Dar es Salaam. Kutokana na utata unaozunguka kifo cha aliyekuwa mfamasia wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke (TRRH), Magdalena Kaduma, mama yake mzazi ameelezea jinsi alivyopokea taarifa za kupotea kwa binti yake.
Magdalena alitoweka Desemba 3, 2024, nyumbani kwake Kibamba, jijini Dar es Salaam, mwili wake ulipatikana ukiwa umefukiwa pembezoni mwa nyumba aliyokuwa akiishi.
Mama mzazi wa marehemu, Sophia Kaduma, leo Jumapili, Desemba 8, 2024, akiwa nyumbani kwake kwenye msiba, amesimulia jinsi ilivyotokea.
Sophia amesema siku ya tukio, Jumatano asubuhi alipigiwa simu na mume wa marehemu, Kenan Mwandalima akimtaarifu kuwa mkewe hapatikani na hajulikani alipo.
“Mumewe alinipigia simu na kuniuliza kama Magdalena alikuwa nyumbani kwangu kwa sababu hajamuona,” amesimulia mama huyo.
Baada ya kupokea taarifa hizo, Sophia amesema alipata wasiwasi, hivyo akaamua kuchukua hatua za haraka kufuatilia zaidi taarifa hizo.
“Familia ilianza juhudi za kumtafuta Magdalena katika maeneo mbalimbali, huku tukijaribu kufahamu mazingira yaliyosababisha kutoonekana kwake,” amesimulia mama huyo.
Amesema walipofika nyumbani kwake Kibamba, alimhoji mumewe kuhusu kilichotokea na kwa nini hakuchukua hatua za haraka alipoona mkewe hapatikani nyumbani.
“Nilifika katika hali ambayo nafsi ilikuwa nzito, niliona kuna eneo lilikuwa limelimwa lina mboga na miwa, lakini pembeni yake kama kumepaliliwa ndipo nikasogea kuangalia nilijikuta nimekanyaga sehemu kukawa kunabonyea, ikabidi nimshirikishe mdogo wangu,” amesimulia Sophia.
Baada ya kuona hivyo, amesema ikabidi asogee mpaka eneo lililolimwa kwa sababu palikuwa panaonyesha hapajalimwa siku nyingi, alipolifikia eneo hilo na kadiri alivyokuwa akipiga hatua hakukuonyesha kama ni pa siku nyingi, na alipopiga hatua zaidi alijikuta amekanyaga sehemu iliyokuwa inabonyea kama godoro.
“Tulivyoona hivyo tukasema hapa kuna jambo si salama, ikabidi tuite vyombo vya usalama na wao wakaamrisha pafukuliwe, ndipo ulipotolewa mwili wa Mage ukiwa umefungwa kwenye shuka.
“Baada ya kumfunua alikuwa kama mtu aliyekatwa na kitu shingoni, maana hata ulimi ulitoka nje,” ameeleza mama huyo.
Baada ya mwili wa Magdalena kupatikana, mama huyo amesema alikamatwa na Jeshi la Polisi, huku msaidizi wao wa kiume akitokomea kusikojulikana na mpaka leo jioni alikuwa hajapatikana.
Mama mzazi wa Magdalena amesema hakuwahi kupewa taarifa na marehemu kuwa alikuwa na matatizo yoyote na mumewe.
“Ukimya wake umetufanya tushindwe kuelewa chanzo cha kifo chake kwa sababu hakuna anayejua sababu ya mauaji hayo, hata kuhisi tu,” amesema mama huyo.
Hata hivyo, mama huyo amesema kifo ni mipango ya Mungu, mwili wa Magdalena unatarajiwa kusafirishwa kuelekea Makambako, mkoani Njombe kesho Jumatatu Desemba 9, 2024 kwa maziko yatakayofanyika Jumanne, saa nne asubuhi.
Hata hivyo, baadhi ya ndugu wa karibu wameliambia Mwananchi kuwa baada ya mume huyo kukamatwa na kuanza kuhojiwa na polisi, alikuwa akitaja jina la Hans kama mtu anayejua ukweli wa tukio hilo.
Magdalena alifunga ndoa na mumewe mwishoni mwa mwaka 2018 katika Kanisa la Efatha. Mume wake alikuwa Katibu wa tawi la Kibamba la kanisa hilo. Hata hivyo, hawakubahatika kupata watoto.
Mwili wa Magdalena ulifukiwa kwenye migomba ya ndizi, umbali kidogo kutoka nyumbani kwao, karibu na mpaka wa eneo lao.
Akisimulia hali ilivyokuwa, jirani aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Saidy ameeleza mume wa marehemu alikuwa akilia kwa sauti wakati mwili ukifukuliwa, akisisitiza aliyehusika lazima ajulikane.
Amesema jirani na shimo hilo walikuta jembe limetelekezwa.
Amesema hata ndani ya nyumba yao waliikuta pete ya ndoa ya marehemu, umbali kutoka eneo alipofukiwa Magdalena na nyumba yao ni mdogo, jambo linalozua maswali zaidi kuhusu madai ya mume kwamba alimtafuta mkewe bila mafanikio.
Mwananchi ilimtafuta Mwenyekiti wa Mtaa wa Hondogo, Leonad Peter amesema alilijua tukio baada ya wazazi wa Magdalena kwenda ofisi kwake Ijumaa kuripoti kutomuona mtoto wao wala kuwasiliana naye tangu Jumatano.
“Baada ya kunieleza tatizo hilo kwa kweli tulifunga safari pamoja na wazazi wa marehemu Magdalena wote wawili hadi kituo cha polisi Gogoni, baada ya kuwaeleza mtu kapotea walituambia kwa kuwa tumekwenda kutoa taarifa watafuatilia,” amesema.
Leonad amesema wakati wanarudi walikwenda hadi kwenye nyumba hiyo wakawa wanafuatilia na walipokwenda hadi sehemu moja kuna migomba ya ndizi, waliona kulikuwa kumelimwa baada ya kusimama waliona kunatitia.
“Tulichukua mti na kuanza kufukua kuangalia na tukauona mwili umefukiwa na tulitoa taarifa, polisi wakaja,” amesema Leon.