Mambo haya yanaharibu ufanisi wako kazini

Tofauti kati ya maeneo ya biashara, ujasiriamali, kazi za kuajiriwa, au shughuli nyinginezo kama matumizi ya barabara na maisha ya familia, mara nyingi hujikita katika maadili yanayotawala maeneo hayo.

Ni takriban asilimia 5 hadi 10 tu ya watu wanaofuata maadili ya kazi kikamilifu, huku wengi wakiendeshwa na mazoea na hali walizozikuta, bila kujiuliza kama mifumo hiyo inasaidia kukuza au kudumaza taaluma zao.

Mazoea haya yamekuwa yakitufanya kila mara kulalamikia ukosefu wa maendeleo ambayo hatuyaoni na hata kama yatafikiwa, basi yatachukua muda mrefu.

Hebu tujiulize, je, hujawahi kuona mfanyakazi akisoma gazeti kazini wakati kazi zimemsubiri?

Si tu kwamba wanasoma, bali pia wanajadili yaliyomo magazetini kwa muda mrefu bila kujali majukumu yao.

Hii haimaanishi kuwa magazeti ni mabaya, bali mfanyakazi anaposhindwa kupanga muda wake vema, hupoteza muda wa kazi kwa mambo yasiyo na tija.

Mtu huyu huyu huenda akalalamikia ugumu wa maisha, bila kujua kuwa anapoteza rasilimali muhimu ya muda pasi kujua thamani yake.

Vikao visivyo rasmi kazini

Katika mazingira mengi ya kazi, kuna vikao vya wafanyakazi visivyo rasmi vinavyojadili mambo nje ya ofisi.

Mazungumzo hayo ingawa yanaweza kuonekana kufurahisha, lakini mara nyingi huchukua muda mwingi uliopaswa kutumika kutekeleza majukumu yake ya kazi.

Halafu mwisho wa siku, wafanyakazi haohao hulalamika tena kuhusu malipo ya mishahara midogo au faida ndogo ya kampuni au taasisi bila kuelewa kuwa wao wenyewe ndio wanachangia uwapo wa hali hiyo.

Tabia za kula na mapumziko

Wafanyakazi wengi wanapanga ratiba zao kwa kuzingatia muda wa kula badala ya kazi. Simu nyingi za asubuhi zinaahirishwa hadi muda wa chakula cha mchana, hali inayodhihirisha kwamba wafanyakazi wengi hutumia muda mwingi wa kufikiria muda wa mapumziko badala ya utendaji kazi.

Mfanyakazi anayetoa kipaumbele kwa marafiki, ndugu, au watu wa karibu badala ya kuwahudumia wateja wote kwa usawa, anakosa kufuata maadili ya kazi.

Maadili yanapaswa kutanguliza haki sawa kwa kila mteja anayefika kwenye kampuni au taasisi hiyo, bila kujali uhusiano wa kifamilia au kihisia.

Kuchelewa na kuwahi kazini

Ni jambo la kawaida kwa wafanyakazi kuchelewa kufika kazini lakini kuwahi kutoka, hasa katika maeneo ambayo hawawajibishwi ipasavyo. Hali hii huathiri uzalishaji wa kazi na inachochea malalamiko kuhusu ukosefu wa maendeleo au mshahara mdogo.

Katika miaka ya hivi karibuni, wafanyakazi wengi huamua kuzianza wikiendi mapema zaidi, na wengi huianza Alhamisi badala ya Ijumaa jioni.

Lakini watafiti wanasema cherekochereko za wikiendi zinapunguza ufanisi wa kazi siku za mwanzo wa juma, hasa kwa wale waliozitumia siku hizo kufanya starehe hasa ya kunywa pombe au burudani kupita kiasi.

Mazoea haya yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito kwa sababu nayo pia huchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza ufanisi wa kazi na maendeleo ya taaluma.

Kila mfanyakazi anapaswa kuzingatia maadili ya kazi na kujiuliza ikiwa mienendo yake inajenga au inadumaza utendaji wake.

Related Posts