Ushindi Namungo wampa nguvu Mgunda

USHINDI mtamu buana asikuambie mtu. Saa chache baada ya Namungo kupata ushindi wa mabao 2-1 na kutinga hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Tanesco, kocha wa timu hiyo, Juma Mgunda amesema anaona mwanga mkubwa wakati akijiandaa kukabiliana na Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu.

Namungo ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa  Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi katika mechi ya 64 Bora ya michuano hiyo kwa mabao ya Pius Buswita na Erasto Nyoni na mara baada ya mchezo huo Mgunda alisema ushindi umemuongezea mzuka kabla ya kugeukia Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda alisema licha ya kukutana na timu iliyopo First League, lakini  imewapa mchezo mzuri na wa ushindani akiwapongeza wachezaji wa kikosi cha Namungo kwa kufanya kile alichowaelekeza.

“Mchezo haukuwa rahisi kilikuwa ni kipimo sahihi kwetu kupambania nafasi inayofuata. Wachezaji wangu wameonyesha ukomavu na mchezo mzuri ambao umetupa nafasi nyingine kwenye mashindano hayo,” alisema Mgunda na kuongeza:

“Matokeo mazuri tuliyoyapata yamerejesha morali kwa wachezaji wangu kuelekea mchezo wa ligi dhidi ya Kagera Sugar ugenini Disemba 11. Natarajia mwendelezo huu ili kuendelea kujiweka kwenye mazingira mazuri kabla ya kumaliza mzunguko wa kwanza.”

Mgunda alisema hawana matokeo mazuri katika ligi, wakiwa wanakumbuka kupoteza nyumbani kwa mabao 2-0 dhidi ya Yanga na kusisitizhawatarajii kurudia makosa, huku akiweka wazi kuwa kama wapinzani wanapata matokeo ugenini hata wao wanaweza kufanya hivyo.

“Nafasi tuliyopo sio nzuri mimi kwa kushirikiana na wenzangu tumekaa na wachezaji kujua shida iliyopo na kuanza kuifanyia kazi kabla ya kuifuata Kagera Sugar ambayo pia inapambana kujinasua kwenye nafasi iliyopo, hivyo hatutarajii mchezo mwepesi mbinu na maandalizi mazuri ndivyo vitaamua matokeo ndani ya dakika 90.”

Namungo ipo nafasi ya 15 baada ya kucheza mechi 12 ikishinda tatu, hakuna sare, ikifungwa mechi tisa imekusanya pointi tisa, inakwenda kukutana na Kagera Sugar ambayo pia ipo nafasi ya 14 ikicheza mechi 13, ushindi mbili, sare nne na vipigo saba ikikusanya pointi 10.

Related Posts