BEKI wa Kitanzania, Haji Mnoga anayekipiga Salford City inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu, huko England anatarajiwa kuwavaa wababe wa Ligi Kuu ya England (EPL), Man City katika mechi ya Kombe la FA itakayopigwa Januari 11 mwakani.
Nyota huyo kabla ya kujiunga na klabu hiyo ya Ligi Daraja la Tatu msimu huu, alipita Portsmouth, Aldershot Town na Gillingham za England na amekuwa akitumika mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo inayoshika nafasi ya 12 kati ya 24 za ligi hiyo maarufu kama EFL League Two.
Salford itashuka uwanjani mwezi ujao kwenye raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la FA dhidi ya Man City ya Pep Guardiola.
Beki huyo wa kulia hivi karibuni amekuwa mhimili mkubwa wa timu hiyo kwenye eneo la ulinzi na huenda akaanza katika mchezo huo kutokana na mwendelezo mzuri wa kiwango chake.
Kama ataanza mbele ya Man City atakuwa na kazi ya kumzuia winga, Jeremy Doku na Matheus Nunes ambao wamekuwa wakicheza upande wa Mtanzania huyo.
Kwenye mechi 18 za Ligi ilizocheza Salford, Mnoga amecheza 16 akikosa mechi mbili na kutumika kwa dakika 1,002.
Beki huyo aliitumikia timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwenye mechi nane zikiwamo zile za fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) kule Ivory Coast mwaka jana.