pia tunatimiza miaka 80 tangu siku hii ilipoanza kuadhimishwa mnamo Desemba 7 mwaka 1944.
Bw. Msangi alieleza katika kuadhimisha wiki ya usafiri wa anga duniani, Mamlaka kupitia kitengo cha
uhusiano na mawasiliano pamoja na watalaam wake kutoka Idara mbalimbali ilitumia wiki hiyo kujenga uelewa juu ya kazi za Mamlaka katika kuelekea miaka 80 ya usafiri wa anga duniani, hii ikienda sambamba na kutoa uelewa kwa jamii juu ya matumizi ya ndege nyuki (drones) ikiwa ni sheria na taratibu za vibali na leseni kumiliki ndege nyuki hizo.
Alisema elimu hiyo ilitolewa katika vyombo vya habari Radio na televisheni ikiwemo Clouds FM, Radio One FM na Kituo cha Azam TV.
Alisema mbali na vyombo vya habari pia walitembelea baadhi ya shule za sekondari zilizopo mkoa wa Dar es Salaam ikiwa na lengo la kuelimisha na kuhamasisha wanafunzi waliopo mashuleni kusoma kwa bidii na kuweza kuingia kwenye sekta ya anga nchini ambayo inakabiliwa na uhaba wa wataalam wazawa.
Shule zilizotembelewa ni Shule ya Sekondari Kibasila iliyopo wilaya Temeke, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani iliyopo wilaya ya llala, Shule ya Sekondari Makongo iliyopo wilaya ya Kinondoni na Shule ya Sekondari Kwemba iliyopo wilaya ya Ubungo
Pia alisema wiki hiyo ilimalizwa semina kwa njia ya mtandao (Webinar) ikiwa na ujumbe ‘meet the professionals of aviation’ iliyozungimzia maendeleo mbalimbali yaliyofikiwa katika sekta usafiri wa anga nchini Tanzania. Ambapo hoja mbalimbali ziliibuliwa na kufanyiwa majadiliano.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu madhimisho ya Siku ya Usafiri wa Anga Duniani pamoja na kuwapongeza vijana wa kitanzania waliobahatika kupata udhamini wa kusomea urubani na Uhandisi wa Ndege iliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Banana-Ukonga jijini Dar es Salaam.