Dar es Salaam. Mwishoni mwa mwaka hushuhudiwa mabadiliko makubwa katika mifumo ya usafiri kutokana na ongezeko la watu wanaosafiri kwa ajili ya shughuli za sikukuu, familia na biashara.
Kipindi hiki cha msimu wa sikukuu kimekuwa na athari nyingi kwa usafiri wa umma na binafsi, ikiwemo ukosefu wa usafiri wa umma wa kutosha na kuongezeka kwa gharama za nauli.
Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeongeza safari za treni kuelekea mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro na Arusha) kutoka safari mbili kwa wiki hadi tatu, huku likitangaza gharama za nauli zitakazotumika.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Desemba 7, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Fredy Mwanjala, safari zitakuwa Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.
Awali, treni hiyo ilikuwa na ratiba ya kusafiri katika mikoa hiyo Jumatatu na Ijumaa. Lakini katika kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, shirika hilo limeongeza safari za treni kuelekea mikoa hiyo.
“Ongezeko hilo la Jumatano ni hatua mahususi za TRC kukabiliana na ongezeko la abiria katika kipindi hiki hususani kuelekea mikoa ya kaskazini mashariki mwa Tanzania,” amesema.
TRC kupitia taarifa hiyo, imeeleza kuwa kila Jumatatu kuanzia Desemba 9, 2024 hadi mwanzoni mwa Januari 2025, itapeleka mabahewa 18 yatakayobeba abiria 1,000 hadi 1,200 kwa wakati mmoja kuelekea mikoa hiyo.
“TRC inawahakikishia wananchi kwamba hakutakuwa na ongezeko la nauli katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, hivyo nauli zitasalia kama zilivyo sasa,” imeeleza taarifa.
Shirika hilo limetaja mchanganuo wa nauli ni Sh16,500 daraja la tatu, Sh23,000 daraja la pili kukaa na Sh39,100 daraja la pili kulala kwenda Moshi.
Nauli ya Sh18,700 daraja la tatu, Sh26,700 daraja la pili kukaa na Sh44,400 daraja la pili kulala ni kwa ajili ya wasafiri wa kwenda Arusha ambazo nao hazitakuwa na mabadiliko.
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), imesema wanaamini kuanza kwa safari za treni ya umeme (SGR), na mabasi ya mikoani kufanya safari saa 24, huenda mwaka huu kusiwe na adha ya usafiri mwishoni mwa mwaka kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Hata hivyo, Mamlaka hiyo imesema imejipanga vya kutosha kusimamia huduma hizo, ikiwemo kuwadhibiti wale wanaopandisha nauli kiholela.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Latra, Salum Pazzy, amesema hayo alipozungumza na Mwananachi leo Jumamosi, Novemba 7, 2024 kuhusu namna walivyojipanga kudhibiti adha ya usafiri kuelekea msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Pazzy amesema tofauti na miaka ya nyuma wanaamini mwaka huu adha hiyo itapungua kwa kiasi kikubwa kwa kuwa usafiri wa SGR, mtu anaweza kuanza safari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, kisha akachukua basi hapo na kufika siku hiyohiyo Mwanza au Kigoma.
“Dodoma ni mkoa ambao abiria yeyote anaweza kusafiri kwenda mkoa wowote bila ya kulazimika kulala njiani, hivyo mtu akiona hataki kusafiri kwa basi moja kwa moja anaweza kufanya hivyo,” amesema Pazzy.
Amesema tangu SGR imeanza kufanya kazi wamekuwa wakiwashauri wenye mabasi yaliyokuwa yanakwenda katika mikoa ambayo treni hiyo inapita kwenda mikoa mingine na tayari baadhi ya kampuni zimeshafanya hivyo, akieleza huenda kipindi hiki wataongezeka.
Licha ya huduma za usafiri kuboreshwa, Pazzy amesema wapo tayari endepo kutatokea changamoto ya uhaba wa usafiri katika kipindi hiki kutoa vibali vya muda kwa mabasi mengine, lengo likiwa kuwafanya wananchi kupata usafiri bila usumbufu wowote.
Akieleza namna walivyojipanga, Pazzy amesema wameweka udhibiti wa kufuatilia mienendo ya madereva ikiwamo utumiaji wa kitufe cha utambulizi kwa kufuatilia kupitia mfumo wa VTS, ambacho kinawawezesha kujua nani anavyoendesha gari kwa wakati husika na kunapotokea changamoto inakuwa rahisi kumtambua.
“Mfumo huu unasaidia kufuatilia madereva wa masafa marefu ambao hawaruhusiwi kuendesha zaidi ya saa nane kwani ikifika muda huo anapaswa kumpa dereva mwingine,” amesema.
Hata hivyo, Pazzy amesema ili ufanisi uwe mzuri, abiria na wasafirishaji kupata haki zao na kutimizi wajibu wao wameweka kambi za wakaguzi watakaofanya kazi usiku na mchana kufuatilia safari hizo.
“Wakaguzi hao pamoja na kufuatilia madereva, wataangalia matumizi ya tiketi mtandao, kutozidisha ukomo wa mwendo, kutozidisha abiria, uzima wa mabasi na mikanda ya usalama kufanya kazi,” amesema.
Amesema kituo cha huduma cha Latra kwa wateja kitakuwa kikifanya kazi saa 24. Amewataka abiria watakaopata changamoto wasisite kuwapigia.
Pazzy akisema hayo, Desemba 3, 2024, Kamanda Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’anzi akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam alitaja mikakati waliyonayo ya kudhibiti ajali za barabarani mwishoni mwa mwaka.
Kamanda Ng’anzi ametaja mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza kamera ‘tochi’ ili kudhibiti ajali za barabarani akisema askari wenye kamera watakaa maeneo mbalimbali, yakiwamo ya kificho.
Amewataka Watanzania kutowapangia sehemu za kukaa wakati wa kutekeleza jukumu hilo la kubaini mwendokasi wa magari.
Kamanda Ng’anzi alisema mikakati mingine ni kuhakikisha mabasi yanafuata ratiba, kukagua vyombo vyote vya moto, kuongeza askari, kuhakikisha mabasi yanakuwa na madereva wawili, na kuangalia mfumo wa kuratibu mwenendo wa mabasi (VTS).
“Hatutajali askari wetu amejificha au kuonekana, tukiona mbinu ya kujificha inatupa matunda tutaitumia ama kuonekana inatupa matunda tutaitumia au zote mbili hatutaki mtu atupangie tutumie mbinu gani. Lengo letu ni kudhibiti ajali za barabarani,” alisema.
Alisema chanzo kikubwa cha ajali ni mwendokasi na uzembe wa madereva barabarani, hivyo wataimarisha mifumo ya udhibiti wa mwendo, akisema polisi wamejipanga ipasavyo.
Kamanda Ng’anzi alisema wataongeza idadi kubwa ya askari barabarani, akieleza baadhi ya madereva wakiona polisi wengi wanaogopa, jambo litakalowezesha kuimarisha usalama barabarani.
Alisema watakagua mifumo mingi ya magari ikiwemo ya breki na wasiporidhika na gari au chombo cha moto watakizuia kuingia barabarani.
Amewaelekeza makamanda wa kikosi hicho kukamata magari yote mabovu yakiwemo malori yanayotembea na taa moja usiku au magari yenye matairi vipara (yaliyoisha).
“Kutakuwa na vitabu maalumu vya madereva kwenye vituo vitakavyowekwa ili kuhakikisha wanabadilisha usukani, badala mmoja kuendesha umbali mrefu. Tunafanya hivi ili kuwaondolea uchovu madereva wanaotembea zaidi ya saa nane.
“Wale madereva wanaokwenda Kanda ya Ziwa, watabadilisha Singida, wanaokwenda mikoa ya Nyanda za Juu Kusini watabadilishana Iringa. Dereva atashuka na kusaini kitabu kisha dereva mwingine atapanda,” amesema.
Kamanda Ng’anzi amesema kumekuwa na utaratibu wa watu kusafiri na familia zao, baadhi wanaendesha magari mapya kwenda nayo mikoani kwa ajili ya mapumziko.
“Nitoe wito wale madereva wasiokuwa na uwezo wa kuendesha umbali mrefu zaidi ya saa nane, ni bora wachukue madereva wazoefu watakaosafirisha familia zao au wahakikishe wanakuwa na muda mzuri wa kumpumzika.
“Ni hatari sana umebeba abiria halafu unatembea kilomita 1,000 uko peke yako, ukifika mahali unasimamia unaagiza chakula, nyama kisha unashushia kinywaji kitakachokufanya mwili wako usiwe timamu,” amesema.
Amesema ili kudhibiti hilo, watatawanya vipima ulevi ambavyo vitatumika kwa madereva wote watakaokuwa barabarani, wakiwamo wa bodaboda.
“Ukibainika kukutwa na kilevi utakaa mahabusu ambazo zimetengezwa kiasi kwamba zinaweza kuondoa kilevi cha aina yoyote,” amesema.
Kamanda Nga’nzi amesema madereva 259, wakiwemo wa magari ya Serikali na kampuni binafsi wamefungiwa leseni kuanzia Januari hadi Novemba 2024 kutokana na kufanya makosa hatarishi barabarani.