Usiku wa heshima kwa Yanga Algeria

Dar es Salaam. Ikifika saa 4 usiku leo, wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga watakuwa uwanjani kuvaana na MC Alger mchezo utakaochezwa Uwanja wa 5 July 1962.

Ni mchezo wa kujiuliza kwa Yanga inayonolewa na Kocha Mjerumani, Sead Ramovic ambaye ataiongoza timu hiyo kwa mara ya tatu tangu atambulishwe Novemba 15, 2024, akichukua nafasi ya Muargentina, Miguel Gamondi.

Ramovic anavaana na MC Alger akiwa ametoka kupata ushindi wa mabao 2-0 ugenini katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo, kabla ya hapo alipoteza nyumbani mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Hilal kwa kichapo cha 2-0.

Kitu pekee ambacho kinampa matumaini Ramovic na Wanayanga kwa ujumla ni namna ambavyo kikosi chao kimekamilika kwa maana ya wale waliokuwa majeruhi wamepona na kufanya mazoezi na wenzao huko Algeria.

Wachezaji hao ni Khalid Aucho anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji na mshambuliaji Clement Mzize. Wengine ni Kiungo Aziz Andabwile na beki wa kushoto Chadrack Boka, lakini pia nahodha msaidizi Dickson Job anayecheza beki wa kati, afya yake ipo vizuri baada ya kuumia dhidi ya Namungo na kushindwa kumaliza mchezo huo zikisalia dakika 10.

Mashimo yalionekana waziwazi katika mchezo dhidi ya Al Hilal ambao waliingia kwa mfumo wa kuwasikilizia Yanga kisha kushambulia kwa kushtukiza. Kila Al Hilal waliposhambulia kwa kushtukiza, ilikuwa hatari zaidi, hiyo yote ni kutokana na kukosekana kwa Aucho eneo la kiungo mkabaji, pia upande wa kushoto alipocheza Nickson Kibabage kwenye ulinzi hakufanya vizuri, Boka anaweza kuimarisha eneo hilo.

Wakati Yanga ikiuendea mchezo huo, ni wazi Ramovic ana kazi kubwa ya kufanya ili kusahihisha makosa yaliyotokea katika mchezo uliopita dhidi ya Al Hilal ambapo Yanga ilifunga mabao yote kwa mtindo mmoja wa kushambuliwa kwa kushtukiza.

MC Alger ni timu ambayo inatumia sana mbinu hiyo huku kocha wa zamani wa Simba, Abdelhak Benchikha, akiwapa tahadhari Yanga kwa kuwaambia: “MC Alger inacheza soka la mashambulizi ya kushtukiza, Yanga wanatakiwa kujipanga sana na hilo.”

Katika kipindi cha mwisho cha Gamondi ndani ya Yanga, timu hiyo iliruhusu mabao ya aina hiyo dhidi ya Azam ilipofungwa 1-0 pia dhidi ya Tabora United kwenye kichapo cha 3-1. Ramovic akaendelea hapohapo dhidi ya Al Hilal kabla ya kubadili upepo mbele ya Namungo.

Andy Delort, ndiye anaongoza safu ya ushambuliaji ya MC Alger, anapaswa kuangaliwa kwa zaidi na walinzi wa Yanga lakini pia Kocha wa MC Alger, Patrice Beaumelle anaweza kumtumia winga Kipré Junior kuivuruga Yanga kwani anaifahamu baada ya kukutana nayo mara kadhaa wakati akiitumikia Azam.

Rekodi zinaonyesha kwamba Yanga imekuwa na matokeo mazuri ikicheza uwanja wa ugenini msimu huu tofauti na wapinzani wao wakiwa kwao nyumbani.

Katika Ligi Kuu Bara msimu huu, Yanga imecheza michezo 11 na sita kati ya hiyo ni ya ugenini, ambapo imeshinda yote ikifunga mabao manane, haijaruhusu nyavu zake kutikiswa.

MC Alger katika Ligi ya Algeria, imecheza michezo 10 na mitano kati ya hiyo nyumbani, imeshinda mmoja, sare mitatu na kupoteza mmoja, ikifunga mabao matatu na kuruhusu manne.

Ramovic amesema: “Kila mmoja wetu yupo katika hali nzuri ya kupigania pointi ngumu za kwanza ugenini, utakuwa mchezo wa tofauti kabisa kwa sababu tunahitaji kurejesha morali kwa mashabiki zetu na kuweka matumaini ya kundi letu hai,” alisema na kuongeza.

“Tunahitaji kufanya vizuri zaidi ya tulivyoanza, kuhakikisha hatuwapi nafasi ambazo zinaweza kutugharimu huku tukicheza kwa lengo la kupata pointi tatu ugenini, kama nilivyosema hapo awali kwamba ni mchezo mgumu ila kila kitu kinawezekana.” 

Waswahili wanasema ugeni ni siku ya kwanza tu, lakini ukienda sehemu kwa zaidi ya mara moja, wewe sio mgeni bali ni mgeni mwenyeji kwani utakuwa unajua vichochoro vyote.

Hicho ndicho walichonacho Yanga kwani hii ni mara ya tano wanakwenda Algeria kucheza mechi za Caf kuanzia hatua ya makundi dhidi ya timu za nchi hiyo huku mara moja wakishinda hukohuko.

Pia Yanga sio wageni sana kwenye Uwanja wa 5 July 1962 ambao itautumia kwa mchezo wa leo dhidi ya MC Alger kwani tayari imecheza hapo mara tatu huku mara ya mwisho ikiwa Novemba 24, 2023 katika mchezo wa Kundi D wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad.

Mara ya kwanza Yanga kucheza nchini Algeria ilikuwa Juni 20, 2016 dhidi ya MO Bejaia katika mchezo wa Kundi A michuano ya Kombe la Shirikisho na kupoteza kwa bao 1-0. Kipute hicho kilipigwa Uwanja wa Maghreb Unity.

Mei 6, 2018, ilikuwa ni mara ya pili Yanga kucheza nchini Algeria, safari hii ilikuwa dhidi ya USM Alger katika mchezo wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza kwa mabao 4–0. Mchezo huu ulipigwa Uwanja wa 5 July 1962, ambao ndio watautumia leo kuvaana na MC Alger.

Baada ya mara mbili kupoteza mfululizo nchini Algeria, Juni 3, 2023 Yanga ikafanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, mechi ikichezwa Uwanja wa 5 July 1962.

Licha ya ushindi huo lakini Yanga haikuwa bingwa kutokana na sheria ya bao la ugenini kufuatia matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2. Nyumbani Yanga ilifungwa 2-1, ugenini ikashinda 1-0.

Mara ya nne ilikuwa Novemba 24, 2023 dhidi ya CR Belouizdad na Yanga kupoteza kwa mabao 3–0 ukiwa ni mchezo wa Kundi D wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Uwanja wa 5 July 1962.

Unaweza kusema Yanga ni kama ina njia zake za kupita katika michuano ya Caf kwani mara zote ilizocheza hatua ya makundi, haijawahi kushinda mchezo wa kwanza. Msimu huu imeanza kwa kufungwa 2-0 nyumbani dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Msimu wa kwanza tu tangu michuano ya Klabu Bingwa Afrika ibadilishwe na kuwa Ligi ya Mabingwa mwaka 1997, Yanga iliandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutinga makundi ya michuano hiyo mwaka 1998.

Enzi hizo ilifahamika kama Nane Bora ya Ligi ya Mabingwa na Yanga iliangukia Kundi B sambamba na Asec Mimosas ya Ivory Coast, Raja Casabalanca kutoka Morocco. Pia Manning Rangers ya Afrika Kusini ambayo ilifungua nayo dimba jijini Dar es Salaam na kulazimishwa sare ya 1-1.

Baada ya sare hiyo, Yanga ilisafiri hadi Abidjan, Ivory Coast kuifuata Asec Mimosas iliyoikaribisha kwa kipigo cha mabao 2-1, kisha kuunganisha safari hadi Casablanca nchini Morocco kuvaana na Raja na kutandikwa 6-0, huku ikimpoteza nahodha wake, Kenneth Mkapa aliyelimwa kadi nyekundu dakika za mapema kabisa na kuidhoofisha ngome ya timu hiyo.

Yanga ikarudiana na Raja na kutoka nayo sare ya 3-3, licha ya awali kuonekana kama ilikuwa ikiondoka na ushindi nyumbani kabla ya Waarabu kubadilika dakika za lala salama.

Yanga ikaenda Sauzi, ikachapwa 4-0 na Manning, iliporudi nyumbani dhidi ya Asec Mimosas, ikalala tena mabao 3-0 na kumaliza mkiani ikiwa na pointi mbili tu, ikifunga mabao matano na kufungwa 19.

Baada ya kukaa muda mrefu bila ya kufuzu makundi, mwaka 2016 ikatinga makundi ya Kombe la Shirikisho ambapo mechi ya kwanza ilikuwa ugenini dhidi ya MO Béjaïa ya Algeria na kupoteza kwa bao 1–0. Msimu huo ilimaliza pia mkiani mwa Kundi A ikikusanya pointi nne, ikifunga mabao manne na kuruhusu tisa.

Ishu ya kupoteza mechi ya kwanza ya makundi ilijirudia tena mwaka 2018 katika Kombe la Shirikisho ilipofungwa 4-0 na USM Alger ya Algeria. Yanga ikamaliza mkiani mwa Kundi D ikikusanya pointi nne, huku ikifunga mabao manne na kuruhusu 13.

Msimu wa 2022/23 tena katika Kombe la Shirikisho Kundi D, Yanga ilianza kwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya US Monastir lakini safari hii ikafanya kweli na kufanikiwa kumaliza kinara kwa pointi 13 ikifunga mabao tisa na kuruhusu matatu. Msimu huo ndio ilifika hadi fainali.

Pia msimu uliopita 2023/24 katika Ligi ya Mabingwa, Yanga ilianza kwa kufungwa 3-0 dhidi ya CR Belouizdad, ikaja kumaliza nafasi ya pili kwa pointi nane, ikifunga mabao tisa na kuruhusu sita. Safari yao iliishia robo fainali ikiondoshwa na Mamelodi Sundowns kwa penalti 3-2 baada ya mechi zote mbili matokeo kuwa 0-0.

Mshambuliaji wa Yanga, Kennedy Musonda, amezungumzia kuelekea mchezo wa leo dhidi ya MC Alger akisema: “Wachezaji wengi tumekuwa hapa kwa misimu 2 hadi 3, ukitazama historia, tumepoteza nadhani mara mbili mfululizo kama sio tatu mechi yetu ya ufunguzi (2022, 2023 na 2024).

“Hivyo si kusema tumekuwa tukizoea, lakini angalau tunajua jinsi ya kurudi tukiwa imara,” alisema Musonda ambaye mara zote hizo Yanga ikipoteza alikuwepo kikosini hapo kwani alitua Januari 2023 akitokea Power Dynamos.

“Kwa hiyo sisi jambo muhimu ni kupata matokeo chanya katika mechi yetu inayofuata, tunafanya kazi kwa bidii kuhakikisha tunarudi kwa nguvu,” amesema Musonda.

MWAKA                    MATOKEO                                        UWANJA

20/06/2016 MO Béjaïa    1–0 Yanga    Maghreb Unity

06/05/2018 USM Alger    4–0     Yanga 5 July 1962

03/06/2023 USM Alger    0-1      Yanga 5 July 1962

24/11/2023 CR Belouizdad         3–0     Yanga 5 July 1962

TANO ZA MWISHO MC ALGER NYUMBANI

MC Alger 0-0 Olympique Akbou

MC Alger 1-3 CR Belouizdad

Related Posts