KOCHA wa KenGold, Omary Kapilima amekiri timu hiyo kupitia kipindi kigumu baada ya kushuhudia ikiondolewa hatua ya 64 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho na Mambali FC ya Tabora, ikiwa ni mwendelezo mbovu wa kikosi hicho msimu huu.
Timu hiyo ilikumbana na kichapo hicho cha kutolewa kwa penalti 4-3, baada ya sare ya kufungana bao 1-1, ndani ya dakika 90 na kukifanya kufikisha jumla ya michezo saba mfululizo bila ya ushindi, jambo linalompa wakati mgumu zaidi Kapilima.
“Licha ya kutolewa kwa penalti ambazo kiuhalisia hazina mwenyewe ila hatuna kisingizio juu ya hilo, hatukustahili kufika hadi huko, ni kipindi kigumu ambacho tunapitia na tunapaswa kuhakikisha tunaamka kwa haraka ili kuokoa hali iliyopo.”
Kapilima alisema tayari ametoa mapendekezo yake kwa viongozi kwa ajili ya kuboresha maeneo mbalimbali ambayo anaamini itakuwa chachu ya kukirejesha kikosi hicho katika ushindani, ikiwemo kuanzia eneo la ulinzi, kiungo na ushambuliaji.
Kocha huyo aliyezifundisha na kuchezea timu mbalimbali zikiwemo za, Majimaji, Yanga na Mtibwa Sugar amejiunga na kikosi hicho Oktoba 22, mwaka huu akichukua nafasi ya Fikiri Elias aliyeamua kuondoka mwenyewe kikosini Septemba 17, mwaka huu.
Fikiri aliondoka kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo ambapo aliiongoza katika michezo mitatu tu ya Ligi Kuu Bara na kati yake alipoteza yote akianza na mabao 3-1, dhidi ya Singida Black Stars, (2-1) na Fountain Gate kisha 1-0 na KMC.
Baada ya hapo kikosi hicho kikaongozwa na Jumanne Challe aliyeipandisha timu hiyo Ligi Kuu Bara wakati ikishiriki Ligi ya Championship, ambapo katika michezo yake mitano aliyoiongoza alishinda mmoja, akitoa sare mmoja na kupoteza mitatu.
Kitendo cha Challe kutokuwa na sifa za kusimamia benchi la ufundi kwa zaidi ya michezo mitano ya Ligi Kuu Bara, ndipo Kapilima akajiunga na kikosi hicho na kukiongoza katika mechi tano akianza na kichapo cha mabao 4-1, dhidi ya Azam FC.
Baada ya hapo, timu hiyo ikatoka sare ya mabao 2-2 na Dodoma Jiji, ikachapwa bao 1-0 na Tanzania Prisons, sare ya 1-1 na Coastal Union, ikapoteza 1-0, dhidi ya Pamba katika michezo ya Ligi ya Kuu, kisha ikatolewa Shirikisho na Mambali FC.
Timu hiyo mara ya mwisho kushinda ilikuwa ni ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania Oktoba 4, mwaka huu ukiwa ni ushindi pekee hadi sasa katika michezo 13 ya Ligi Kuu iliyocheza, baada ya kutoka sare mitatu na kuchapwa tisa.