TRC waongeza ratiba za treni mikoa ya kaskazini

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeongeza safari za treni kuelekea mikoa ya Kaskazini Tanga, Kilimanjaro na Arusha, kutoka safari mbili kwa wiki hadi tatu, huku likitangaza gharama za nauli zitakazotumika.

Kwa mujibu wa  taarifa kwa umma iliyotolewa leo Desemba 7, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Fredy Mwanjala,  safari zitakuwa Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.

Awali treni hiyo ilikuwa na ratiba ya kusafiri katika mikoa hiyo siku za Jumatatu na Ijumaa.

Lakini katika kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, shirika hilo limeongeza safari za treni kuelekea mikoa hiyo.

“Ongezeko hilo la siku ya Jumatano ni hatua mahususi za TRC kukabiliana na ongezeko la abiria katika kipindi hiki hususani kuelekea mikoa ya kaskazini mashariki mwa Tanzania,” amesema.

Pia TRC kupitia taarifa yake imeeleza kuwa kila siku ya Jumatatu kuanzia Desemba 09, 2024 hadi mwanzoni Januari 2025,  itapeleka  mabahewa 18 yatakayobeba abiria takribani 1,000 hadi 1,200 kwa wakati mmoja kuelekea mikoa hiyo.

“TRC inawahakikishia wananchi kwamba hakutakuwa na ongezeko la nauli katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka hivyo nauli zitasalia kama zilivyo sasa,” imeandikwa kwenye taarifa hiyo.

Shirika hilo limetaja mchanganuo wa nauli ni Sh16, 500 daraja la tatu, Sh23, 000 daraja la pili kukaa na Sh39, 100 daraja la pili kulala kwenda Moshi.

Aidha, nauli ya Sh18, 700 daraja la tatu, Sh26, 700 daraja la pili kukaa na Sh44, 400, daraja la pili kulala kwenda Arusha nazo hazitakuwa na mabadiliko.

Related Posts