Waziri wa fedha Dkt. Mwigulu Nchemba akiwafariji wafiwa mara baada ya kuaga mwili wa aliyekuwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Aman Kamguna Simbayao leo Desemba 08, 2024 katika Viwanja vya Michezo TRA vilivyopo Kurasini jijini Dar es Salaam. Amani alifariki Dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha Mifupa -Moi-Dar es salaam baada kushambuliwa na watu katika eneo la Tegeta kwa Ndevu, jijini Dar es Salaam, tarehe 6 Disemba, 2024 akiwa anatimiza majukumu ya kazi yake kwa majibu wa sheria.
Waziri wa fedha Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza wakati wa kuaga mwili wa
aliyekuwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Aman Kamguna Simbayao leo Desemba 08, 2024 katika Viwanja vya Michezo TRA vilivyopo Kurasini jijini Dar es Salaam. Amani alifariki Dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha Mifupa -Moi-Dar es salaam baada kushambuliwa na watu katika eneo la Tegeta kwa Ndevu, jijini Dar es Salaam, tarehe 6 Disemba, 2024 akiwa anatimiza majukumu ya kazi yake kwa majibu wa sheria.
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ameahidi kuwahudumia kimahitaji watoto wawili wa marehemu, Amani Kamguna Simbayao, aliyekuwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, aliyefariki Dunia katika Hospitali ya Taifa ya Mifupa Muhimbili-Moi-Dar es salaam, aliyefariki dunia kwa kushambuliwa na watu katika eneo la Tegeta kwa Ndevu, jijini Dar es Salaam, tarehe 6 Disemba, 2024.
Dkt. Nchemba ametoa ahadi hiyo wakati akiongoza waombolezaji kuuaga mwili wa marehemu katika Viwanja vya Michezo vya TRA, Kurasini Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba. Amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maanry Mwamba, ambaye aliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu, Bw. Elijah Mwandumbya, katika tukio hilo, na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bw. Yusuf Juma Mwenda, kuhakikisha kuwa kiasi cha shilingi milioni 200 kinatafutwa kwa ajili ya kuanzisha Mfuko Maalum utakao tumika kuwanunulia watoto hao (Najimu Amani Sumbayao (8) na Badria Amani Simbayao (3), pamoja na mama yao, Bi. Arafat Abdalla Ukomo, Hati Fungani za Benki Kuu ya Tanzania, kwa ajili ya uhakika wa kupata huduma stahiki kama vile elimu na mambo mengine.
Maelekezo hayo yanafuatia maombi yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila, wakati alitoa salam za Mkoa wake, ambapo alipendekeza uwepo mpango mahsusi wa kuisaidia familia hiyo kimaisha ili iwe motisha kwa familia hiyo iliyopoteza shujaa aliyemwaga damu yake wakati akilitumikia Taifa.
Marehemu Amani Simbayao, alikuwa Afisa Usafirishaji (dereva) wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, ambaye alipigwa na kuumizwa vibaya na watu akiwa kazini na wafanyakazi wenzake wengine wawili katika eneo la Tegeta Kwa Ndevu, Jijini Dar es Salaam. wakati walipokuwa wakilifuatilia gari moja lililokuwa linashukiwa kukiuka masuala ya kiforodha.
Katika tukio hilo la kuuaga mwili wa marehemu, Mhe. Dkt. Nchemba, alilaani vikali tukio hilo la watu kujichukulia Sheria mkononi na kumuua Mtumishi asiye na hatia hata baada ya kujitambulisha kuwa ni Mtumishi wa TRA, na ametoa wito kwa vyombo vya dola kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote waliohusika na tukio hilo baya ili liwe fundisho kwa watu wengine.
Aliwatia moyo wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wasikatishwe tamaa na tukio hilo, bali waendelee kuchapakazi kwa bidii kwa manufaa ya Taifa.