Mwigulu kuongoza waombolezaji kumuaga ofisa wa TRA aliyeuawa

Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Aman Simbayao aliyefariki dunia kwa kushambuliwa na wananchi wenye hasira eneo la Tegeta kwa Ndevu, jijini Dar es Salaam, utaagwa leo Jumapili, Desemba 8, 2024.

Shughuli ya kuaga mwili huo itafanyika viwanja vya michezo vya TRA Kurasini kuanzia saa 6 mchana na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba anatarajia kuwaongoza waombolezaji kuaga mwili huo.

Simbayao ni miongoni mwa maofisa watatu walioshambuliwa na wananchi eneo la Tegeta kwa Ndevu, usiku wa Desemba 5, 2024 ambao walizuia gari aina ya BMW x6 lililodaiwa kutokuwa ndani ya mfumo wa mamlaka hiyo.

Watumishi hao wa TRA walipojaribu kulizuia gari hilo, kuliibuka mzozo hadi dereva akapiga kelele kuomba msaada akidai anatekwa, jambo lililosababisha wananchi kuwashambulia kwa mawe maofisa hao.

Siku moja baadaye, Desemba 6, 2024, Simbayao alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Tukio hilo la kushambuliwa kwa ofisa huyo akiwa na wenzake wawili, lilitokea usiku wakati watumishi hao wakiwa kwenye gari la Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumapili, Desemba 8, 2024 na TRA shughuli hiyo, Waziri Nchemba anatarajiwa kuongozana na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shughuli ya kuaga mwili huo itakapoanza saa 6 mchana itaambatana na salamu mbalimbali kutoka kwa viongozi hao, kabla ya heshima za mwisho kutolewa.

Baada ya heshima za mwisho, mwili wa Simbayao utasafirishwa kwenda Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro kwa maziko.

Shughuli hiyo ya kuagwa mwili wa Simbayao inafanyika wakati tayari Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam imetangaza kuwashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.

Jana Jumamosi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Kamanda Jumanne Muliro akizungumza na waandsishi wa habari  kuhusu tukio hilo aliwataja inaowashikilia kuwa ni Deogratius Masawe na Bakari Idd (wabeba mizigo), Omary Issa (mpiga debe) na Rashid Mtonga (mwendesha bodaboda) kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Simbayao.

“Watuhumiwa hawa wakati wakiwashambulia maofisa hao waliharibu pia gari la TRA. Tukio hili lilitokea baada ya maofisa hawa kukamata gari ambalo lilidaiwa kuwa na makosa ya kikodi,” alisema Muliro.

Muliro alisema watumishi hao wa TRA walikuwa wakitekeleza jukumu hilo kisheria kwa kufuata taratibu zote dhidi ya mtuhumiwa, lakini lilijitokeza kundi la watu, wakiwemo watuhumiwa wanne walioshambuliwa kwa mawe na baadaye kusababisha kifo cha Simbayao.

Related Posts