Medo matumaini kibao Kagera sugar

KOCHA wa Kagera Sugar, Melis Medo, ameweka wazi kuwa anaona dalili za maendeleo katika kikosi chake baada ya kuvuna pointi tano katika michezo minne ya hivi karibuni ya Ligi Kuu Bara.

Medo aliyeiongoza timu hiyo juzi jioni kuvaana na Tanzania Prisons na kulazimishwa suluhu nyumbani alisema kuwa, licha ya timu yake kupata matokeo hayo, bado wana kazi kubwa mbele yao ili kumaliza msimu wakiwa nafasi za juu.

Kagera imevuna pointi tano kwa kushinda dhidi ya Dodoma Jiji kwa mabao 2-1, kutoa sare mbili dhidi ya Mashujaa (1-1) na Tanzania Prisons (0-0) na kupoteza mbele ya Azam FC kwa bao 1-0.

“Matokeo haya yanaonyesha mwelekeo mzuri lakini bado tunahitaji kufanya kazi zaidi ili kuboresha michezo yetu. Hatuwezi kuridhika na hapa, kuna mengi ya kuboresha,” alisema Medo.

Suluhu dhidi ya Tanzania Prisons mchezo uliochezwa majuzi umeiweka Kagera Sugar katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na sasa wana pointi 10. H

Hata hivyo, Medo alisisitiza kuwa bado wana kazi kubwa ya kufanya ili kutorudi nyuma, kwani wanahitaji pointi nyingi zaidi ili kujiepusha na hatari ya kushuka daraja.

“Vita yetu bado ni kubwa, lakini kila mchezo unavyopita tunaendelea kujifunza na kujiimarisha. Lengo letu ni kutoka katika nafasi hii na kujihakikishia nafasi salama kwenye ligi,” alisema Medo.

Kagera ambayo ilianza msimu kwa kusuasua inahitaji kuendelea kupigana ili kujiepusha na hatari ya kushuka daraja, huku Medo akisisitiza morali ya wachezaji inazidi kuongezeka na wanajitahidi kutimiza malengo.

Related Posts