Wakizungumza katika kongamano la kitaifa la afya ya uzazi kwa vijana, Dr. Felix Bundala, Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Watoto Watoto na Vijana katika Wizara ya Afya, na Dr. Dinah Mbaga kutoka Women Fund Trust (WFT), wamehimiza wadau kuongeza juhudi za kuwafikia vijana na kupambana na changamoto zinazowakabili.
Dr. Felix Bundala alisema, “Tunapozungumzia vijana, tunaongelea kundi muhimu sana. Tuliweka misingi ya kuwa na kauli moja ya kuwafikia kupitia shule, vyuo, na jamii. Lazima pia tufanye ufuatiliaji kuhakikisha miradi yetu inaleta matokeo chanya.”
Kwa upande wake, Dr. Dinah Mbaga alisisitiza umuhimu wa kuelimisha vijana kuhusu haki zao za msingi, ikiwemo kujithamini, kujitambua, na kujilinda dhidi ya ukatili wa kijinsia. “Tufanye kazi kwa pamoja kubadili Sheria ya Ndoa ya 1971 na kupinga ndoa za utotoni ili kumwezesha mtoto wa kike kufikia ndoto zake,” alisema.
Wadau waliombwa kushirikiana kwa karibu ili kuimarisha afya ya uzazi na haki za vijana kwa ujumla.