Mitazamo tofauti ya wadau panga-pangua ya Rais Samia

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kupanga safu ya wasaidizi wake kwenye nafasi mbalimbali ikiwemo kuligusa kwa mara nyingine baraza lake la mawaziri.

Katika mabadiliko hayo, Rais Samia ameirejesha wizara ya zamani ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Awali, majukumu ya sekta ya habari yaliunganishwa kwenye Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Kwa mabadiliko hayo yaliyotangazwa leo Jumapili, Desemba 8, 2024, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo itaongozwa na Profesa Palamagamba Kabudi ambaye awali, alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Profesa Kabudi anapewa dhamana ya kuongoza wizara hiyo ikiwa ni siku 116 tangu aliporejea rasmi katika baraza la mawaziri baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria Agosti 14, 2024

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, itaongozwa na Waziri Jerry Silaa ambayo awali ilijulikana kama Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ilianzishwa Septemba 12, 2021 na Rais wa Samia Suluhu Hassan, baada ya maoni na mapendekezo ya wadau wa habari kutaka sekta hiyo kuwa na wizara mahususi inayojitegemea.

Wizara iliunganisha majukumu yaliyokuwa yakitekelezwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hapo awali na Idara ya Habari ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Katika mabadiliko hayo, Innocent Bashungwa ambaye alikuwa Waziri wa Ujenzi sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani akichukua nafasi ya Waziri Hamad Masauni ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira.

Masauni amechukua nafasi iliyoachwa na Waziri, Dk Ashatu Kijaji ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uchuvi akimrithi Waziri Abdallah Ulega aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi akichukua nafasi ya Bashungwa.

Bashungwa amehudumu ndani ya wizara ya ujenzi kwa siku 466 tangu alipotolewa katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alipokuwa kihudumu kama Waziri. Bashungwa amekuwa miongoni mwa mawaziri wa Rais Samia anaowahamisha hamisha.

Wizara nyingine ambazo Bashungwa amezihudumu kwa vipindi tofauti ni Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Wizara ya Viwanda na Biashara, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na sasa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Dk Ndamas Ndumbaro aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo amerejeshwa kwenye wizara aliyowahi kuiongoza ya Katiba na Sheria, akichukua nafasi ya Profesa Kabudi.

Msigwa arejeshwa tena, mabalozi…

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemteua Gerson Msigwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kumrudisha tena katika nafasi ya Msemaji Mkuu wa Serikali ikiwa ni siku 442 tangu alipotolewa katika nafasi hiyo.

Septemba 23, 2023, Rais Samia alimteua Msigwa kuwa Katibu Mkuu na nafasi ya Msemaji Mkuu wa Serikali ilijazwa Oktoba 2, 2023 kwa Mobhare Matinyi kuteuliwa. Matinyi alihudumu kwa siku 257 kabla ya nafasi hiyo kuchukuliwa na Thobias Makoba.

Makoba aliteuliwa na Rais Samia Juni 15, 2024. Rais Samia alisema Matinyi atapangiwa kazi nyingine. Katika mabadiliko ya sasa ya Rais Samia amewateua Matinyi na Makoba kuwa mabalozi ambao vituo vya kazi vitatangazwa baadaye.

Wengine walioteuliwa kuwa mabalozi ni Anderson Mutatembwa, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad, Kamishna wa Polisi, Suzan Kaganda.

Oktoba 24, 2024, Rais Samia alimpandisha cheo Kaganda kutoka kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi hadi Kamishna na kumteua kuwa Kamishna wa Utawala na Raslimali Watu wa Jeshi la Polisi.

Rais Samia amewateua James Kilabuko kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) huku Dk Stephen Nindi akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo anayeshughulikia masuala ya Ushirika na Umwagiliaji.

Dk Suleiman Serera amehamishwa kutoka Wizara ya Kilimo kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara huku taarifa hiyo ikieleza Dk John Simbachawene atapangiwa kituo cha kazi.

Pia uteuzi huu umemgusa, Profesa Mohamed Janabi ambaye ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais Masuala ya Afya na Tiba huku akiendelea na  majukumu yake ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)

Wateuliwa wote wataapishwa Jumanne, Desemba 10, 2024 saa 5 asubuhi, Ikulu ndogo, Tunguu Zanzibar.

Walichokisema wadau wa habari

Akitoa maoni yake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tan) Edwin Soko amesema mabadiliko hayo yanalenga kuimarisha ufanyaji kazi wa Serikali.

Kuhusu kurejeshwa kwa majukumu ya sekta ya habari kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenda Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema: 

“Mwanzo tulidhani kupelekwa sekta ya habari katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya habari ni kuweka vyombo viwili kwa pamoja yaani TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) na Habari Maelezo vinavyosimamia sekta ya habari.

“Wadau tukapeleka mapendekezo ya kwamba vyombo vya habari vinavyosimamia sekta ya habari vikae sehemu moja ndio maana ikaletwa Wizara ya Teknolojia na Mawasiliano.

“Maoni yangu ni kwamba itapunguza ufanisi kiutendaji sasa sijui Rais anapima ufanisi wa utendaji wa ngazi za mawaziri ingawa maoni ya wadau walitaka vyombo vinavyosimamia sekta ya habari vikae sehemu moja,” amesema.

Amesema jambo hili litakuwa linachelewesha uamuzi kwa kuwa hadi yafanyike katika wizara mbili tofauti.

Amesema faida iliyopo ni kuongea lugha ya kisheria katika sekta ya habari kwa kuwa ana uzoefu na sekta hiyo. 

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Deodatus Balile limesema wamepokea mabadiliko hayo kwa moyo mmoja. Awali tuliomba sekta ya habari ihamishwe katika wizara hii kutokana na kwamba ilionekana kumezwa na sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambapo mawaziri wengi waliipa kisogo sekta ya habari.

“Rais imempendeza kuirejesha huko, tunaamini waliopewa dhamana hawataiweka kando sekta ya habari kama ilivyokuwa awali,” amesema Balile.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura amesema wasiwasi wake ni muundo wa sekta ya habari baada ya kurejeshwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, huku ikiachwa Wizara ya Teknolojia ya habari ambapo ndipo kuna vyombo kama televisheni, redio na mitandao kunakuwa kama kuna mchanganyiko. 

“Kuna kamchanganyiko kidogo. Tuone namna ya kuunganisha TCRA na Habari Maelezo ili kuwa na chombo kimoja kinachosimamia masuala ya habari,” amesema.  

Amesema sekta ya habari kuliko kuiunganisha ni heri ikapewa uzito: “Ushauri wangu ni kwamba tuyape heshima mambo ya habari kwa sababu ni muhimili wa nne usiokuwa rasmi kuwa wizara inayojitegemea,” amesema Sungura.

‘Watu wanaishi kwa wasiwasi’

Mabadiliko hayo yamepokewa kwa mitazamo tofauti na wadau ambapo Dk Hellen Bisimba amesema panga pangua hii inafanya watu kuishi kwa wasiwasi, kushindwa kuanzisha mipango ya muda mrefu na kuitekeleza kwa kuhofia kutolewa kabla hawajafikia malengo.

Dk Bisimba aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) amesema, “Dk Ndumbaro alitolewa hata miezi haijapita amerudishwa, hawawezi kufanya kazi kwa kujiamini, hii inafanya mambo mengi yanaanza lakini hayafanikiwi, watu hawawezi kukaa kazini kwa kujiamini.

Amesema hali hii pia huweza kuibua wasiwasi kwa baadhi ya watu wanaofuatilia huku akitolea mfano wa kuteuliwa kwa makamanda wa polisi na kupewa ubalozi usiokuwa na vituo.

 “Hata watu wanaowazunguka akitolewa mtu wanakuwa na maswali akirudi tena wanakuwa na maswali, halafu watu ni walewale ni kama wanajaribu,” amesema.

Kwa upande wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe kilichofanyika ni uamuzi wa kawaida unaolenga kuboresha ufanisi wa utendaji.

Uamuzi wa mabadiliko hayo, alisema aghalabu hufanyika kutokana na ukweli kwamba mamlaka ya uteuzi inaridhishwa na weledi wa mtendaji, isipokuwa katika nafasi tofauti na aliyopewa awali.

(Imeandikwa na Aurea Simtowe, Jumaa Issihaka na Sute Kamwelwe)

Related Posts