Bajana, Zayd wamkosha Taoussi | Mwanaspoti

KOCHA wa Azam FC, Rachid Taoussi, ameonyesha kuridhishwa na viwango vya viungo wake, Sospeter Bajana na Yahya Zayd, baada ya kuongoza timu hiyo kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao 4-0 dhidi ya Iringa SC kwenye mchezo wa raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho (FA).

Ushindi huu unakuwa ni wa nane mfululizo kwa Azam FC katika mashindano yote huku mechi saba ikiwa za Ligi Kuu Bara, hatua ambayo inamfanya kocha Taoussi kuwa na matumaini makubwa msimu huu.

Kwa mara ya kwanza, Bajana na Zayd, ambao walikuwa wakitibu majeraha kwa pamoja walipata nafasi ya kuanza kwenye mechi hii. Ufanisi wao ulionyesha wazi kwamba Azam FC ina kikosi kilichoongezeka nguvu, huku Bajana akifunga bao moja kwenye mchezo huo.

Akizungumzia kuhusu mchezo huo, Taoussi alikiri kutoridhishwa na kiwango cha timu yake katika kipindi cha kwanza, ambapo alielezea kwamba walikosa umakini na kupoteza mipira mara kwa mara kabla ya kubadilika.

“Katika kipindi cha kwanza, hatukufanya vizuri, tulikosa kuutawala mchezo vile nilivyokuwa nikihitaji na kupoteza mipira isivyo lazima,” alisema Taoussi na kuongeza;

 “Lakini kipindi cha pili, wachezaji walijitahidi na walionesha kiwango bora. Ni furaha yangu kuwaona Bajana na Zayd wakicheza kwa kiwango cha juu, na walisaidia sana kuleta ushindi huu.”

Kwa upande wa Bajana, ambaye alifunga bao moja, na Zayd, ambaye alikuwa na kitambaa cha unahodha, Taoussi alisema, “Kwa mara ya kwanza, tuliona umuhimu wa wachezaji hawa kwenye kikosi. Wamefanya vizuri na naamini wanamengi ya kuonyesha bado kwenye timu yetu.”

Kocha Taoussi alitaja kwamba ushindi huu wa 4-0 ni muhimu, lakini bado kuna changamoto kubwa mbele. “Nina furaha kuona timu yangu ikiendelea kufanya vizuri, lakini bado tunahitaji kuboresha baadhi ya maeneo. Kwa sasa, ushindi huu unatufanya kuwa na morali kubwa, na tunajivunia kuweza kufikia ushindi wa nane mfululizo,” alisema Taoussi.

Mbali na Bajana na Zayd, wachezaji wengine ambao nao walipata nafasi kwenye mchezo huo ni pamoja na Zuberi Foba (kipa), Ever Meza, Mamadou Samake, Cheick Diakite, Adam Adam, Franck Tiesse, na Daud Paul.

Hata hivyo urejeo wa Bajana na Zayd unampa Taoussi mchaguo zaidi kwenye eneo la kiungo. Hata hivyo, ushindani mkubwa utaendelea kuwa eneo hilo kutokana na uwepo wa Adolf Mtasigwa na James Akaminko.

Related Posts