Yanga imepoteza mchezo wa pili mfululizo wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa mabao 2-0 na wenyeji wao MC Alger ya Algeria.
Ikicheza vizuri dakika 45 za kwanza na kuonyesha nidhamu kubwa, wawakilishi hao wa Tanzania kwenye mashindano hayo, ilipoteana kipindi cha pili na kuruhusu bao la kichwa dakika ya 64, lililofungwa na beki na nahodha wa MC Alger, Ayoub Abdelaoui akitumia shambulizi la mpira wa adhabu ndogo.
Baada ya bao hilo, Yanga ikapanga mashambulizi yake kwa Alger iliyokuwa ikicheza mechi yake ya kwanza nyumbani bila mashabiki baada ya kufungiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutokana na vurgu za mashabiki wao, hata hivyo, ikashindwa kupiga shuti hata moja langoni mwa wapinzani.
Umakini mdogo wa kumalizia wa washambuliaji Kennedy Musonda na Maxi Nzengeli uliinyima Yanga nafasi kusawazisha bao.
Wakati Yanga ikipambana kutafuta bao la kusawazisha ikajikuta inapigwa bao la pili dakika ya 90+1, mfungaji akiwa mshambuliaji Soufiane Bayazid aliyeingia kipindi cha pili, akitumia makosa ya beki wa Yanga Bakari Mwamnyeto na kipa wake Djigui Diara waliojichanganya na kushindwa kumdhibiti, mfungaji aliyeudokoa mpira na kumpita kipa kisha kubaki mwenyewe na goli na kufunga.
Haya ni matokeo ya pili mabaya kwa Yanga na kabla ya mchezo huu, ilipoteza dhidi ya Al Hilal ya Sudan nyumbani kwa mabao 2-0 na mabingwa hao wa soka wa Tanzania inaendelea kuburuza mkia bila pointi yoyote kwenye msimamo wa kundi A.
Hiki ni kipigo cha pili kutoka kwa Alger zikikutana mara ya tatu na mwaka 2017 ilifungwa mabao 4-0, mchezo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya awali Yanga kushinda bao 1-0 nyumbani.
Yanga itasafiri hadi DR Congo kucheza dhidi ya mabingwa wa nchi hiyo, TP Mazembe Desemba 14, ukiwa ni mchezo wa tatu wa kundi hilo.