Wanne wakamatwa kwa tuhuma za mauaji ya ofisa TRA

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya dereva la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Iman Simbayao aliyefariki dunia jana Ijumaa Disemba 6, 2024 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Kamanda Jumanne Muliro ameeleza hayo leo Jumamosi Disemba 7, 2024 wakati akizungumza na wanahabari akisema watuhumiwa hao wanahojiwa.

Simbayao ni miongoni mwa maofisa watatu walioshambuliwa na wananchi Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es Salaam, walipokuwa wakitaka kukamata gari linalodaiwa kuingizwa nchini kimagendo.

Taarifa za kifo chake zilitolewa jana usiku Ijumaa Desemba 6, 2024 na mamlaka hiyo kupitia taarifa kwa umma iliyopochapishwa katika mitandao yake ya kijamii.

“Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inasikitika na kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa kutokana na kifo cha mtumishi wetu wa TRA, Amani Kamguna Simbayao kilichotokea leo mchana wa Desemba 6, 2024 (jana) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa baada ya tukio la shambulio akiwa katika majukumu yake ya kikazi kwa masilahi ya Taifa katika eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es Salaam.

Pia katika taarifa hiyo TRA imesema: “Tunatarajia wahusika wote watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.”

Tukio hilo la kushambuliwa kwa ofisa huyo akiwa na wenzake wawili lilitokea usiku wa Desemba 5, 2024 wakati watumishi hao wakiwa kwenye gari la Serikali.

Endelea kufuatilia Mwananchi na mitandao yake.

Related Posts