Mvua yawaliza walima tumbaku Chunya wajipanga upya kimkakati

Chunya. Wakulima wa tumbaku katika Kata ya Lupa, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, wamesema mabadiliko ya tabianchi yameathiri uzalishaji wa zao hilo.

Wanasema hali hiyo imesababisha kutofikiwa kwa lengo la msimu uliopita huku wakisema katika msimu mpya wa kilimo, wamepanga mikakati madhubuti itakayosaidia kuongeza uzalishaji.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku (Mtanila Amcos), Isaya Hussen, matarajio ya msimu wa 2023/24 yalikuwa kuzalisha kilo milioni 1.6 za tumbaku.

Hata hivyo, uzalishaji ulipungua hadi kilo milioni 1.5, sawa na asilimia 96.4 ya malengo, kutokana na mvua nyingi zilizonyesha na kusababisha hasara kwa wakulima.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka uliofanyika leo Jumapili Desemba 8, 2024, Hussen ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Chunya (Chutcu), amesema mkutano huo ulioanza jana na kuhitimishwa leo, ulikuwa na ajenda za kujadili changamoto za msimu uliopita, taarifa za mapato na matumizi na maandalizi ya msimu wa 2024/25.
Hussen amesema mvua nyingi zilisababisha mabani ya kukaushia kubomoka, mashamba kufurika maji na wakulima kupata hasara, ni moja ya agenda zilizojadiliwa na kuwekewa mkakati.

Hata hivyo, kwa msimu mpya amesema wamepanga kuongeza uzalishaji hadi kufikia kilo milioni 2.1, iwapo hali ya hewa itakuwa nzuri.

“Tumepokea asilimia 100 ya mbolea ya NPK, huku CAN na UREA zikipatikana kupitia mfuko wa pembejeo wa wanachama. Pia, tumepanda miti 375,000 aina ya Albizia na mikaratusi ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa,” amesema Hussen.

Kwa upande wa uwajibikaji kwa jamii, chama hicho kimetoa msaada wa madawati 15, meza mbili, vitanda vitano, kompyuta mpakato na mashine ya kudurufu karatasi kwa shule za msingi na sekondari, vyote vikiwa na thamani ya Sh3.5 milioni.

Kauli za wadau
Mkulima Alfredy Juma amesema msimu huu wakulima wamejiandaa vyema kwa matarajio ya uzalishaji wenye tija. “Tunajivunia juhudi za uongozi wetu katika kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo,” amesema.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Chunya, Anacret Michombero amepongeza Mtanila Amcos kwa kuwa ushirika wa mfano unaoigusa jamii na kutoa mchango mkubwa katika uzalishaji wa tumbaku.

Ofisa kutoka Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku Chunya (Chutcu), Juma Shinshi amesema amcos hiyo ni miongoni mwa vyama vya msingi 33 vilivyozalisha kilo milioni 1.5 za tumbaku msimu wa 2023/24.

Ofisa Tarafa wa Kipembawe, Kassim Salum amesema chama hicho kimepata hati safi kwa miaka minne mfululizo kutokana na usimamizi bora wa rasilimali.

Pia, amesifu juhudi zake katika kuboresha huduma za kijamii, kama vile kuchangia vifaa kwa shule, hatua inayosaidia kuongeza ubora wa elimu na kupunguza utoro wa wanafunzi.

Related Posts