JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa wanne kwa kosa la mauaji ya Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Amani Kamguna Simbayao kilichotokea baada ya kushambuliaji wa raia maeneo ya Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa iliyotolewa leo na Taarifa iliyotolewa leo tarehe 7 Disemba, 2024 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro imewataja watuhumiwa hao ni pamoja na Deogratius Paul Masawe (49), Mkazi wa Tegeta kwa ndevu na Idd Bakari (30), Mkazi Tegeta kwa ndevu ambao wote ni Makuli, pia Omar Issa (47) Mpiga debe Mkazi wa Tegeta Dawasco na Rashid Mtonga (29) Dereva bodaboda Mkazi wa Bunju.
Inaeleza kuwa watuhumiwa hao wanashikiriwa kwa tuhuma za kufanya mauaji ya Mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania aitwaye Amani Kamguna Simbayao pia kumjeruhi Adriano Fredrick wa TRA.
“Watuhumiwa hao na wengine ambao bado wanahojiwa kwa kina walikamatwa baada ya kuwashambulia Maafisa hao wa TRA wakati wakitekeleza majukumu yao ya kisheria, waliliharibu pia gari STL 9923 Toyota Land Cruiser mali ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.
“Tukio hilo lilitokea tarehe 5 Disemba , 2024 majira ya saa 3:00 usiku maeneo ya Tegeta kwa Ndevu, Kinondoni jijini Dar es Salaam, baada ya Maafisa hao wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukamata gari T 529 DHZ aina ya BMW rangi nyeupe lililodaiwa kuwa na makosa ya kikodi,” iliandika taarifa hiyo.
Jeshi la Polisi Kanda Maaalum ya Dar es Salaam linawaonya vikali na halitavumilia watu ambao wanataka kujenga tabia ya kuwashambulia watumishi wa Serikali wakati wakitekeleza majukumu yao licha ya kuwa wanakuwa wamefuata taratibu zote za kisheria, Jeshi halitasita kuchukua hatua kali za haraka na za kisheria dhidi ya Wahusika kwa kuwafikisha kwenye Mamlaka nyingine za haki.