Mlugu, Simbu kuchuana uenyekiti Kawata, Saliboko ajiengua

Nyota wa Riadha, Alphonce Simbu na mwanajudo bingwa wa Taifa, Andrew Thomas Mlugu ni miongoni mwa wagombea watatu wanaochuana kuwania uenyekiti wa Kamisheni ya Wachezaji Tanzania (Kawata).

Mwingine ni Omar Bakari Omar anayewania nafasi hiyo kwenye uchaguzi unaofanyika leo Desemba 8, 2024 mjini Dodoma ukisimamiwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Muogeleaji, Collins Saliboko aliyekuwa pia akiwania uenyekiti amejiengua.

Nafasi ya  katibu mkuu inawaniwa na Andrew Rhobi na Mohammed Khamis Kassim huku wagombea wanane wakichuana kuwania ujumbe wa Kamisheni hiyo.

Wagombea kwenye nafasi ya ujumbe ni Faraja Damas, Failuna Abdi, Josephat Gisemo, 
Khamis Hussein Ali, Hisham Mzee Amour, Salma Juma Rajabu, Rauhma Hassan Suluhu na Nyanzinge Said Yatabu huku Joseph Panga naye akijiengua.

Katika hatua nyingine, wagombea 11 wamejitosa kuwania uongozi wa Olimpians katika uchaguzi utakaofanyika Jumanne ya Desemba 10, 2024.

Wagombea hao ni Tasir Kitisa anayewania uenyekiti akiwa mgombea pekee kwenye nafasi hiyo inayoshikiliwa na Gidamis Shahanga anayemaliza muda wake.

Nguli wa riadha, Suleiman Nyambui ni mgombea pekee kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti akitetea kiti chake.

Kwenye ukatibu, bingwa wa zamani wa Afrika wa mbio za mita 800, Samwel Mwera anachuana na muogeleaji nguli,  Khalid Rushaka.

Katibu anayemaliza muda wake, Mwinga Mwanjala amesema wagombea wengine saba wanachuana kuwania nafasi tatu za ujumbe.

Wagombea hao ni Restitution Joseph, Mosi Ally, Failuna Matanga, Andrew Thomas Mlugu, Zakaria Barie, Samwel Kwang na Zakia Mrisho.

Wapiga kura kwenye uchaguzi huo ni wale wanamichezo wote waliowahi kushiriki michezo ya Olimpiki kuanzia 1964 Tanzania iliposhiriki kwa mara ya kwanza ikijulikana kama Tanganyika.

Related Posts