Ramovic aigomea Yanga usajili dirisha dogo

KIKOSI cha Yanga jana usiku kilikuwa uwanjani kumenyana na MC Alger ya Algeria katika mechi ya pili ya Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku nyuma kocha mkuu wa timu hiyo akifanya mambo mawili kabla ya kikosi hakijarejea kujiweka tayari kwa pambano lijalo la ugenini pia dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.

Yanga iliyoanza kwa kupoteza nyumbani mbele ya Al Hilal ya Sudan kwa mabao 2-0, itaifuata Mazembe katika mechi ijayo ya CAF, ikiwa na rekodi tamu ya kupata ushindi jijini Lubumbashi katika mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika misimu miwili iliyopita na timu hiyo kufika hadi fainali ya michuano hiyo.

Kabla ya mechi hiyo ya jana usiku, huku nyuma mabosi wa Yanga walipelekewa dili mezani juu ya straika wa timu hiyo, Kennedy Musonda, lakini walipomjulisha Ramovic alitoa msimamo wa kuzuia dili hilo kwanza kwa sasa hadi kwanza ili amsome vyema Mzambia huyo akisema rekodi zake za timu ya taifa zinamsisimua mno.

Ipo hivi. wakati zimesalia siku chache dirisha dogo la usajili kufunguliwa, klabu ya Al Ittihad ya Libya, ilipiga honi Jangwani ikimtaka Musonda, lakini kocha Sead Ramovic, amegomea dili hili na kutoa sababu zake kwa mabosi wa klabu hiyo.

Mzambia huyo anayetumika Yanga kwa msimu wa tatu tangu alipotua klabuni dirisha dogo la Januari 2023, inadaiwa amewavutia Walibya kutokana na moto aliouwasha katika michuano ya kuwania kufuzu Afcon 2025 akiichezea timu ya taifa ya Zambiake ya Taifa.

Katika michuano hiyo fainali zake zitakazopigwa Morocco, Musonda amefunga jumla ya mabao na kuipeleka fainali hizo za mwakani, mabao hayo ni mengi kuliko hata yaliyofungwan na staa wa  Senegal, Sadio Mane anayemiliki matatu tu.

Musonda aliyafunga mabao mawili dhidi ya Sierra Leone, kisha kutupia mbele ya Ivory Coast na Chad, huku akiwa na rekodi tamu ya kufunga mabao matatu na kuasisti mara tatu wakati Yanga ikifika fainali za Kombe la Shirikisho Afrika misimu miwili iliyopita na msimu uliopita katika Ligi ya Mabingwa lifunga pia mabao matatu katika mechi 10 wakati Yanga ikiiishia robo fainali.

Takwimu za Musonda katika Ligi Kuu msimu uliopita zinaonyesha alicheza dakika 1116, alifunga mabao matano na asisti mbili akitumika katika mechi 22, alipiga mipira iliyolenga goli 16, iliyotoka nje tisa, huku kwa msimu huu katika mechi 11 za Yanga iliyovuna pointi 27, Mzambia huyo ametumika kwa dakika 322 akicheza mechi tisa na kufunga mabao matatu bila ya kuwa na asisti.

Sasa inaelezwa kutokana na rekodi hizo za kimataifa, Waarabu waliamua kugonga hodi Yanga kuona kama inaweza kupata saini ya Mzambia huyo kupitia dirisha dogo, huku ikijua kabisa kuwa msimu huu ndio mwisho wa mkataba wa staa huyo.

Al Ittihad ipo kundi B katika Ligi ya Libya ikishika nafasi ya nne ikicheza mechi 20 na kushinda tisa,sare 10 na kupoteza mara tatuikivuna jumla ya 28 na taarifa zinasema imeshatuma ofa hiyo ili kumbeba Musonda, lakini kocha Ramovic amechomoa.

Taarifa za ndani zinasema, ofa hiyo ilipotua kwa mabosi wa klabu hiyo, hawakuwa na hiana kwani mkataba wa staa huyo upo ukingoni, lakini zilipomfikia Ramovic, aliyetuma mwezi uliopita kuchukua nafasi ya Miguel Gamondi, alichomoa ofa hiyo.

“Kocha amezuia akisema hawezi kuruhusu jambo hilo…Ramovic amewaambia viongozi wa Yanga bado anataka kumsoma zaidi Musonda baada ya kuona vitu vinavyomsisimua na kumuaminisha Musonda ni bonge la straika na asingekuwa rahisi kumruhusu kuondoka,” kilisema chanzo hicho kutoka Yanga. “Mabosi wa Yanga nao wamekubaliana na maamuzi hayo kutokana na kuumizwa na namba za Musonda akiwa timu ya taifa akionekana kuwa mshambuliaji hatari vs namba za akiwa Yanga,” kiliongeza chanzo hicho.

Kocha huyo aliyeiongoza katika mechi mbili za kimataifa na moja ya ligi, amekuwa akionekana kumuelewa Musonda kwa kumtumia kwa dakika 90 za mechi ya Ligi dhidi ya Namungo na kumuingiza katika mechi ya kimataifa dhidi ya Al Hilal.

Kwa sasa ndani ya Yanga kuna washambuliaji wanne, huku wawili tu kati yao wakiwa na rekodi ya kufunga mabao na mmoja akiwa anaongoza kwa kucheza dakika nyingi.

Ikiwa chini ya Gamondi, Musonda alikuwa akikosa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza na katika dirisha la usajili ilielezwa angetemwa kabla ya kubakishwa dakika za lala salama baada ya Joseph Guede kuchomolewa na kwa sasa mkataba alionao unamalizika katika dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15 na kufungwa Januari 15.

Related Posts