Dar es Salaam. Utata umeibuka kuhusu kifo cha aliyekuwa mfamasia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Magdalena Kaduma.
Taarifa kuhusu kifo chake zimetolewa leo Desemba 7, 2024 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Joseph Kimaro, bila kuelezo zaidi kuhusu sababu za kifo hicho.
“Menejimenti na uongozi wa hospitali unatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wafanyakazi wenzake marehemu kwa msiba huu mzito, imeeleza taarifa ya hospitali hiyo.
Samuel Lusufi, ambaye ni mjomba wa marehemu na msemaji wa familia, akizungumza na Mwananchi kuhusu msiba huo amesema maswali yote waulizwe polisi kwa kuwa kifo hicho ni cha kijinai.
“Ni kweli tumepata msiba, lakini kwa sasa mambo haya tumeshayafikisha polisi. Tuliripoti polisi Gogoni, Kibamba kwa kuwa tukio limetokea huko, kwa hiyo yote waulizwe polisi,” amesema Lusufi.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema anazo taarifa kuhusu tukio hilo lakini hakutoa ufafanuzi zaidi.
Kuhusu taratibu za mazishi, Lusufi amesema wanasubiri taarifa za polisi.
“Polisi walifika nyumbani kwake huko Kibamba wakachukua vielelezo wakaondoka, hivyo waulizwe kila kitu,” amesema.
Mwananchi lilifika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke ambako mmoja wa watumishi alisema wamepata taarifa za kifo chake na mwili uko Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi.
“Kifo chake kilibainika kuwa na utata, mwili umepelekwa Muhimbili, inadaiwa huyo dada aliuawa. Hapa hospitali tunasubiri taarifa za uongozi tujue ni wapi anazikwa na wapi ataagwa,” amesema mtumishi huyo ambaye hakutaka kutajwa jina.
Hata hivyo, mmoja wa ndugu wa familia hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina alidai Magdalena ameuawa na mwili wake ulizikwa nyumbani kwake eneo la Kibamba wilayani Ubungo, siku tatu zilizopita.
“Alipotea kama siku mbili zilizopita, kwa hiyo tukawa tunamtafuta. Mama (Sophia Kaduma) alikwenda Kibamba na ndugu wengine wakamtafuta, wakaenda hospitali, mochwari na vituo vya polisi bila mafanikio.
“Jana (Desemba 6) mama mzazi akashauri warudi nyumbani Kibamba kwa kuwa hicho kiwanja walichojenga alimpa mwanaye, anakijua. Wakiwa hapo alikuwa anazunguka nje ya nyumba, ndipo akaona mahali panadidimia.
“Akauliza hapa kuna nini, mbona kama kuna kitu kimefukiwa? Ikabidi waite polisi, walipokuja walifukua na kuukuta mwili wa Magdalena ukiwa umefunikwa shuka,” amedai.
“Inasemekana walikuwa na ugomvi wa muda mrefu na mume wake,” amesema ndugu huyo.
Akizungumza na Mwananchi mmoja wa marafiki wa Magdalena amedai walikuwa na safari ya kikazi kwenda Dodoma Jumatatu Desemba 2, 2024.
Amedai jioni wenzake waliokuwa wasafiri pamoja, walimtafuta mwenzao kwa simu lakini hakupatikana.
Kwa mujibu wa rafiki huyo, walipomkosa waliamua kumpigia mume wake ambaye alisema yeye alipoondoka nyumbani asubuhi, alimwacha Magdalena.
Baada ya siku kupita, rafiki huyo alimtafuta jirani wa Magdalena ambaye alisema hajamuona, lakini maeneo jirani na nyumbani kwake kuna harufu kali inayoashiria uwepo wa kitu kilichooza.