Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameonya kuhusu ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza, akisema hali ni mbaya na huenda ikazidi kuwa mbaya zaidi endapo hatua hazitachukuliwa na watu kutozingatia afya za miili yao.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Desemba 8, 2024, wakati wa matembezi ya pamoja yaliyoandaliwa na Pharm Access kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, kama sehemu ya kampeni maalumu ya kuhamasisha jamii kufanya mazoezi mara kwa mara kupambana na magonjwa hayo.
Amesema mazoezi yana mchango mkubwa katika kuimarisha afya, akieleza kuwa tafiti nyingi zimeonyesha kuwa mazoezi yanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kupata magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.
Aidha, Rais Mwinyi amesema takwimu zinaonyesha ongezeko kubwa la magonjwa hayo, hivyo ni muhimu kuchukua hatua za makusudi ili kukabiliana nayo.
“Takwimu zinaonyesha ufanyaji wa mazoezi na kuishughulisha miili umeshuka kutoka asilimia 52 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 33 mwaka 2013, ugonjwa wa kisukari umepanda kutoka asilimia 3.8 mwaka 2011 hadi asilimia 7.5 mwaka 2023,” amesema Dk Mwinyi.
Kwa upande wa shinikizo la damu, imepanda kutoka asilimia 33 mwaka 2011 hadi asilimia 43 mwaka 2023, uzito na unene kupitiliza vimepanda kufikia asilimia 43.4 kutoka asilimia 36.6 huku matumizi ya tumbaku yamepanda kutoka asilimia 7.3 mwaka 2011 hadi kufikia asilia 10.3 mwaka 2023.
Katika jitihada za kukabiliana na magonjwa ya saratani, Dk Mwinyi ameweka wazi kuwa Serikali ya Zanzibar inashirikiana na taasisi binafsi kupitia mradi wa miaka mitano wa uchunguzi wa saratani na utoaji wa matibabu kwa wananchi.
Amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa jamii ikilenga kufanikisha uchunguzi wa awali, kuwajengea uwezo wahudumu wa afya na kujenga kituo cha umahiri cha saratani.
“Wizara inaendelea kuhakikisha huduma bora zinapatikana katika hospitali na vituo maalumu. Kwa sasa, jumla ya vituo 60, vikiwemo 36 Unguja na 24 Pemba, vinatoa huduma hizo,” amesema Dk Mwinyi.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote kuthamini umuhimu wa mazoezi, kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta na wanga sambamba na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya kuhusu lishe bora.
Amesisitiza pia umuhimu kwa watu kufanyiwa vipimo vya mara kwa mara ili kujua hali ya afya zao.
“Mazoezi yana faida si tu kwa kuboresha afya ya mwili, bali pia kuimarisha afya ya akili, kupunguza msongo wa mawazo, kuboresha usingizi, na kuongeza furaha. Matembezi ya pamoja yanasaidia kuimarisha mshikamano na uhusiano wa kijamii. Ni muhimu kuyaendeleza kwa kuandaa utaratibu maalumu,” ameongeza.
Naye Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Pharm Access, Dk Heri Marwa amesema tangu mwaka 2023 walianza kufanya kazi na SMZ, ushirikiano huo umesababisha kuwapo kwa afua mbalimbali kutekelezwa kisiwani humo na kuwafikia watu mbalimbali.
Amesema tatizo la magonjwa hayo limekuwa janga duniani Tanzania ikiwamo likishabihiana na ulivyoanza ugonjwa Ukimwi mwanzoni mwa miaka 1980.
“Nasema unashabihiana kwa sababu wakati ugonjwa wa Ukimwi unaingia nchini kulikuwa na dhana kuwa ni kwa ajili ya watu fulani na sio kwa jamii yote, ilikuwa inaaminika kwamba watu wanaofanya biashara na watu wenye uwezo wa kifedha na wale wanaouza miili ndio watu wanaoweza kuupata,” amesema Dk Marwa na kuongeza;
“Matokeo ya dhana hiyo yametufanya tujikute tunakaribisha janga ambalo limesababisha majanga makubwa kwenye nchi na dunia kwa ujumla hasa kwenye nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.”
Amesema tofauti kubwa kati ya magonjwa yasiyoambukiza na Ukimwi; “Ukimwi kuna fedha nyingi ambazo zimetoka nje ya nchi kuja kupambana nao, lakini kwa magonjwa hayo tusitegemee msaada huo kwa sababu hayaambukizi na wenzetu walishaanza kufanya mazoezi kwa hiyo ni suala la sisi kuchukua hatua za kujikinga na kuilinda jamii yetu kwa ujumla.”
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Mngereza Miraji Mzee amesema Serikali inachukua jitihada kuimarisha sekta ya afya na vituo vya afya na ujenzi vituo vipya 35 vya afya.
Waziri wa Afya, Ahmed Mazrui amesema dhamira ya Serikali ni kuona wananchi wana afya nzuri na bora kwani maradhi hayo yamekuwa sugu na kuongezeka siku hadi siku.
Amesema wanahamasisha jamii kufanya mazoezi kwani kwa sasa sio tu jambo la kupenda bali kila mwananchi afanye.
“Tufanye mazoezi kwenye taasisi zetu vitambi basi, mazoezi yaanze na viongozi tuonyeshe mfano.
Amesema kila mwezi wizara itaweka utaratibu kufanya mazoezi ili kuonyesha njia.