Mbio za uenyekiti za Mbowe, Lissu zinavyoigawa Chadema

Dar/mikoani. Uamuzi wa Tundu Lissu kukusudia kuchuana na Freeman Mbowe katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Chadema, umekigawa chama hicho pande tatu huku sababu za Lissu kuamua kuchukua hatua hizo zikibainika.

Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara anatarajia kutangaza nia hiyo wakati wowote kumvaa mwenyekiti wake, Mbowe kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mapema mwakani.

Si Mbowe ambaye tangu mwaka 2004 anakiongoza chama hicho akimrithi Bob Makani aliyeshika usukani kutoka kwa Edwin Mtei au Lissu aliyejitokeza hadharani na kusema kuwa atawania uenyekiti.

Hata hivyo,  wapambe wa kila mmoja, wamejitokeza na kuwapigia chapuo wakidai kuwa wanaweza kukiongoza chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Mbali na nafasi ya uenyekiti wa chama hicho kilichoanzishwa mwaka 1992, wawili hao kwa mujibu wa vyanzo vyetu,  wanatajwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao mwakani.

Katikati mwa Agosti 2024, Lissu alisema amemwandikia barua Katibu Mkuu, John Mnyika kuonesha kusudiao lake la kuwania urais na kutetea umakamu mwenyekiti-bara. Mnyika alithibitisha kupokea barua hizo.

Awali, uchaguzi mkuu wa Chadema ulikuwa ufanyike Septemba 2024 ukasogezwa mbele kwa sababu kadhaa miongoni ni kutokamilika kwa chaguzi za ndani, rasilimali fedha na kupisha uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Jumatano ya Novemba 27, 2024.

Kutokana na sababu hizo, Chadema ilipanga kufanya uchaguzi mkuu Desemba hii, lakini suala la ukata bado limekikwamisha na sasa umesogezwa tena  hadi Januari au Februari mwakani.

Mwananchi lina taarifa za kina kutoka kwa viongozi waandamizi wa Chadema na wanachama, kuhusu kinachoendelea baada ya Lissu kuonesha nia hiyo.

Uamuzi huo wa Lissu kutaka kuwania nafasi hiyo umeibua mijadala mikali ndani na nje ya Chadema.

Katika makundi sogozi ya mtandao wa WhatsApp,  wanachama wanapigana vijembe, huku  kila mmoja akivutia kwa yule anayemuunga mkono.

Hatua hiyo ya Lissu kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi,  umekigawa chama katika makundi matatu.

La kwanza ni lile ambalo linaona Mbowe baada ya kuongoza kwa miaka 20 tangu mwaka 2004 anatosha ama anapaswa kupumzika.

Kundi la pili ni lile linalomuunga mkono Lissu likiamini ndio wakati wake kupokea kijiti cha Mbowe.

Pia kuna kundi la tatu la  wale ambao wako kimya, hawasemi kama wako upande wa Mbowe ama Lissu wakiangazia jinsi hali inavyokwenda.

Katika mitandao ya kijamii  kumekuwa na taarifa za Lissu kufanya mkutano na waandishi wa habari.

 Awali, mkutano huo ulikuwa ufanyike wiki iliyopita Dar es Salaam lakini ukahamishiwa Dodoma na sasa umerejeshwa tena Dar es Salaam.

Hakuna sababu zilizotolewa na washirika wa Lissu. Vipande vya video vya kuonesha Lissu anastahili na atatangaza nia hiyo karibuni vimetengenezwa.

Aidha, kuna vipande vya Mbowe akioneshwa kuwa  ni ‘mwamba’ wa kukivusha chama kwenye nyakati mbalimbali.

Minyukano hiyo imekuwa ikiwaibua hata  wasio wana-Chadema kuizungumzia kwa kuchangia kama alivyofanya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, alipokuwa akitoa nasaha zake baada ya makada wa Chadema kushambuliana:

“Kuna maisha baada ya uchaguzi. Usiseme jambo ambalo litakufanya uwe mtumwa baada ya uchaguzi. ⁠Atakayekubali kushindwa ndiye mshindi.”

“Chadema ina mashabiki wengi kuliko wanachama. CCM ina wanachama wengi kuliko mashabiki. Mgogoro wa Chadema hauamuliwi na wanachama kwa haki. Mgogoro wa CCM unaamuliwa na dola – si wanachama wala mashabiki,”aliandika Askofu Bagonza.

Mwananchi limezungumza na mwanahabari mkongwe na mchambuzi wa siasa, Absalom Kibanda kupata mtazamo wake wa kinachoendelea,  ambapo amesema kuelekea uchaguzi mkuu wa Chadema, watetezi au wanaomuunga mkono Mbowe na Lissu wanatakiwa kujipanga kwa hoja  endapo vigogo hao watachuana pamoja.

“Lakini pia Chadema wanatakiwa kufanya uchaguzi wa kidemokrasia ili yeyote atakayeshinda ajenge mustakabali wa Chadema.Isipokuwa wakifanya kosa kama walilolifanya NCCR- Mageuzi la kumtoa Marando (Mabere) kwa fitina, basi mwaka 2025 Chadema itafika ikiwa hoi.

“Lakini kingine Mbowe anatakiwa aje na hoja za kuthibitisha kwanini anataka kuwania uenyekiti kwa miaka mitano mingine ijayo. Kuna maneno yanasemwa yakidai hana jipya na siasa zake za kunja ngumi, sasa aje na vitu vipya,” alisema Kibanda.

Kibanda aliongeza:”Mbowe amekuwa akiijenga Chadema kwa vitu vipya, sasa aje navyo, kwa sababu siasa za kunja ngumi hazimsaidii tena, aje na vision  (dira) mpya,” alieleza.

Kwa mujibu wa Kibanda kila inapofika uchaguzi mkuu wa Chadema,  kunakuwa na minyukano kuanzia mwaka 2009 kati ya Mbowe na Zitto Kabwe, mwaka 2014 Mbowe na Zitto tena na mwaka 2019.

“Kila unapofika uchaguzi mkuu kuna minyukano ambayo bahati mbaya au nzurii inawapa nafasi Chadema ya kufuatiliwa sana. Mara nyingi minyukano hii inamgusa Mbowe.

“Ni kweli Mbowe amedumu muda mrefu, lakini ni ukweli ameshiriki kuijenga Chadema kwa muda mrefu. Minyukano imechochewa zaidi na chaguzi za Chadema za kanda  na madai ya safu kupangwa maeneo hayo ili kupata uungwaji mkono,” amesema.

Duru za siasa kutoka Chadema zinaeleza, Lissu ameamua kubadili uamuzi wa kutetea nafasi ya umakamu mwenyekiti kwa kile anachodai hatua ya Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria, Ezekiel Wenje kutangaza kuwania umakamu mwenyekiti-bara, kuna baraka za uongozi wa juu.

“Lissu anadai kwa nini Wenje atangaze kugombea umakamu, anaona kabisa ametumwa, sasa anasema kuliko kushindwa na Wenje basi wacha akachuane  kwenye uenyekiti,” kimedai chanzo chetu.

Agosti 5, 2024, Wenje aliyewahi kuwa Mbunge wa Nyamagama alitangaza nia ya kuwania umakamu mwenyekiti-Bara akisema amejiona anatosha kuwa msaidizi wa Mbowe.

Wenje alisema baada ya tafakuri ya muda ameona ana uwezo wa kuwa msaidizi wa karibu wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye duru za kisiasa zinaonyesha atagombea tena uenyekiti kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

“Kutokana na uzoefu nilionao chamani, nimejitathimini kuwa nina uwezo wa kuwa msaidizi wa Mbowe, naomba ifahamike chama chetu cha Chadema kimekuwa kikijipambanua siku hadi siku katika kupigania haki za watu, ikiwemo uhuru, haki na maendeleo,” alisema.

‘Nendani mkakubaliane kwanza’

Hatua hiyo ya Lissu kutaka kuonesha nia ya kushindana na Mbowe iliibuka katika kikao cha kamati kuu iliyoketi Desemba 2, 2024 makao makuu ya chama hicho, Mikocheni, Dar es Salaam.

Taarifa zinadai, kamati kuu hiyo iliwataka Mbowe, Lissu na baadhi ya wajumbe kwenda kukaa na kujadiliana kwa pamoja ili kuwa na maridhiano ya kukinusuru chama na mpasuko mkubwa.

“Haiwezekani chama kwenda kwenye uchaguzi Mbowe na Lissu wakigombania nafasi moja. Tumewaeleza wakae na kukubaliana nani agombee nani asigombee.

“Wote hawa tunawahitaji. Lakini kuingia kwenye uchaguzi na hawa jamaa, ni hatari na hatuwezi kubaki salama na ikizingatiwa mwakani ni uchaguzi mkuu,” alidokeza mmoja wa wajumbe wa kamati kuu.

Taarifa zingine zilidai katika kikao cha kamati kuu, iliamualiwa viongozi wakuu waketi kuzungumza kwa pamoja, ili kupata mwelekeo sahihi wa kuhakikisha Chadema inasonga mbele.

Iliamuliwa kikao hicho kiwe na Mbowe, Lissu, Mnyika na naibu makatibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na Benson Kigaila (Bara). Hata hivyo, Lissu alitaka wawe watatu, manaibu waondolewe.

Taarifa zaidi zinadai kiongozi mmoja mkubwa wa dini jina limehifadhiwa aliitwa katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa siku tatu kuanzia Jumatano.

Hata hivyo, katika mazungumzo hayo Lissu aliweka msimamo wake wa kuwania uenyekiti, wakati inaelezwa Mbowe hakuweka wazi kama atagombea au atawania urais mwakani.

Desemba 6, 2024 Mwanachi lilipomtafuta Lissu juu ya taarifa hizo za kutaka kufanya mkutano kutangaza nia yake alisema: “No comment (sina la kusema). Ninachotaka kukwambia ni kwamba, wakati utakapofika nitakujulisha au utajulishwa.”

Hata hivyo, Mbowe hakupatikana lakini Jumanne hii ya Desemba 10, 2024 atakuwa na mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Pamoja na mambo mengine suala hilo linatarajiwa kuibuka.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema lengo la mkutano huo ni kutoa mrejesho wa maazimio ya kamati kuu , kutoa maazimio ya Kikao cha kamati kuu juu ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongozi uliofanyika Novemba 27, 2022 ulioshuhudia CCM ikiibuka na ushindi wa asilimia 99.

Mchungaji Msigwa ahusishwa

Katika minyukano hiyo ya makada wa Chadema, aliyekuwa mwenyekiti wa kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa ambaye Juni 30, 2024 alitangaza uamuzi wa kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) amekuwa akihusishwa kwenye uamuzi huo wa Lissu.

Mchungaji Msigwa ambaye akiwa Chadema alikuwa miongoni mwa marafiki wakubwa wa Lissu, anaelezwa ndiye yuko nyuma ya mkakati wa Lissu kuchuana na Mbowe na ndiye anawapigia simu baadhi ya watu kuwashawishi kumuunga mkono.

Mbunge huyo wa zamani wa Iringa Mjini (2010-2020) inaelezwa kwenye mijadala anapanga mikakati hiyo na baadhi ya wajumbe wengine wa kamati kuu,  ambao ni marafiki na ikiwezekana mbele ya safari wakajiunge na CCM.

Mwananchi lilipomtafuta Mchungaji Msigwa juu ya kuhushishwa kwake na mpango huo na madai hayo mengine, alisema: “Wanaosema hivyo hawajielewi, mimi nimfanyie kampeni Lissu kwa masilahi gani? Nipo chama tawala, kwa hiyo yoyote kati yao, ni  hasimu wangu kisiasa.

“Nimfanyie Lissu kampeni ili iweje? Ni watu  waliokosa hoja na wameshindwa kumtetea mwenyekiti wao aliyedumu muda mrefu, kwa hiyo wanatafuta mtu wa kumfia. Hayo ni matatizo yao wasinihusishe mimi,” alisema Mchungaji Msigwa.

Mmoja wa wanamuunga mkono Lissu ni aliyekuwa mgombea wa uenyekiti wa Kanda ya Pwani, Gervas Lyenda ambaye aliandika ujumbe kwenye akaunti yake yake ya X akiambatanisha na picha ya Mbowe akisema:

“Ameongoza mapambano akiwa mwenyekiti wa Chadema kwa takribani miaka 20 tangu 2004. Mbowe, mwamba wa siasa za upinzani aliyeweka alama kubwa kwenye siasa za Tanzania.

“Ni muda wake wa kung’atuka kwenye kiti? a good dancer must know when to leave a stage. (mchezaji mzuri ni yule anayejua lini ataondoka jukwaani)

Akifafanua maana ya ujumbe huo, alipozungumza na Mwananchi Lyenda alisema kuwa aliuliza tu kama mwenyekiti wao ana kitu kingine anachoweza kukifanya ambacho hakukifanya ndani ya miaka yake 20.

“Bado nina shaka kama anacho tutajua, lakini jambo kubwa ni kwamba unaweza kuweka alama kubwa, lakini usipokuwa na muda mzuri wa kuondoka, alama yako itaharibika, kwa sababu ukikaa muda mrefu wanaokupinga wanaongezeka wanaokuona kama mchoyo wa madaraka, na huoni mtu atakayevaa viatu vyako,” alisema.

Lyenda alisema mtu makini anajua muda sahihi wa kuondoka haijalishi wapambe wanakushauri nini.

“Kwa tulipofika na CCM tunamhitaji mtu kama Lissu ili kwenda  sambamba na chama tawala,” alisema Lyenda.

Kada mwingine aliyeweka  bayana kumuunga mkono Mbowe kwenye moja ya mijadala mitandaoni alisema:

“Kuna heshima inatakiwa kuwekwa na kuondoa hizi kelele za hapa na pale. Tunataka kuweka viwango vya kuheshimiana baada ya uchaguzi huu.”

“Binafsi natamani kumuona Tundu Lissu akichukua fomu ya kugombea uenyekiti. Nafikiri sasa ni wakati wake sahihi kugombea uenyekiti wa chama chetu. Tunataka asaidiwe kwa vitendo kwa kumuonesha tafsiri nzuri ya uchaguzi,” amesema na kuongeza:

“Uchaguzi wa ushindani. Ushindani ndani ya chama. Uchaguzi wenye joto kali. Uchaguzi ambao utamlazimisha kuheshimu mtu/watu muhimu katika siasa zetu. Atafundishwa namna ya kufanya kampeni na kushinda uchaguzi ndani ya chama. Nasisitiza, lengo liwe uchaguzi tu, siyo kuondoka Chadema au kustaafu siasa.”

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917

Related Posts

en English sw Swahili