Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Aman Simbayao aliyefariki dunia kwa kushambuliwa na wananchi wenye hasira eneo la Tegeta kwa Ndevu, jijini Dar es Salaam, umeagwa leo Jumapili Desemba 8, 2024 jijini Dar es Salaam.
Shughuli ya kuaga mwili huo imefanyika viwanja vya michezo vya TRA Kurasini kuanzia saa 6 mchana na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliwaongoza waombolezaji kuaga mwili huo.
Simbayao ni miongoni mwa maofisa watatu walioshambuliwa na wananchi eneo la Tegeta kwa Ndevu, usiku wa Desemba 5, 2024 ambao walizuia gari aina ya BMW x6 lililodaiwa kutokuwa ndani ya mfumo wa mamlaka hiyo.
Watumishi hao wa TRA walipojaribu kulizuia gari hilo, kuliibuka mzozo hadi dereva akapiga kelele kuomba msaada akidai anatekwa, jambo lililosababisha wananchi kuwashambulia kwa mawe maofisa hao.
Siku moja baadaye, Desemba 6, 2024, Simbayao alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Tukio hilo la kushambuliwa kwa ofisa huyo akiwa na wenzake wawili, lilitokea usiku wakati watumishi hao wakiwa kwenye gari la Serikali.
Waziri Nchemba aliongozana na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Shughuli ya kuaga mwili huo ilianza saa 6 mchana, ikiambatana na salamu mbalimbali kutoka kwa viongozi hao, kabla ya heshima za mwisho kutolewa.
Baada ya heshima za mwisho, mwili wa Simbayao ulisafirishwa kwenda Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro kwa maziko.
Moshi Kabengwe, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TRA, akisoma wasifu wa marehemu, alisema alizaliwa Aprili 3, 1985 Malinyi mkoani Morogoro
Mwaka 2013 alisoma udereva na 2018 alijiendeleza katika fani hiyo katika Chuo cha Usafirishaji (NIT).
Alipata ajira TRA Septemba Mosi, 2019 kama deveva daraja la pili kituo chake cha kazi kikiwa mkoani Shinyanga.
Mwaka 2022 alihamishiwa Dar es Salaam ili apate muda wa kuhudhuria mafunzo chuo cha CBE.
Alikuwa kwenye kitengo cha forodha na ushuru wa biashara na Juni mwaka huu, alipandishwa cheo na kuwa dereva daraja la kwanza.
Hadi mauti inamkuta, alikuwa ameitumikia TRA kwa miaka sita.
Shughuli hiyo ya kuagwa mwili wa Simbayao imefanyika wakati tayari Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam imetangaza kuwashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Juzi Jumamosi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Kamanda Jumanne Muliro akizungumza na waandsishi wa habari kuhusu tukio hilo, aliwataja inaowashikilia kuwa ni Deogratius Masawe na Bakari Idd (wabeba mizigo), Omary Issa (mpiga debe) na Rashid Mtonga (mwendesha bodaboda) kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Simbayao.
“Watuhumiwa hawa wakati wakiwashambulia maofisa hao waliharibu pia gari la TRA. Tukio hili lilitokea baada ya maofisa hawa kukamata gari ambalo lilidaiwa kuwa na makosa ya kikodi,” alisema Muliro.
Muliro alisema watumishi hao wa TRA walikuwa wakitekeleza jukumu hilo kisheria kwa kufuata taratibu zote dhidi ya mtuhumiwa.
Hata hivyo, alisema lilijitokeza kundi la watu, wakiwemo watuhumiwa wanne walioshambuliwa kwa mawe. na baadaye kusababisha kifo cha Simbayao.